ZIARA MADAKTARI SAMIA HOSPITALI 184... Siku sita za kila mkoa wanaofikia waacha ujuzi na kuokoa vichanga

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:04 AM Oct 10 2024
Timu ya Madaktari Bingwa wa Samia, waliotua mkoani Kigoma Jumatatu wiki hii kutoa huduma ya siku sita, wakiwa pamoja mjini hapo.
PICHA: MTANDAO.
Timu ya Madaktari Bingwa wa Samia, waliotua mkoani Kigoma Jumatatu wiki hii kutoa huduma ya siku sita, wakiwa pamoja mjini hapo.

HADI sasa nchini kuna kikosi maalum cha madaktari bingwa kilichoandaliwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kusaidia kupunguza vifo vya watoto wachanga na kuwajengea uwezo watoa huduma wengine.

Ni hatua inayochukuliwa katika hospitali za halmashauri nchini, lengo pia kuwa na wodi maalum za watoto wachanga wenye umri siku 28 na chini ya hapo, ili kuokoa maisha yao. 

Aliyekuwa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akatamka hayo Mei 6 mwaka huu mkoani Iringa, alipozindua kinachoitwa ‘Mpango Kabambe wa utoaji wa huduma za kibingwa kwenye hospitali 184 katika ngazi ya halmashauri…” kupitia kaulimbiu ‘Tumekufikia, Karibu Tukuhudumie.’

KYELA WIKI JANA

Dk. Halima Mohamed Abass wilayani Kyela Ijumaa wiki iliyopita, akiwa na wataalamu wenzake alikuwa na maelezo: “Mafunzo haya ni sehemu ya mikakati ya serikali ya kuboresha huduma za afya kwa wananchi na kuhakikisha kila kituo cha afya, kina wataalamu waliobobea na kuwa na weledi stahili kwenye utoaji huduma.

 “Ni muhimu kila mhudumu wa afya anakuwa na ujuzi wa kisasa ili kuboresha matokeo ya afya kwa wagonjwa wetu, hususan watoto ambao wanahitaji uangalizi wa kipekee, kwani serikali chini ya uongozi imara wa Rais Samia Suluhu Hassan imewekeza vya kutosha katika miundombinu na vifaa tiba vya kisasa.” 

Mnamo Oktoba 4 wikiendi iliyopita, katika Hospitali ya Wilaya Kyela mkoani Mbeya, Madaktari Bingwa na Rais Samia, waliendesha mafunzo elekezi kwa watoa huduma za afya, kuwajengea uwezo watalamu hao wa Halmashauri ya Wilaya Kyela.

Mafunzo hayo Ijumaa iliyopita yakiongozwa na tabibu bingwa wa Watoto, Dk. Halima, yakalenga kuwafanya wataalamu wenyeji hospitalini kuongeza ufanisi wa huduma wanazotoa. 
 
 “Tunafanya kazi kwa karibu kuhakikisha kila kituo cha afya kina wataalamu waliobobea na wenye mafunzo ya kutosha ili kuboresha afya ya wananchi kwa ujumla,” anasema Dk. Halima. 
 
 Pia, akabainisha umuhimu wa watoa huduma kujua kutumia vifaa tiba kwa usahihi, kwani vina uwezo mkubwa wa kuboresha matibabu, vikitumika ipasavyo na kusaidia wananchi wa maeneo hayo. 
 
 “Mafunzo haya yatawawezesha kujifunza mbinu bora za kutumia teknolojia na vifaa vya kisasa ili kutoa huduma bora zaidi kwa wagonjwa na kupunguza rufani zisizooza lazima,” anaongeza.

Dk. Halima akawahimiza wananchi wa Kyela kuchangamkia fursa hiyo ya kipekee kupata huduma za kibingwa, kwa kujitokeza wapate vipimo, ushauri na matibabu kutoka kwao madaktari hao wageni.

WALIVYOTUA KATAVI

Wiki hii kikosi hicho cha Madaktari Bingwa wa Rais Samia, wamefika na mageuzi kwa kuwaanzishia Kitengo Maalumu cha Uangalizi wa Watoto Wachanga (NCU) katika Hospitali ya Wilaya ya Nkasi, ambayo haikuwapo wilaya.

Bingwa wa Magonjwa ya Watoto, Dk. Amos Rubeja, anasema wamejitahidi kuongeza nguvu kuanzisha vitengo NCU, kuhudumia watoto wachanga wenye changamoto za kiafya.

Hapo kuna waliozaliwa kabla ya muda, pia wenye uzito mdogo wanaowekwa vifuani mwa mama (kangaroo mother care) na wenye uzito mdogo, wakikaa katika wodi yao watoto.

"Baada ya kufanikisha kuanzisha kitengo hicho, mpaka jana tumepata watoto wawili, mmoja alikuwa na kilo moja ambaye alizaliwa wiki ya 31 na mwingine alikuwa na kilo 1.3, aliyezaliwa wiki ya 32 na wote wanaendelea vizuri," anatamka.

Dk. Rubeja anasema wamefanikiwa kuwagundua watoto wenye changamoto na kuweza kuwapa rufani kwenda hospitali za juu kupatiwa matibabu.
 
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya Nkasi, Dk. Thomas Ndeule, anasema ujio wa madaktari hao umekuwa wa manufaa kwa wananchi Nkasi kupata huduma za kibingwa wilayani hapo.
 
 "Pasingekuwa na uwepo wa madaktari Bingwa wa Rais Samia tungelazimika kuwapa rufani wazazi wa watoto hawa kuwasafirisha kuwapeleka katika Hospitali ya Rufani," anasema.

Mkazi wa Nkasi, Anastazia Benedikto, kwa niaba ya wenzake anamshukuru Rais kwa kufanikisha uwapo wa madaktari hao bingwa katika makazi yao.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko mnamo Oktoba, 7, wakati anazindua kambi ya Madaktari Bingwa wa Samia, kuhudumia hospitali tano za mkoa huo na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya katika hospitali hizo, akatamka:

“Nendeni mkatoe hamasa kwa wananchi kuwa na utamaduni wa kupima afya zao kabla ya kuugua, ili kujua hali za afya zao na kupata matibabu sahihi kabla ya tatizo kuwa kubwa na kuleta athari kubwa wakati wa matibabu.”

Pia, akashauri uhamasishaji wajawazito kwenda kwenye vituo vya kutoa huduma za afya mapema   kuanza kliniki kwa wakati, kuepuka baadhi ya matatizo yanayoweza kutokea wakati wa ujauzito.

“Namshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa aliofanya katika sekta ya afya, hasa kwa kuona umuhimu wa kusogeza huduma za kibingwa na bingwa bobezi karibu na wananchi na kuleta tija ya kutotumia gharama kubwa kufuata huduma hizo,” anatamka Mkuu wa Mkoa.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Dk. Jonathan Budenu, anasema kambi hiyo ya madaktari bingwa, itatoa huduma za kibingwa kwa siku saba na kutoa ujuzi kwa wataalamu wa afya walipo katika hospitali tano, ambazo mabingwa wanaenda kutoa huduma.

KIGOMA NAKO

Wiki hii Jumatatu, jumla ya madaktari bingwa 57 wa Rais Samia wamewasili mkoani Kigoma kutoa huduma za kibingwa kwenye halmashauri zote za mkoa kwa muda wa siku sita na wamepokewa na Katibu Tawala, Hassan Rugwa. 

Akiwakaribisha kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Thobias Andengenye, akafafanua katika utashi na nadharia ileile ya Katavi, kutoa huduma kibingwa na kuwajengea uwezo wataalamu wa mkoani humo, akizitafsiri kuokoa maisha ya watu.

Rugwa anasema, huduma hiyo inatolewa kwa ushirika wa Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais – TAMISEMI, lengo ni kuboresha huduma na kupunguza vifo vya kinamama na watoto vitokanavyo na uzazi. Pia, inagusa huduma jumuishi za kibingwa Kigoma.

Mratibu wa huduma hizo za madaktari bingwa mkoani Kigoma, Jackline Ndanshau, anasema mkoani himo zipo huduma hizo ngazi ya halmashauri.

Anataja mradi husika una mafunzo elekezi kazini kwa watoa huduma za afya, kuimarisha ubora wa huduma za afya katika hospitali wanazopelekwa Madaktari Bingwa wa Rais Samia.

Mganga Mkuu wa Mkoa Kigoma, Damas Kayera, anasema ugeni wa madaktari bingwa Kigoma, ni furaha kwa wananchi kuhudumiwa kibingwa kwa waliyopaswa kufuata mbali, ikiwamo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Aidha, anasisitiza hamasa ya wananchi kupata lishe bora na sahihi kwa watoto wadogo, vijana, rika la kati na wazee, kulingana na maelekezo ya wataalamu wa lishe katika maeneo yao.

Anasema, ni hamasa inayowasaidia wananchi kujitambua mapema kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza, kuanza uchunguzi na matibabu mapema, kabla ya tatizo kuwa kubwa.

MKOANI TABORA

Katibu Tawala wa Mkoa huo, George Mboya, wakati wa hafla ya mapokezi Madaktari Bingwa Samia mkoani Tabora, Jumatatu wiki hii wakitarajiwa kuwapo hadi Jumamosi ijayo, anasema magari ya matangazo yameunguka kunadi uwapo wa huduma hiyo.

Katibu Tawala akatumia fursa hiyo kumshukuru Rais kuelekeza zaidi ya shilingi bilioni 29.3 kwenye uimarishaji wa miundombinu ya afya na vifaa tiba.

"Ujio wenu unazidi kutuonyesha ni jinsi gani Mheshimiwa Rais anatupenda, maana baada ya kutuimarishia miundombinu, ameamua kutushushia huduma hadi ngazi ya za msingi,” anatamka Mboya, akiwataka watumishi wa afya mkoani kuwapa ushirikiano.

Mboya, pia amewataka watumishi wa afya katika mkoa huo na wananchi kwa jumla, kuwapa ushirikiano madaktari bingwa waliopangwa kwenye mkoa wao.

Mkurugenzi wa Afya ya Uzazi kwa Huduma za Mama na Mtoto, Rais Samia , anasema hilo linafanyika, ikiwa ni matokeo ya mafanikio ya awamu ya kwanza.

Timu  hiyo, ambayo huzunguka katika mikoa mbalimbali, kwa ratiba ya siku sita za kuhudumia kila mkoa, hivi karibuni wamekuwa katika mikoa ya Songwe na Singida.