Msako wamiliki wa silaha kinyume cha sheria kuanza rasmi Novemba

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 07:32 AM Oct 05 2024
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), David Misime.
Picha:Mtandao
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), David Misime.

JESHI la Polisi nchini limesisitiza baada ya mwezi huu kuisha msamaha uliotolewa kwa wamiliki wa silaha kinyume cha sheria kuzisalimisha, linatarajia kuanza msako dhidi ya waliokaidi.

Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), David Misime, aliyasema hayo jana na kusisitiza watakabainika bado wanatumia silaha hizo kinyume cha sheria, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Misime alisema lengo la kutangaza msamaha huo ni kuhakikisha silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria zinaondoshwa katika jamii ili zisisababishe madhara kwa raia yakiwamo vifo, majeruhi, watu kuhama makazi, njaa pamoja na uchumi kuzorota.

Alisema masharti yaliyotolewa katika tangazo hilo la msamaha ni pamoja na kipindi cha usalimishaji wa silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria kilichoanzia Septemba Mosi hadi Oktoba 31, mwaka huu.

“Maeneo ya usalimishaji wa silaha hizo ni vituo vya Polisi, Ofisi za Serikali za Mitaa na katika Ofisi za Watendaji Kata/Shehia pamoja na muda wa usalimishaji wa silaha ambao ni kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa kumi jioni,” alisema.

 Misime alizitaja silaha zinazopaswa kusalimishwa ni pamoja na zile ambazo hazijawahi kusajiliwa nchini na zimekuwa zikimilikiwa kinyume cha sheria na zile awali zilikuwa zinamilikiwa kihalali, lakini kwa sasa wamiliki wamefariki dunia na ndugu kuendelea kuzimiliki kinyume cha sheria.

 “Jeshi la Polisi linawahakikishia wananchi kuwa yeyote atakayesalimisha silaha hizo ndani ya kipindi cha msamaha hatoshtakiwa na wala  hakutohitajika kujua jina la atayesalimisha au kujua uhalifu uliotendeka kwa kutumia silaha hiyo,” alisema.

Takwimu zinaonesha mwaka 2023, silaha 337 na risasi 262 zilisalimishwa kwa hiari na baada ya msako ulifanyika nchi nzima na watuhumiwa 176 walikamatwa na silaha 195.

Pia walikamatwa watuhumiwa saba ambapo wanaume walikuwa sita na mwanamke mmoja  ambao walikutwa wakimiliki risasi 334 kinyume cha sheria na kufikishwa mahakamani na baadhi walitiwa hatiani na kutumikia kifungo gerezani na wengine kesi zao zipo katika hatua mbalimbali.