MAHITAJI ya kuwa na uchumi unaogusa na kuondoa umaskini, kuainisha gharama na hasara zitokanazo na ukatili wa kijinsia (GBV) kwa taifa na kujenga viwanda vinavyomilikiwa na wanawake, ni mambo yanayotajwa na kinamama kuwa lazima yaingie kwenye dira ya maendeleo ya taifa ya 2050.
Ni maoni ya Mtandao wa Wanawake na Dira, kwa wajumbe wa Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, wanapokutaja kuhakiki rasimu ya dira.
Akifungua pazia la mjadala, Profesa Ruth Meena anasema licha ya rasimu wa dira kutaja kuwa uchumi umekua kwa kipindi cha 2020 hadi 2025, hakuna uhalisia kwasababu haukugusa umaskini.
“Uchumi ulikua lakini umaskini unaongezeka, huko ni kukua kwa vitu lakini sio watu, hata Mwalimu Julius Nyerere alisema uchumi hauwezi kukua kama hauondoi umaskini.” Anakumbusha.
Anawaambia wajumbe wanaokutana na wadau kuhakiki rasimu ya dira ya taifa kuwa lazima dira ionyeshe kuwa taifa linahitaji kuwa na uchumi imara, jumuishi na linganifu unaogusa wanawake na wanaume.
Aidha, hakuna maendeleo kiuchumi kama vikwazo vya kibiashara na uzalishaji vinavyowabana wanawake na kuwabakiza kwenye sekta isiyo rasmi havitaondolewa na dira inayoandaliwa.
Anasema wanawake wanachuuza mboga, matunda kwenye mabeseni mijini, ni mamalishe pembeni ya barabara wakiuza vyakula mbalimbali.
"Lazima kuondoa vikwazo na kuwawezesha wainuke na kufanya biashara kubwa, wamiliki kampuni na viwanda, si uchuuzi na hilo dira ilianishe," Profesa Ruth anasema.
HASARA GBV
Profesa Ruth anasema ukatili wa kijinsia unaligharimu taifa kwenye nguvukazi, tiba, afya ya akili na hata vifo. Kwa hiyo lazima utafiti ufanyike ili kujua hasara na madhara yake kwa nchi.
Anafafanua kuwa wanawake wakiumizwa hawazalishi, wala kutunza na kuhudumia familia, wanahitaji tiba, wanapata matatizo ya shida ya akili, hivyo kurudi tena kwenye umaskini.
"Tunataka utafiti wa hasara GBV ufanyike na takwimu zinazotolewa na mashirika mbalimbali ya kijamii kuhusu wanawake, zitumike ili kupata uhalisi wa madhara, hasara na athari kwa nchi," anasema.
"Tunapotambua madhara yake, tunafahamu hasara kiuchumi, gharama kwenye afya, malezi kupoteza nguvu kazi, mapato ya mwanamke na taifa.”
VIWANDA VIDOGO
Wana mtandao wanataka dira ianishe inapozungumzia uchumi wa viwanda, ni viwanda gani itamke kuwa ni viwanda vidogo na vikubwa vinavyomilikiwa na wananchi.
"Tunahitaji viwanda vidogo vinavyomilikiwa na wanawake vijijini na popote penye uhitaji. Kwa mfano matunda yanaoza barabarani, wanawake wanasuka mikeka vikapu, nyungo na mapambo wako barabarani hakuna soko.
Kwa nini tusijenge viwanda vidogo wakavilimiki? Wakaongeza mnyororo wa thamani wakakua kiuchumi na kuondoa umaskini?” anasisitiza.
Anasema ni wakati dira ya 2050 kuainisha ulazima wa wanawake kupewa ujuzi wa kuzalisha, kufungasha na kuuza bidhaa kutoka kwenye kampuni na viwanda vidogo wanavyomiliki iwe vijijini na popote kwenye unafuu wa upatikanaji wa malighafi.
MANI/USALAMA
Rebecca Gyumi anazungumzia msingi mkuu wa dira wa utawala bora, amani, usalama, utulivu na umoja akisema rasimu ya dira inachukulia uwepo wa amani kwa mtazamo wa 'kizamani' unaomaanisha ni ukosefu wa vita, wakati si hivyo tu.
"Amani ni zaidi ya kukosekana vita, ni kitu kinachoanzia nyumbani, kwa hapa kwetu GBV inakosesha watu wengi amani, wanawake, watoto na wale wanaotuhumiwa kwa uhalifu wanachomwa, albino wanauawa, watoto wananajisiwa ni ukosefu wa amani," anasema Rebeca.
Anataka dira ifafanue kuhusu amani kuwa ni usalama wa kila mtu, iwe nyumbani, sehemu za kazi, ndani ya jamii, shuleni na taifa zima.
Rebeca anakumbusha kuwa iwapo msingi mkuu wa dira ni utawala bora, usalama, amani na utulivu, lakini wanawake wengi, wazee, watoto, wenye mahitaji maalum (albino), wanakatiliwa, hawako salama na kwamba ni vigumu kuwa na taifa na raia wenye kujivunia uwepo wa amani na usalama.
TEHAMA
Anazungumzia usalama na amani kwenye Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na mifumo ya kidijitali kuwa inahatarisha amani, akitolea mfano kuwa inatumika kufanya mashambulizi ya kimtandao dhidi ya wanawake, watoto hata taifa.
"Kwa hiyo dira ionyeshe namna ya kujilinda dhidi ya mashambulizi ya kimtandao kwa watu na taifa. Nchi inaweza kuanzisha vita vya kimtandao dhidi ya nchi nyingine na kuvuruga uchumi na maendeleo ya kijamii," anaonya.
BIMA YA AFYA
Akiwasilisha umuhimu wa bima ya afya kwa kila Mtanzania, Janeth Mawinza, anataka dira itamke kuwa tiba ni haki ya kila Mtanzania bila kujali kipato, hadhi wala makazi.
"Bima ya afya ni kama imebagua imewaacha nje wanawake, ambao wengi hawana ajira, ndio mama lishe, wauza mboga, wachuuzi wa biashara ndogo. Hao ndio wanaowatunza watoto kulea na kutunza familia, lakini hawana bima ya afya," anasema Janeth.
Anasema wanapoumwa, wanaacha uzalishaji watafute dawa kwa ajili ya gharama za kujitibu na kutibu watoto, wakati mwingine hawana pesa za kutosha wanapata huduma duni na hii inachangia vifo vya watoto, kinamama na wanafamilia wengine.
"Ndio maana tunasema bima ya afya iwe ni kwa kila Mtanzania bila kujali kingine chochote kwa sababu utaratibu uliopo hauwagusi wote," anasema.
ELIMU USALAMA
Dk. Avemaria Semakafu anazungumzia kipengele cha kuwana jamii iliyoelimika inayomudu ushindani ndani ya dira akisema pengo linalotakiwa kuzibwa ni dira izungumzie uwepo amani na usalama shuleni.
Ianzie shule ya msingi, sekondari, vyuo vya kati na vikuu iwe ni sehemu salama ya kusoma kwa wote, wenye ulemavu na wazima, kusiwe na GBV.
Anakumbusha ukosefu wa usalama shuleni umesababisha wanafunzi kukwama kielimu na kuongeza kuwa taifa linapoingia kwenye uchumi wa kati, raia walioelimika ni kigezo muhimu cha kufikia lengo hilo.
Akijibu hoja za wana mtandao wanawake, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Nyongo, anawapongeza wana mtandao hao kwa maoni yanayosimama imara kutetea wanawake wote wa Tanzania.
Anasema wanawake wamewasilisha maoni ambayo yanazingatiwa, kwa kuwa hata sasa tume inaendelea kupokea maoni na ushauri kutoka kwa watu mbalimbali.
"Niseme mmewasilisha maoni yenye tija yanayosimamia haki za wanawake wote wa Tanzania. Niseme mmeupiga mwingi," anasema Nyongo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED