RIPOTI zinaonyesha kuwa wanawake wapo kwenye hatari ya kuathirika zaidi na mabadiliko ya tabianchi kuliko wanaume.
Takwimu za Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Mazingira (UNEP), zinaonyesha kuwa asilimia 80 ya wanaolazimika kuhama makazi yao kutokana na mabadiliko ya tabianchi ni wanawake.
Majukumu yao ya ulezi na kuhudumia familia kwa karibu zaidi huwaweka katika mazingira hatari zaidi wakati mafuriko, tufani na ukame vinapotokea.
Wanawake wa Kijiji cha Unguja Ukuu Mkoa wa Kusini Unguja, nao ni sehemu ya changamoto hiyo na kwamba katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi wamethibitisha kuwa ni vinara kutunza mazingira ikiwamo kupanda mikoko.
Mikoko ni miti pekee yenye umuhimu mkubwa katika kudhibiti mabadiliko ya tabianchi, kwa kuhifadhi kaboni na kusaidia kukabili athari za mawimbi makubwa kwenye fukwe za bahari.
Abdi Mgeni Juma, katibu wa kikundi cha kupanda na kuhifadhi mikoko kijijini hapo cha mikoko ni urithi wetu, anasema wanawake ni vinara kuhifadhi mazingira kutokana na ushiriki mzuri katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Anasema kikundi hicho kilianzishwa mwaka 2020 na sasa kina wanachama 150 kati ya hao wanawake 121 na wanaume 29, wenye lengo la kuhifadhi mazingira hasa kupanda na kuhifadhi mikoko kijijini hapo.
Tangu kuanzishwa kwa kikundi hicho kimepanda mikoko 2,900,700 kijiji hapo nguvu kubwa ikitokana na wanawake, anasema.
Aidha, malengo ya kikundi hicho ni kukabili athari za mabadiliko ya tabianchi kutokana na bahari kuvamia makazi ya wanakijiji.
Anasema awali kabla ya kupata taaluma ya uhifadhi, uharibifu wa mazingira ulikuwa mkubwa kijijini hapo lakini kwa sasa uharibifu huo umepunguwa kwa kiasi kikubwa na wananchi hasa wanawake wamehamasika zaidi katika uhifadhi huo.
Akizungumzia changamoto katika uhifadhi anasema, miradi ya maendeleo huchangia uharibifu wa mazingira ambapo ujenzi wa daraja unaoendelea kati ya kijiji hicho cha Unguja Ukuu na Kisiwani Uzi umekata mikoko mingi.
“Tuna masikitiko makubwa, maendeleo tunayataka lakini ujenzi wa daraja hili umerejesha nyuma juhudi zetu za uhifadhi maana zaidi ya mikoko 2,000 imekatwa ili kupisha ujenzi wa daraja,” anasema katibu huyo.
Warda Ramadhan Ali (28) mwanachama wa kikundi hicho, anaeleza kuwa elimu wanayoipata ya uhifadhi wa mikoko huitoa kwa jamii ikiwamo wanafunzi shuleni kutokana na umuhimu wa miti hiyo inauoto wa asili na husaidia kulinda ardhi na mmong’onyoko wa fukwe.
Mikoko pia inasaidia kulinda viumbe vya baharini kama samaki na huzuia maji baharini yasipande juu kwenye makaazi, mashambani na kwenye shughuli za kijamii.
“Kabla ya mikoko haijashambuliwa kwa kukata samaki wengi walikuwapo katika eneo hili na wakati maji yakijaa huja ndege wa kila aina lakini wametoweka. Hivi sasa ndio tumeanza kurejesha hali nzuri ya mikoko,” anaeleza.
Ukataji mikoko kwa mujibu wa maelezo yake ulifanywa na serikali kutokana na kupisha ujenzi wa daraja, na kwamba umerejesha nyuma nguvu za vijana katika kupanda mikoko.
Anawataka vijana wasivunjike moyo na kuzidisha ari na nguvu katika uhifadhi wa mazingira ikiwamo kupanda miti hiyo kwa faida yao na vizazi vya baadaye.
Salama Hussein Makame (52), mwanachama wa kikundi hicho, anasema serikali imekuwa ikihimiza kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi lakini wakati mwingine inachangia kuharibu mazingira kutokana na kulazimika kupisha miradi ya maendeleo ikiwamo ujenzi wa miundombinu ya barabara.
Licha ya wanawake kukabiliwa na majukumu mengi ya kuhudumia familia lakini wanatenga muda wa uhifadhi wa mzingira ikiwamo kupanda mikoko, anasema Salama.
“Wanawake wa kijiji hiki ndiyo tunaongoza kuhifadhi mazingira kwa sababu ndiyo waathirika wakuu na wakati mwingine athari zinapojitokeza ikiwamo upepo mkali au maji ya bahari kuvamia makazi wanaume huwa hawapo majumbani sisi ndio tunaohangaika,” anakumbusha.
Anasema hamasa kubwa ya wanawake wa kijiji hicho kuwa vinara wa uhifadhi wa mazingira kumetokana na kupatiwa elimu ya uhifadhi wa mazingira kutoka mashirika na taasisi mbalimbali kama mradi wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi wa ZAN ADAPTI.
Sheha wa Unguja Ukuu, Khamis Ibrahim Shomari, anakiri mikoko mingi imekatwa kutokana na mradi wa maendeleo, lakini serikali imeamua kufanya hivyo ili wananchi kupata maendeleo na kuondosha changamoto ya usafiri kutokana na maji ya bahari.
Anasema kutokana na jografia ya kisiwa cha Uzi na Ng’ambwa kuzungukwa na bahari wananchi wanapata usumbufu mkubwa katika harakati za kiuchumi, maendeleo na kijamii serikali imeamua kujenga daraja hilo lenye urefu wa kilometa 2.5.
Anawataka wananchi kuendelea kuhifadhi mazingira na kuacha kukata miti hiyo ili kukinusuru kijiji hicho na majanga mbalimbali ya kimazingira.
Shehia ya Unguja Ukuu kwenye wakazi 4,000 wakiwamo wanawake 1,800 na wanaume 2,200 ambapo shughuli kuu za wananchi wa kijiji hicho ni uvuvi na kilimo, akizungumzia kuhusu kukatwa mikoko katika eneo hilo anasema, ni kupisha ujenzi wa daraja kutoka Unguja Ukuu hadi Uzi Ng’ambwa.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Harous Said Suleiman, anasema serikali imelazimika kuikata kupisha ujenzi huo lakini baada ya kukamilika ujenzi watairejesha mikoko hiyo.
“Tutasharikiana na wananchi kupanda tena mikokoko ili kufidia iliyokatwa na serikali imeamua kuikata si kwa nia mbaya bali ni kuwajengea daraja na kurahisisha usafiri,” anasema.
Aidha, anasema kukamilika kwa daraja hilo kutachochea maendeleo hivyo wananchi wasivunjike moyo katika kuendeleza jitihada za kuhifadhi mazingira ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuwa na Zanzibar ya kijani.
Waziri anataja faida za mikoko kuwa ni nyingi kwa mazingira na viumbe hai ikiwamo kupunguza kasi ya mawimbi makubwa ya bahari ambayo yangeharibu matumbawe na ufukweni.
Waziri anasema mikoko ni mazalia ya samaki, hukata kasi ya mawimbi makali, inahifadhi hewa ya ukaa (carbondioxide) kutoka angani na kuzalisha oksijeni kupitia mchakato wa mimea kujitengenezea chakula "photosynthesis".
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED