RAIS Samia Suluhu Hassan amesema mrejesho alioupata katika ukusanyaji wa kodi ni kuwapo kwa malalamiko ya mianya ya ukwepaji wa kodi, makusanyo kidogo, huku mengi yakiingia mifukoni mwa watu.
Pia amesema baadhi ya watumishi wa serikali si waadilifu na kuna utaratibu usioridhisha katika utoaji wa misamaha ya kodi kwa wawekezaji.
Rais Samia aliyasema hayo jana Ikulu, Dar es Salaam, wakati akizindua Tume ya Rais ya Kutathmini na Kushauri Masuala ya Kodi.
“Hapa kuna malalamiko makubwa sana. Ni dhahiri kuna idadi kubwa ya sekta isiyo rasmi ambayo inakadiriwa zaidi ya asilimia 60 ya uchumi na hali hiyo inachangiwa na mfumo wa kodi kutovutia urasimishaji wa biashara na kutozingatia uleaji wa biashara zinazoanza. Hapa napo kuna tatizo,” alisema.
Rais alisema serikali inalenga kujenga uchumi jumuishi unaokua kwa kasi na kuimarisha ustawi wa watu kwa kuboresha huduma za jamii na kupunguza umaskini wa kipato kwa mtu mmoja mmoja.
Alisema mambo yanayotakiwa kufanywa ili kufikia hatua hiyo, kwanza ni amani na utulivu katika nchi ambapo Tanzania jambo hilo liko vizuri.
“Tunajaribu kuhakikisha nchi yetu inabaki na amani na utulivu na wakuu wa vyombo wapo hapa na tunawashukuru mmefanya hiyo kazi,” alisema.
Jambo la pili, Rais Samia alisema ni suala la mifumo ya haki inayoeleweka hali iliyosababisha kuunda tume ya kuangalia haki jinai ambayo ilifanya tathmini nchi nzima na kutoa mapendekezo.
“Kwa kiasi kikubwa mahakama wametekeleza vizuri, wako asilimia 70 ya utekelezaji lakini vyombo vingine navyo Jeshi la Polisi, DPP (Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali) na kwingine nako wanaendelea kutekeleza,” alisema.
Alitaja jambo la tatu ambalo linaifanya nchi itoke hatua moja kwenda nyingine ni mifumo mizuri ya kodi ili ilipwe kwa urahisi na kwa wakati bila misuguano.
“Wafanyakazi kila siku utasikia tupunguzie kodi kubwa na wafanyabiashara na wao malalamiko. Jambo la kodi halijawahi kuwa rahisi kutokana na ushirikiano na wadau mbalimbali. Serikali imeamua kulifanyia kazi suala la kodi nchini pamoja na mambo mengine,” alisema.
Rais Samia alisema wameimarisha mifumo ya ukusanyaji mapato na kuijengea uwezo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kuimarisha mazingira ya kufanya biashara nchini na kuchangia kuleta matokeo chanya ambapo makusanyo ya kikodi yameongezeka kutoka wastani wa Sh. bilioni 850 kwa mwezi mwaka 2015 hadi wastani wa Sh. trilioni mbili kwa mwezi mwaka 2023.
Alisema takwimu za makusanyo ya mwezi uliopita zinaonesha walikusanya zaidi ya Sh. trilioni tatu.
“Eneo hilo ni muhimu kusimamiwa vizuri ili kuongeza ukuaji wa uchumi wa nchi. Uchumi unakua ila hauakisi uhalisia wa kile kinachokusanywa. Kinachokusanywa ni kidogo kingi kinaingia mifukoni mwa watu bure.
“Shughuli za kiuchumi zinazoendelea nchini na idadi ya watu hauakisi uhalisia kukua kwa uchumi na shughuli mbalimbali za kiuchumi na idadi ya watu haiendani na mapato tunayoyapata,” alisema.
Alisema vyanzo vya ndani na visivyo vya ndani vya kodi vipo chini ya lengo walilojiwekea.
“Miongoni mwa viashiria vya utulivu wa uchumi jumla vilivyoainishwa katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano hadi mwaka 2026 ni kuongezeka kwa pato la kodi hadi kufikia asilimia 14.4. Kiwango hicho kitawawezesha kujitegemea.
“Kwa mujibu wa TRA, mwaka 2023/24 mapato ya kodi yamefikia asilimia 12 ya pato la taifa, hivyo bado wapo chini, kuna kazi ya kufanya,” alisema.
Alisema mifumo ya kielektroniki kwa taasisi za serikali zinazotoa leseni kutokusomana ni jambo jingine ambalo linalalamikiwa.
“Kutokuzingatia weledi wakati wa ukusanyaji wa kodi mfano matumizi ya nguvu, lugha zisizo na staha na ubabe kwa baadhi ya watumishi wa serikali hayo nayo yanalalamikiwa.
“Nilikuwa Ruvuma mama lishe analalamikia mikopo ya asilimia 10 ya halmashauari anaenda kufanya biashara ya Sh. 10,000 TRA wanakusubiri, nikasema TRA kwa mama lishe anafanya nini, haya nayo ya kwenda kuyatizama,” alisema.
Alisema idadi ya walipa kodi ni wachache ni zaidi ya milioni mbili kati ya watu milioni 66 wakitoa watoto na watu wengine ambao hawastahili kulipa kodi, hawapungui milioni 37 wanaoweza kulipa kodi.
Rais Samia alisema ameunda tume hiyo ili iwasaidie kufanya tathmini ya mfumo mzima wa kodi kwa upana wake lengo ni kuimarisha zaidi mazingira ya biashara na uwekezaji, kurahisisha usimamizi wa ukusanyaji wa kodi nchini.
Alisema ili isaidie kutathmini, kuchambua na kutoa mapendekezo ya kuimarisha mfumo mzima wa kodi kuendana na mabadiliko ya kiuchumi na kijamii ikiwamo matumizi ya teknolojia.
Rais Samia alisema viashiria vyote vinaonesha uchumi wa nchi unakuwa kwa kasi, lakini ukuaji hauakisi uhalisia wa mapato wanayoyapata.
Alisisitiza kwamba wanataka kujenga mfumo wa kodi ambao unatenda haki ili kila anayestahili kulipa kodi alipe na itozwe kwa mujibu wa sheria.
Alisema tathmini na mapendekezo kuhusu mfumo wa kodi yatawawezesha kuimarisha sekta zote za serikali na kuwaongoza ili kuwamo na mfumo wa kodi unaoendana na maendeleo ya taifa.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka, alisema Mwenyekiti wa Tume hiyo ni Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu, Balozi Ombeni Sefue, na kazi waliyopewa inatakiwa kufanyika ndani ya miezi sita na kuwasilisha ripoti.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED