Wanawake watatu wakazi wa Mkoa ya Njombe na Iringa wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma kwa tuhuma za kuiba vitenge 414 kwenye maduka matatu tofauti yaliyopo katika eneo la Soko Kuu Manispaa ya Songea.
Wanawake hao wamekamatwa wakati wakisafirisha vitenge hivyo kutoka Songea kuelekea Njombe.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Marco Chilya aliwataja wanawake hao wanaotuhumiwa kwa wizi wa vitenge kuwa ni Anna Costa Mtete(22) Mkazi wa Kijiji cha Ndiwile mkoani Iringa,Grace Filipo Kihombo(42) mkazi wa jijini Dar es Salaam na Adeleida John Kihaka (62) mkazi wa kijiji cha Dabaga wilayani Kilolo Mkoa wa Iringa.
Alisema kuwa watuhumiwa hao wakiwa na mali mbalimbali za wizi ambazo waliiba katika maduka tofauti yaliyoko Soko Kuu Manispaa ya Songea ambavyo ni doti 414 za vitenge,doti 6 za kanga,suruali aina ya kadeti 31,pasi za umeme 2,ndoo 1 yenye ujazo wa lita 10 za mafuta ya kupikia,ndoo 1 ya yenye ujazo wa lita 20 ya mafuta ya kupikia.
Alisema kuwa Polisi wanaendelea kufanya uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo ikiwa ni pamoja na kufanya mawasiliano na wenye maduka yaliyoibiwa ili kupata thamani ya mali zote zilizoibiwa upelelezi ukikamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazo wakabili.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED