WIKI YA SAMIA NYANDA ZA JUU...Ashuhudia ‘live’ ndoto tiba hospitali ya wana- Katavi aliyoanza kwa ‘kuokoteza’

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:59 AM Jul 18 2024
Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Katavi.
PICHA: MTANDAO.
Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Katavi.

HOSPITALI ya Rufani Mkoa Katavi ni mradi mpya na mkubwa. Dhana ya utekelezaji wake ilianza mwaka 2019 na hadi kufika 2021, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, akitunukiwa urais kutoka Makamu Rais; hatua ya ujenzi ilikuwa asilima 43, kwa mujibu wa ripoti zilizoko.

Mnamo Aprili mwaka huu akiwa ziarani mkoani Rukwa, Katibu Uenezi na Itikadi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla, akatamka Rais Dk. Samia alikuwa katika hatua nzuri kukamilisha ahadi alizopokea kutoka kwa mtangulizi, Hayati Dk. John Magufuli.

Itakumbukwa, wakati anaingia madarakani, Rais Dk. Samia, akaahidi kusimamia na kuyaendeleza miradi yote kitaifa aliyoacha mtangulizi, Dk. Magufuli.

Leo hii ni miaka mitatu na robo ya Rais Dk. Samia, sasa anahitimisha ahadi na matamshi yake, mojawapo ni mapinduizi makubwa kuhuisha uwapo wa Hospitali ya Rufani Mkoa Katavi, 

Ilikuwa wikiendi iliyopita ziarani mjini Mpanda, akamwaga sifa kwa alichokiona katika hospitali hiyo, hata kuwapa sifa ni wa kuigwa na hospitali zingine nchini

"Nimesimama kuelezea furaha yangu, nimefika kukagua hospitali na kuona inavyoendelea," anasema Rais Dk. Samia, akisifu kwa nafasi ya upekee usafi wake, anampongezaa Mganga Mfawidhi wa Hospitali, Dk. Serafin Patrice na menejimenti yote...

"Hospitali hii imenipa faraja. Wakati naongozwa kuangalia madaktari wote niliofuatana nao ni vijana ambao wangependa kuhudumu kwenye miji mkubwa kama Dar es Salaam, Arusha au Mwanza.

“Lakini, vijana wazalendo wamekubali kukaa Katavi na kuhudumia wananchi, hongereni sana," anapongeza Rais Dk. Samia.

Kuhusu fedha ujenzi awamu ya pili ya mradi, Rais Dk. Samia anasema zimeshafika na kutaendelea kujengwa majengo zaidi, kuhakikisha wananchi wa Katavi na mikoa jirani wananufaika na uwekezaji mkubwa wa kiserikali.

Rais Dk. Samia akawaahidi kwamba, Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuzisogeza huduma za afya karibu na wananchi na utoaji wa huduma bora, kwani ndio lengo lake kuhakikisha matibabu yanapatikana ngazi ya msingi, mpaka taifa.

Kwa mujibu Sera ya Afya ya Msingi (MMAM), kila kata kitongoji kinakuwa na zahanati na kituo cha afya kwa kila kata, huku wilaya inaakuwa na hospitali yake, mkoa unabaki kuwa na hospitali ya rufani.

Pia, juu kuna ngazi Hospitali ya Rufani Kanda, kama ilivyo Mbeya na Hospitali ya Taifa Muhimbili, Jakaya Kikwete na MOI za Dar es Salaam, pia Benjamin Mkapa ya Dodoma.

 MKOANI RUKWA

Mnamo Julai 15, Rais Dk. Samia baada ya kutoka mkoani Katavi, akaingia Rukwa alikokamilisha ziara hado jana. Aliianza na kuzindua Hospitali ya Wilaya ya Nkasi, Rukwa yenye majengo na miundombinu ya kisasa, huko Namanyere.

Ni mradi wa majengo shilingi bilioni tano, sasa ikitoa huduma bora zaidi kwa wananchi wake wilayani, hapo nako akawataka wahudumu wa afya kuendeleza moyo na tija katika kuwahudumia wagonjwa ya bila kinyongo.

Hapo akatoa mfano wa mkasa, mtoto aliyezama kwenye maji na kupatiwa matibabu ya haraka hospitalini hapo, sasa anaendelea vizuri, imewezekana kwa hospitali hiyo kuwa na vifaa vya kisasa. 

SAFARI YA MRADI

Hadi sasa, serikali kupitia Wizara ya Afya na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Katavi, inaendeleza ujenzi wa Hospitali ya Rufani Mkoa wa Katavi, kama ilivyoelekezwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Ilikuwa Agosti 25 hadi 27, mwaka 2021, ikaanishwa namna pande zote mbili zinavyoshiriki katika ujenzi wa hospitali hiyo, ikianishwa katika Hati ya Makubaliano (MoU) iliyotiwa saini na Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi.

Katika Hati ya Makubaliano (MoU) iliyosainiwa jukumu kubwa la Katibu Mkuu-Afya ni kuandaa bajeti na kufuatilia upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kuendeleza ujenzi pamoja na kuingia mikataba yote ya ujenzi. 

Inaanishwa, Katibu Tawala Mkoa Katavi, jukumu ni kusimamia matumizi ya fedha za ujenzi kwa kuratibu na kusimamia ununuzi wa vifaa vya ujenzi, malipo ya mkandarasi na Mshauri Elekezi kupitia kamati anazoziunda, kutekelezaji mradi kila siku.

Ujenzi wa Hospitali Rufani Mkoa wa Katavi, unatekelezwa kwa awamu kama, kulingana na upatikanaji fedha.

Awamu ya Kwanza, mradi ulianza na majengo matatu; jengo kuu lenye ghorofa moja lenye Kitalu A na B la kudumia Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto; Huduma za Dharura (EMD); Wagonjwa wa Nje (OPD); Famasia; Radiolojia; Upasuaji; Uangalizi Maalumu (ICU); na jengo la Maabara. 

Ujenzi wake ulianza mwezi Mei, 2018 chini ya usimamizi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi na ilikuwa itekelezwe kwa wiki 48 kwa gharama ya shilingi bilioni 9.7. Ilipofika Februari 2019, mradi ulikabidhiwa kwa Wizara ya Afya ukiwa kwenye hatua ya msingi sawa na asilimia 20 ukiendelea kutekelezwa na Mkandarasi SUMA JKT kwa mfumo wa Kandarasi (Conventional Method). 

Mradi huo uliendelea kutekelezwa kwa utaratibu wa kandarasi mpaka April 2021 ukiwa katika asilimia 43 ya utekelezaji ikishatumia shilingi bilioni 3.6.

Serikali iliamua kubadilisha mfumo wa utekelezaji kwenda kwenye kinachojulikana ‘Force Account’ ili kuharakisha utekelezaji wake.

Serikali kupitia Wizara ya Afya, ilikamilisha taratibu za ununuzi na kumpata Mhandisi Mshauri na Mshauri Elekezi – ‘Crystal Consultant’ na Fundi Mjenzi SUMA JKT. 

Hadi sasa gharama za kukamilisha mradi zinakadiriwa kuwa shilingi bilioni 12, zikijumuisha za ufundi na kwa mshauri elekezi.