Stars, DRC Congo majaribuni

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 10:31 AM Oct 10 2024
Taifa Stars
Picha:Mtandao
Taifa Stars

WAKATI ikiwa ugenini kusaka pointi tatu muhimu, Kaimu Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Hemed Suleiman 'Morocco', amesema malengo yao ni kuona wanaongoza katika Kundi H na hatimaye kufikia malengo ya kusaka tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON 2025), zitakazofanyika baadaye mwakani nchini Morocco.

Hata hivyo, wakati Stars inatua mjini Kinshasa, mshambuliaji nyota wa timu hiyo, Mbwana Samatta, aligeuka kivutio kwa mashabiki waliojitokeza na hiyo inaonyesha heshima kwa Mtanzania huyo aliyewahi kuichezea TP Mazembe ya nchini humo.

Timu hizo zinakutana huku wenyeji wenye pointi sita wakiwa kinara katika Kundi H wakifuatiwa na Taifa Stars iliyojikusanyia pointi nne, Ethiopia yenye pointi moja inashika nafasi ya tatu huku Guinea wakiburuza mkia kutokana na kutokuwa na pointi yoyote.

Akizungumza na gazeti hili kuelekea mechi hiyo, Morocco, alisema anaiheshimu DRC Congo lakini malengo yake ni kupata ushindi katika mchezo wa leo ili kujiweka kileleni kwenye msimamo wa kundi.

"Nafahamu hautakuwa mchezo mwepesi, tupo ugenini, lakini lazima tupambane kufikia malengo yetu, ni mchezo ambao ushindi utatuweka juu katika msimamo wa kundi. Tumejiandaa vizuri lakini tutacheza kwa nidhamu kubwa kuhakikisha tunafikia malengo yetu ya kuondoka na pointi tatu," alisema Morocco.

Kocha huyo alisema akili na nguvu zao zote wamezielekeza katika mchezo huo utakaoanza saa 1:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

"Baada ya mchezo ndio sasa tutaanza kuupigia mahesabu mchezo wa marudiano ambao tutakuwa nyumbani, nina imani na kikosi changu na kila mchezaji yupo kwenye morali na ari nzuri," Morocco alisema.

Naye nahodha wa timu hiyo, Mohamed Hussein 'Zimbwe Jr', alisema wako tayari na ushirikiano 'mkubwa' waliopata kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan, umewaongezea chachu ya kwenda kupambana.

Alisema wanaona wanadeni la kuwalipa Watanzania na njia pekee ni kupambana na kuhakikisha wanafanya vizuri katika mchezo huo.

"Kikubwa cha kuwalipa Watanzania ni kufanya vizuri," alisema beki huyo anayeichezea Simba ya Dar es Salaam.

Katika hali iliyoamsha shangwe, Samatta, ambaye amerejeshwa katika kikosi cha timu hiyo baada ya kuwa nje kwenye mechi mbili zilizopita, amekuwa gumzo Congo ambapo mashabiki wengi wanamzungumzia.

Wakiwa kwenye Uwanja wa Ndege Mjini  Kinshasa, mashabiki hao waliweka wazi hisia zao na mapenzi kwa mchezaji huyo wa zamani wa mabingwa wa Afrika, TP Mazembe yenye makazi yake Lubumbashi.

"Kwenye kikosi cha Tanzania tunamhofia zaidi Samatta, ni mchezaji mzuri na amefanya makubwa hapa akiwa na TP Mazembe, wengi tutakwenda uwanjani kumwangalia, lakini tunataka Congo ishinde," alisema mmoja wa mashabiki ambaye ni Mkongomani.

Samatta alicheza kwa mafanikio makubwa akiwa na TP Mazembe aliyojiunga nayo mwaka 2011 akitokea Simba na alifikia kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani.