Warioba asisitiza maridhiano kabla uchaguzi

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 07:30 AM Oct 05 2024
WAZIRI Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais Mstaafu, Jaji Joseph Warioba.
Picha:Christina Mwakangale
WAZIRI Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais Mstaafu, Jaji Joseph Warioba.

WAZIRI Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais Mstaafu, Jaji Joseph Warioba, amesema kuna haja ya kuwapo maridhiano na kuondoa kasoro zilizojitokeza mwaka 2019 na 2020 wakati wa kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani.

Amesema uchaguzi wa vipindi hivyo tofauti, ulikuwa na dosari ambazo baadhi ni ngumu kuepukika, ingawa kadiri kasoro zinapobainika, kuna haja ya kufanyiwa kazi ili kujenga imani kwa pande zote, wananchi na vyama vya siasa.

Jaji Warioba aliyasema hayo jana Dar es Salaam, alipozungumza na waandishi wa habari, kuhusu masuala mbalimbali ya nchi yakiwamo siasa na uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao. Alionya kuwa kasoro kuu ya rushwa miongoni mwa wagombea isipofanyiwa kazi inaweza kusababisha matatizo. 

“Ni kweli kwamba kila uchaguzi una dosari. Duniani  nako hakuna ambako hakuna dosari. Ziko za kawaida, ndogo ndogo na uchaguzi unaofuata unakuwa mzuri zaidi. Lazima tukubali katika uchaguzi unaokuja, tumelizungumza sana kwa sababu ya matukio yaliyotokea mwa 2019 na 2020.

“Katika maisha yangu nimeshapiga kura kwa takribani miaka 13 tangu tupate uhuru na kila baada ya miaka mitano lazima tuwe na uchaguzi. Kwa kipindi chote hiki hakukuwa na matatizo makubwa katika uchaguzi, ukiacha yaliyotokea Zanzibar,” alisema.

Alisema uchaguzi wa serikali za mitaa kwa mwaka 2019 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 ulikuwa na kasoro kubwa na kusababisha baadhi ya watetezi wa haki za binadamu na demokrasia, kushtuka na kuwa miongoni mwa hoja kuu kuwako kwa uhuru na haki kwa uchaguzi ujao.

“Mfano mwaka 2019 tunapozungumzia dosari kipindi hiki kulikuwa na dosari nchi nzima hasa katika uteuzi wa wagombea, usimamizi wa uchaguzi na wajibu wa mawakala. Mwaka huu kuna jitihada kubwa za kufanya ili yaliyotokea yalisitokee tena.

“Serikali za mitaa tumefanya kwa miaka mingi na hata tulipoingia mfumo wa vyama vingi, ulisimamiwa na serikali mwaka 1994 mpaka 2014 hakukuwa na matatizo makubwa.

Ule wa mwaka 2019 ulikuwa kama umepangwa matatizo haukuwa wa kawaida. Mwaka huu pia uchaguzi wa serikali za mitaa utasimamiwa na serikali, maandalizi yamefanyika. Elimu  ni muhimu kwa sababu bila hilo inawezekana uchaguzi wa mwaka huu usiwe na matokeo makubwa,” alisema.

Jaji Warioba alisema uchaguzi ulio huru na wenye haki utaziondoa kasoro zilizotokea awali kwa kuwapo hakikisho hasa wakati wa kuteua wagombea hakutakuwa na tatizo, kwa baadhi yao kuenguliwa.

Pia alisema maandalizi wakati yanakwenda vyema hivi sasa kama vile ya kujiandikisha, kuwako elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kupiga kura kwa sababu uzoefu unaonesha idadi ya wapigakura nchini inapungua licha ya wengi wao kujitokeza katika kusikiliza sera za wagombea wanapojinadi kwenye kampeni.

“Yule aliyesimamia uchaguzi ndiye yule yule atasimamia. Bado wananchi wana wasiwasi, atarudia ile au atafanya tofauti? Kuna haja ya jitihada kuwaaminisha wananchi yaliyotokea nyuma hayatajirudia tena,” alisema.

Warioba alisema kasoro zingine ni kuwa maandalizi ya kuwafanya wananchi wawachague wanaowataka ni duni, licha ya kwamba wapigakura wa kitongoji ndio wanaowafahamu wanaoishi eneo lao.

“Vyama vinapeleka watu wao (wateuliwa). Wakati wa mfumo wa chama kimoja, kulikuwa na utaratibu wa kujua, je, hawa wanakubalika? Kulikuwa na mkutano mkuu kwa ajili ya kupata kura za maoni, lakini nikaja na hoja mkutano mzima unaweza kuhongwa, tuite wote balozi hadi wenyeviti wa wilaya waje.

Lakini haikupita muda kumbe hata kundi hili kubwa kuna watu wana fedha nyingi wanaweza kuwahonga, tuite wanachama wote bado ikashindikana. Tatizo la rushwa likawa linaingilia uchaguzi, tukasema tuwe na wajumbe wa kupiga kura za maoni, bado tatizo,” alisema.

Alisema wagombea wengi nchi nzima, wana uwezo wa kuwahonga wanaowapigia kura za maoni na kwamba ugumu unakuja kutokana na wanaohongwa ni viongozi wanaotarajiwa kupigakura.

“Kwa hiyo hatuna uhakika tuliposema wananchi wana haki ya kumpata yule wanayemwona anafaa. Katika maandalizi, vyama vya siasa viwe na utaratibu ambao unazingatia wanaoteuliwa wanakubalika kwenye maeneo yao, kwa sababu wakichaguliwa wasiofaa hawatasaidia.

“Kwa sababu akiwa mteuliwa na chama lakini hakubaliki, inawapunguzia uwezo hawa viongozi. Kwa  kuwa wananchi hawamkubali, inakuwa ngumu kuwaongoza, hivyo tunataka watu wanaokubalika na jamii,” alisema.

Jaji Warioba alisema uongozi wa serikali za mitaa ni muhimu kutokana na kwamba ndiko unakoanzia uongozi na kubainisha kwamba uongozi wa ngazi ya chini kutokuwa thabiti imekuwa sababu ya jamii linapotokea tatizo, huitazama nafasi ya juu kiuongozi wakimtaka rais awatatulie matatizo yao.

Pia alisema kuna haja ya serikali, mamlaka za usimamizi wa uchaguzi kukaa meza moja na vyama vya siasa kuvihakikishia amani, akionya kuwa matumizi ya nguvu ya vyombo vya ulinzi na usalama, tija yake hupungua kutokana na pande zote kushindana.

Jaji Warioba alisema kwa kipindi cha takribani miongo mitatu demokrasia imejengwa, ingawa utawala bora uliwekwa nyuma na kwamba ni wakati wa kuujenga, kwa kuwa ndio msingi wa uongozi.

“Miaka mitatu iliyopita hali ya siasa haikuwa nzuri. Maandamano yalizuiwa, mikutano ilipigwa marufuku. Rais (Samia Suluhu Hassan) ameiweza nchi sasa imetulia kwa sababu aliondoa yale matatizo. Mfano haya maandamano ya hivi karibuni mimi ninachokiona ni kupambana.

“Jeshi la Polisi linasema watakaokuja watakiona na vyama vya siasa nao wanakuja na wanachokitaka. Watumie lugha nzuri katika shughuli za siasa zetu. Amani inajengwa na wananchi na si polisi peke yao, maana wanasema wanalinda amani, mi nadhani wakae chini pande zote, wakubaliane,” alisema.