Wakandarasi wasimamiwe kutekeleza miradi ya nishati kwa wakati - Kapinga

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:13 AM Feb 24 2025
Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga.

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amewataka watendaji wa Sekta ya Nishati kuwajengea uwezo watoa huduma wanaotekeleza miradi mbalimbali ya sekta ya nishati nchini.

Hayo ameyasema Februari 23, 2025 na Kapinga wakati akizungumza na wafanyakazi wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO, na wakuu wa taasisi za wizara kabla ya kushiriki ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan iliyoanza jana mkoani Tanga.

"Tunataka hii miradi ikamilike kwa wakati na kwa ubora mkubwa, wakandarasi wajengewe uwezo wa utendaji kazi ili kazi ionekane inafanyika, " alisema Kapinga. 

Aidha, aliipongeza REA kwa kumaliza kufikisha umeme kwenye vijiji vyote nchini na kusisitiza miradi inayoendelea na ile inatakayoanza mwaka huu wa fedha itekelezwe kwa wakati. 

"Ni muhimu sana kuwasimamia wakandarasi kwa nguvu kuanzia mwanzo tuwe nao makini ili miradi hii ya kupeleka umeme kwenye vitongoji ikamilike kwa wakati, " alisema Kapinga

Katika hatua nyingine, Kapinga aliwataka watendaji wa taasisi za nishati kuwa na mahusiano mazuri na wananchi hususan wakati wa kupitisha miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao.

"Imarisheni mahusiano na wananchi mnapopitisha miradi yetu na kuwaeleza kuwa Serikali italipa fidia kwa wote miradi hiyo ilipopita," alisema Kapinga