Huduma bora ziendane na mpango kukuza sekta utalii

Nipashe
Published at 07:51 AM Sep 26 2024
Huduma bora ziendane na mpango kukuza sekta utalii
Picha: Mtandao
Huduma bora ziendane na mpango kukuza sekta utalii

UTALII ni moja ya sekta muhimu nchini katika kuchangia pato la taifa na kuzalisha ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja nchini. Kwa mujibu wa takwimu za sasa, sekta hiyo inachangia asilimia 17 ya pato la taifa, hali inayodhihirisha kwamba ni eneo muhimu linalopaswa kupewa kipaumbele cha kipekee.

Ukuaji  wa sekta hiyo, kwa kiwango kikubwa unatokana na  vivutio mbalimbali zikiwamo hifadhi za taifa kama vile Mikumi, Ngorongoro, Serengeti, Manyara, Tarangire, Udzungwa na Ruaha. Hifadhi hizo zina vivutio vingi kama vile wanyamapori wakiwamo simba, tembo, faru, twiga na nyati ambao huwafanya watalii wa ndani na nje kutembelea maeneo hayo na kujionea rasilimali hizo asilia.

Kwa takribani miaka mitatu na nusu tangu Rais Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani, kumekuwa na ongezeko kubwa la watalii wanaofika katika hifadhi hizo, hivyo kuiwezesha nchi kupata fedha za kigeni kwa kutembelea hifadhi, kulala katika hoteli na kununua bidhaa mbalimbali za asili za Tanzania. 

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Maliasili na Utalii, katika mwaka wa fedha wa 2023/24, idadi ya watalii kutoka nje ya nchi, waliongezeka hadi kufikia 1,808,205 kutoka watalii 922,692 mwaka 2021. Ongezeko hilo kwa kiasi kikubwa lilitokana na kutangazwa kwa vivutio vya utalii nchini kulikochagizwa na filamu ya ‘The Royal Tour’ iliyochezwa na Rais Samia.

Filamu hiyo iliitangaza Tanzania kwa kiwango kikubwa, hivyo kufahamika kimataifa kuwa ina vivutio vingi na kuwafanya watalii kuiona kuwa sehemu muhimu ya kutembelea na kushangaa maajabu yaliyomo ndani yake hasa wanyamapori waliomo katika hifadhi za taifa. 

Kutokana na kasi ya kuitangaza nchi nje ya mipaka na duniani kwa ujumla, Waziri wa Maliasili na Utalii, Pindi Chana, mapema wiki hii alisema lengo la serikali ni kufanya jitihada za kuboresha utalii ili kuhakikisha watalii wanaoingia nchini wanafikia milioni tano ifikapo mwaka 2025. Iwapo azma hiyo itafikiwa, ni wazi kwamba serikali itapata fedha nyingi za kigeni kupitia sekta hiyo na hatimaye kuchangia zaidi katika pato la taifa. 

Malengo yaliyowekwa kwa kufikisha watalii milioni tano ndani ya mwaka mmoja ni makubwa, hivyo yanahitaji juhudi za pamoja kati ya serikali na wadau, kwa mantiki hiyo, nguvu zaidi zinatakiwa kuendelea kutangaza vivutio vya utalii vilivyoko nchini ili kuwafanya watalii kuja kwa wingi na kufikia idadi iliyokusudiwa. 

Sambamba na hayo, miundombinu kuelekea kwenye hifadhi za taifa kama vile barabara na viwanja vya ndege vinapaswa kuimarishwa ili kuwawezesha watalii kufika kwa urahisi. Viongozi wa serikali walioko katika mikoa yenye vivutio hivyo, wanapaswa kuweka suala la utalii ajenda namba moja katika shughuli zao za kila siku. 

Kama alivyosema Rais Samia wakati akiwaapisha viongozi, alimwelekeza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, kusimamia suala la utalii kutokana na mkoa huo kuwa kitovu cha sekta hiyo. Kwa mpango wa kuongeza idadi ya watalii, Makonda alikuwa kiwakilishi cha viongozi ambao mikoa yao ina vivutio hivyo, hivyo nao wanapaswa kuzingatia maelekezo hayo. 

Licha ya wajibu huo wa viongozi, sekta binafsi, hususan wamiliki wa hoteli na migahawa ya chakula pamoja na huduma zinazohusiana na utalii moja kwa moja, wanapaswa kuboresha huduma zao ili kuhakikisha watalii wanapofika, wanapata huduma za viwango vya juu na hatimaye wanaporejea kwao wanakuwa mabalozi wazuri wa kuitangaza Tanzania na vivutio vyake. 

Kwa mikakati ya pamoja na ushirikiano baina ya sekta binafsi na ya umma, azma ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utalii itaongezeka na hatimaye sekta hiyo kuchangia ukuaji wa uchumi na pato la taifa maradufu au zaidi kulinganisha na hali ilivyo sasa.