Mkuu wa Shule ya Sekondari Mugani, wilayani Misungwi, ameiomba Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kusaidia kukabiliana na tatizo la utoro na wanafunzi kuacha shule kutokana na shinikizo la wazazi, ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu na kutimiza ndoto zao.
Tatizo hilo limeelezwa kuwa linachangiwa kwa kiasi kikubwa na wazazi wanaowazuia watoto wao kuhudhuria masomo ili wafanye shughuli kama biashara, kucheza ngoma, kilimo, na uchungaji wa mifugo, bila kujali haki yao ya msingi ya kupata elimu.
Akizungumza katika kampeni hiyo, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Masalu Lweyo, amesema mwitikio mdogo wa wazazi na kutotambua umuhimu wa elimu ndicho chanzo cha tatizo hilo.
"Watoto wanapenda kusoma, lakini changamoto kubwa ni wazazi. Kwa mfano, mwaka huu idadi ya wanafunzi wa kidato cha pili ilipaswa kuwa 78, lakini waliopo ni 49 tu. Wengine wamekuwa watoro na hata hawakufanya mtihani wa kuingia kidato cha pili," amesema Lweyo.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mwaniko, Abdul Abeid, amesema licha ya jitihada zilizofanywa, wazazi wengi bado wanahusika katika kuwazuia watoto kuhudhuria shule, hivyo ni muhimu kuwepo mbinu madhubuti za kushughulikia changamoto hiyo.
"Nimewaandikia barua wazazi waliokaidi, lakini bado wapo wanaogoma kuelewa. Wengine hata hudanganya kuwa watoto wao wamepotea, hadi uwatishe ndipo wanasema ukweli. Tunahitaji msaada mkubwa kuielimisha jamii kuhusu umuhimu wa elimu na kuacha tabia ya kuwatumikisha watoto, jambo ambalo ni ukatili," amesema Abeid.
Wakili Ally Zaid amesisitiza kuwa mtoto ana haki ya kupata elimu, na mzazi yeyote atakayemzuia mtoto wake kuhudhuria shule, au kuficha vitendo vya kikatili anavyofanyiwa mtoto, anavunja sheria.
"Sheria ya Elimu inaposomwa kwa pamoja na Sheria ya Mtoto inaweka wazi wajibu wa mzazi kuhakikisha mtoto anapata elimu. Kukwamisha elimu ya mtoto ni kosa la kisheria," amesema Wakili Zaid.
Naye Ofisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Misungwi, Philimon John, amesema ni wajibu wa wazazi kuwajibika katika malezi na masuala ya elimu kwa watoto wao.
"Serikali imewekeza kwenye elimu na kuhakikisha elimu ya msingi hadi kidato cha sita inatolewa bure. Hivyo, wazazi hawana sababu ya kuwazuia watoto kuhudhuria shule. Wazazi watakaoshindwa kutimiza wajibu wao wanaweza kuchukuliwa hatua za kisheria," amesema John.
Kwa pamoja, viongozi na wadau wa elimu wanasisitiza kuwa juhudi za pamoja zinahitajika ili kuhakikisha watoto wanapata elimu bila vikwazo, huku wazazi wakihimizwa kubadilika na kutambua kuwa elimu ni haki ya msingi kwa kila mtoto na msingi wa maendeleo ya taifa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED