SERIKALI imezindua Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia mkoani Pwani, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha haki inapatikana kwa wananchi wote, hususan wale wenye changamoto za kisheria lakini wasio na uwezo wa kugharamia huduma hizo.
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika leo Februari 24,2025 katika Kata ya Maili Moja, Uwanja wa Stendi ya Zamani, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini amesema kuwa serikali imejipanga vyema katika utekelezaji wa kampeni hiyo, ambapo huduma zitaanza kutolewa kuanzia Februari 25 hadi Machi 5, 2025.
"Wizara imejipanga kwa dhati katika utekelezaji wa kampeni hii, na mara baada ya uzinduzi tutaanza kutoa huduma hizo katika mkoa wa Pwani kuanzia kesho, huduma zitakazotolewa ni pamoja na utoaji wa elimu ya kisheria, utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala, kuandaa nyaraka za kimahakama, kuwakilisha wananchi kwenye vyombo vya utoaji haki, pamoja na ushauri wa kisheria," amesema Sagini.
Amefafanua kuwa kampeni hiyo itatekelezwa katika kata 10 za mkoa wa Pwani, ambapo kila kata itajumuisha vijiji au mitaa isiyopungua mitatu, hivyo kufikia vijiji 30 kwa kila halmashauri.
Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Hamis Mtupa, ameomba Serikali kutambua vyeti vya ndoa vinavyotolewa na dini ya Kiislamu ili kuepusha usumbufu unaowakumba waumini wa dini hiyo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Shekhe Mtupa amesema kuwa licha ya waumini wa Kiislamu kupewa vyeti halali vya ndoa na viongozi wa dini yao, mara wanapovipeleka Serikalini hukataliwa kwa madai kuwa havitambuliki kisheria.
"Tunaomba Serikali ifanye maboresho ili vyeti vya ndoa za Kiislamu vitambulike kisheria. Waumini wetu wanakumbwa na usumbufu mkubwa wanapovipeleka Serikalini na kuambiwa vinapaswa kuwa vya ndoa za Serikali, wakati ndoa zao hazikufungwa huko," amesema Mtupa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kupata msaada wa kisheria katika masuala ya ndoa, ukatili wa kijinsia na migogoro ya ardhi. Amesema kampeni hiyo ni sehemu ya juhudi za kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, katika kuhakikisha changamoto za kisheria zinatatuliwa.
Kunenge amebainisha kuwa kampeni hiyo itafanyika katika halmashauri zote na wilaya saba za mkoa huo, ambapo wananchi watapata fursa ya kusikilizwa na kupatiwa msaada wa kisheria kuhusu migogoro yao.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaid Hamis, amewasihi wananchi kufika kwenye vyombo vya sheria mara wanapokumbwa na changamoto, badala ya kubaki na matatizo bila msaada wa kisheria.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED