Wana- Kanda ya Ziwa wanavyohama toka uzazi foleni hadi kuacha nafasi

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 10:26 AM Oct 10 2024

Wazazi wakiwa katika mija ya hospitali mkoani ya Kanda ya Ziwa.
PICHA: MTANDAO.
Wazazi wakiwa katika mija ya hospitali mkoani ya Kanda ya Ziwa.

UZAZI wa kuacha nafasi umeonyesha kichocheo cha ukuzaji uchumi kifamilia, kutokana na wazazi kupata muda kufanya shughuli za maendeleo, wakipanga bajeti zao kwa usahihi na wanaowahudumia watoto kukikidhi mahitaji yao.

Ni aina ya uzazi unaoruhusu usimamizi bora wa fedha na kuongeza uwezekano wa matumizi ya busara ya rasilimali na wazazi kupata muda wa kufanya shughuli zao kiuchumi.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), linasema uzazi wa kuacha nafasi ni muhimu kwa maendeleo endelevu na mapambano ya umaskini katika kaya.

Muuguzi wa Uzazi wa Mpango na Upimaji Saratani, kutoka Hospitali ya Rufani ya Mkoa Shinyanga, Maria Barikwingenza, anasema uzazi wa kuacha nafasi kwa mwanamke unaimarisha afya yake na atakuwa na nafasi ya kufanya shughuli zake kiuchumi, akiinua kipato cha familia.

Anaeleza, hata baba anapata nafasi nzuri ya kuhudumia familia kwa kupanga bajeti zake kwa usahihi na kufanya maendeleo katika kaya yake.

“Uzazi wa kuacha nafasi ni muhimu sana katika familia, kwa sababu ni kichocheo kikubwa cha ukuaji wa maendeleo, kutokana na kupanga bajeti zao vizuri pamoja na kuwa na muda mwingi wa kufanya shughuli za kiuchumi,” anasema Maria.

Anafafanua mwitikio wa wanawake kujitokea, kupata huduma ya uzazi kudhibiti uzazi mfululizo watoto katika hospitali hiyo siyo mkubwa.

Maria anasema, wao wataalamu wamekuwa wakijitahidi kutoa elimu kwa wajawazito wanaofika kujifungua hospitalini hapo.

“Huduma za kudhibiti uzazi zinatolewa bure, na wanawake ambao tunawapatia huduma hizi. Kwanza, huwa tunawapatia ushauri na wengi huwa wanapenda kutumia njia ya vidonge, sindano pamoja na njiti na kwa mwezi mmoja huwa tunawapatia huduma wanawake 10,” anasema Maria.

UTAFITI ULIVYO

Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto wa Viashiria vya Malaria Tanzania (TDHS) 2022, vinawarejea wanawake wanaotumia njia za kudhibiti uzazi kwa walioolewa ni asilimia 38, ambao hawajaolewa wako asilimia 45.

Utafiti huo unautaja mkoa wa Shinyanga, ni asilimia 35 tu ya wanawake wanaotumia njia za kudhibiti uzazi.

Mratibu wa Elimu Afya kwa Umma Mkoa wa Shinyanga, Moses Mwita, anasema kutokana na mwitikio huo kuwa mdogo wa wanawake kutumia njia za uzazi, wamekuwa wakiwapa elimu wanawake kupitia vyombo vya habari, majukwaa mbalimbali na mikusanyiko.

Anasema elimu hiyo wamekuwa wakiitoa kila mwezi, kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, likiwamo shirika binafsi.

Hapo wamekiwa wakiacha nafasi katika uzazi, huku wakiona faida kubwa kwa afya ya mama na mtoto, inayobaki kichocheo cha ukuaji uchumi nchini. 

“Hapa Shinyanga tuna wahudumu wa afya ngazi ya jamii wapatao 2,800 ambao hutembelea kila kaya na kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa wanawake na uzazi wa mpango,” anasema Mwita.

Hadi sasa mkoani humo, kuna mradi uitwao ‘Maamuzi Yako Kesho Yako’ ulioko katika ngazi awamu ya nne, ulioanza Januari mwaka huu na unatarajiwa kudumu hadi Desemba 2026, ukilenga elimu ya uzazi wa kuacha nafasi katika familia.

Mratibu wa Mradi huo, Godbless Mtega, kutoka shirika binafsi mkoani humo, anasema wamekuwa wakifanya kazi kwa karibu na serikali, wakipanga ratiba ya kutoa elimu na huduma ya uzazi wa kuacha nafasi.

“Mradi huu wa ‘Uamuzi Wako Kesho Yako’ ni huduma jumuishi, ambayo timu ya wataalamu wa huduma za uzazi huambatana wataalamu wa chanjo kwenda kwenye kijiji chenye ratiba ya huduma hizo, ambao hutolewa elimu na ushauri kuhusu uzazi wa kuacha nafasi,” anasema Mtega.

Anataja takwimu kwa kipindi cha kuanzia Januari 2024 hadi Septemba mwaka huu, kuwa timu ya wataalamu wa afya ya uzazi wakishirikiana na watoa huduma kutoka vituo vya serikali, wamefikia wanawake 5,222 wakiwapatia njia za uzazi za kisasa, walizochagua kwa hiari yao mara, baada ya kupewa elimu na ushauri.

 Mtega anaongeza kuwa, wamekuwa wakiwajengea uwezo watoa huduma katika hospitali, vituo vya afya, zahanati na wahudumu wa afya ngazi ya jamii, ili kuwaongezea ujuzi wa masuala ya uzazi huo.

“Uzazi wa kuacha nafasi ukifuatwa vyema ngazi ya kaya, familia zitakuwa na uchumi imara, sababu watapangilia bajeti zao vizuri, na hata taifa pia litakuwa kiuchumi sababu halitakuwa na idadi ya watu wengi wasio na kazi,” anaongeza.

Mhudumu wa Afya Ngazi ya Jamii, Getruda Emmanuel, anasema wamekuwa wakitoa elimu kwa wanawake kuhusu umuhimu wa kuzaa kwa kuacha nafasi, kupitia mikutano mbalimbali na hata kutembelea kila kaya.

Anasema wanawake wa vijijini, wengi hawana elimu ya afya ya uzazi, hivyo wao wahudumu wa afya ngazi ya jamii, hulazimika kuwatembelea katika ngazi ya kaya kiwaelimisha na kuwaelezea faida ya kuzaa kwa kuacha nafasi.

WANUFAIKA WANENA

Mama Lishe, Rejina Malongo, anasema ametumia njia za kudhibiti uzazi tangu mwaka 2001 na zimemsaidia kupata muda wa kufanya shughuli zake za kiuchumi.

Anasema, hadi sasa ana watoto watano, wote amewapata akicha nafasi kwa miaka miwili hadi mitatu, iupata muda wa kutosha kufanya shughuli zake za mama ishe.

“Mwanamke akizaa kwa kuacha nafasi, kwanza atakuwa na afya njema pamoja na watoto wake kama unavyoniona mimi, pia atapata muda mwingi wa kufanya shughuli zake za kiuchumi,” anasema Rejina.

Mwingine, Rehema Matondo, mkazi wa wilayani Shinyanga, anasema vijijini, wanawake wengi hawana elimu ya afya ya uzazi, na ndiyo maana huzaa watoto mfululizo bila ya kuacha nafasi na mara nyingi wanakuwa tegemezi kwa waume zao, sababu hawana muda wa kufanya shughuli zao kiuchumi.

Anashauri, elimu hiyo ya afya ya uzazi inapaswa itolewe sana vijijini kwa wanawake na waume zao, kwa sababu wanawake wa vijijini hawana uamuzi katika uzazi, bali hutawaliwa na mwanaume na kupata watoto mfululizo bila hata ya kujali afya ya mama.

Jidayi Magembe, aliyepata elimu ya afya ya uzazi na uzazi wa mpangilio, anasema amekuwa akijifungua kwa kuacha nafasi yamiaka mitano na anapanga bajeti vizuri za matumizi ya familia, huku akifanya shughuli zake kwa uhuru. 

“Kuzaa watoto kwa kuacha nafasi kuna faida yake kiuchumi. Mimi watoto wangu wote wawili wanasoma shule binafsi, sababu nafanya shughuli zangu kwa uhuru napata pesa, lakini ninge zaa mfululizo huenda sasa hivi ningekuwa na watoto hata watano, harafu kuwa hudumia ingekuwa shughuli pevu,” anasema Jidayi.

Mwanaume, Kulwa Jishosha, anasema wao vijijini huwajui kuacha nafasi, wanazaa watoto wengi wakiamini ni nguvu kazi ya kulima shambani na ndiyo utamaduni walioukuta duniani.

Mzee wa kimila, Sonda Kabeshi, anakiri utamaduni wa kijijini ni unaegemea nguvu kazi ya uzazi wa watoto wengi, lakini anasema sasa yameshapitwa na wakati.

Anasema, watoto hao wanapokuwa watu wazima na kuhitaji kujitegemea, hujikuta hawana mali, ikwamo mashamba waliolima wazazi wao.

Mzee Kabeshi anaeleza kwamba, nihali inayowafanya watoto kuwa wategemezi hadi utu uzima na baadhi ndio wanaiojitokeza hatua ya kusuka njama kuwadhuru wazazi wao, kwa tamaa ya urithi wa mali.

“Mimi nina familia mbili moja ipo Shinyanga mjini, nyingine huku kijijini Shantimba, lakini nilizaa watoto kwa kuacha nafasi na nipo vizuri kiuchumi, na watoto wangu wengine wanashughuli zao na baadhi bado wanasoma,”anasema Sonda.

Anawasihi wananaume na vijana wasiige ya zamani, kwa sababu mambo mengi yamebadilika, hata kuifanyua kanuni za kale kukosa nafasi katika shughuli za kimaendeleo.