WAKATI zikiwa zimebaki raundi 10, kabla ya Ligi Kuu Tanzania Bara kumalizika, baadhi ya wachezaji wameanza kujipambanua na kuendelea kujiwekea rekodi ambazo zinaweza kuwafanya kutwaa tuzo mbalimbali mwishoni mwa msimu.
Mbali na baadhi ya timu kuwania ubingwa, zipo zinazowania kuwapo nne bora, zingine zikipambana kuepuka kushuka daraja, wachezaji nao wanapambana kuweka rekodi zao ili kujiongezea wasifu na kujipambanua kwa uwezo wao binafsi kwenye ligi.
Katika makala haya tunakuletea wachezaji 10 walioweka rekodi mbalimbali kwenye Ligi Kuu mpaka sasa, twende sasa...
1# Moussa Camara - Simba
Kipa, Camara, amefikisha mechi 15 kukaa langoni bila kuruhusu bao, akiweka rekodi iliyoachwa na kipa Ley Matampi wa Coastal Union msimu uliopita.
Matampi, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, alimaliza ligi akiwa na 'clean sheets' 15 na kuwa kipa bora wa msimu, hivyo Camara raia wa Guinea, amebakisha michezo 11 kama atasimama langoni ili kuvunja rekodi hiyo.
Kama atasimama langoni bila kuruhusu bao kwenye mchezo wa leo dhidi ya Azam FC, atakuwa tayari ameivunja rasmi rekodi hiyo.
2# Selemani Bwenzi - KenGold
Bwenzi aliweka rekodi ya kufunga bao katikati ya uwanja, dakika nne kabla ya mchezo wa Ligi Kuu kati ya Yanga na KenGold kumalizika, uliochezwa Februari 5, mwaka huu, Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.
Ni bao lilizozua gumzo kubwa kwa sababu aliyemfunga ni mmoja wa makipa bora kabisa kwenye Ligi Kuu ya Tanzania, Djigui Diarra.
Wakati Yanga ikipachika bao la sita, wachezaji wa KenGold walikwenda kuanza mpira, ambapo mchezaji huyo badala ya kuanza kwa kupasia wenzake, aliamua kuupiga moja kwa moja juu kuelekea kwenye lango la wapinzani wao, licha ya juhudi za Diarra, lakini mpira ukajaa wavuni.
Mchezaji huyo aliyesajiliwa na KenGold dirisha dogo la usajili akitokea, Mbeya Kwanza, akimchungulia kipa Diarra aliyekuwa amesogea mbele kidogo. Ni moja ya bao linalotajwa kuwa linaweza kuwa moja ya mabao bora msimu huu, au kutwaa tuzo ya kuwa bao bora la msimu.
3# Jean Ahoua - Simba
Kiungo mshambuliaji wa Simba, Ahoua, raia wa Ivory Coast, anaongoza kwa kufunga penalti nyingi kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara mpaka sasa. Ameshapachika zote tano ambazo ni nusu ya penalti ambazo timu yake imezipata.
Simba imepata penalti 10, ikiwa ni timu inayoongoza kwa wachezaji wake kufanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari, ikifunga tisa na moja ikikoswa na Leonel Ateba.
Ahoua, amefunga zote tano ambazo amepewa kupiga, huku mwenzake Ateba, akifunga nne na kukosa moja kwenye mchezo uliopita dhidi ya Namungo.
4# Ismail Mgunda - Mashujaa FC
Mara nyingi mabao ya vichwa hufungwa ndani ya eneo la hatari, lakini Mgunda wa Mashujaa FC aliweka rekodi ya aina yake Oktoba 21, mwaka jana, kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma, alipofunga bao la kichwa akiwa nje ya boksi, wakati timu yake ikicheza dhidi ya KenGold.
Krosi iliyopigwa kutoka wingi ya kulia, ilimkuta straika huyo akiwa amesimama nje ya boksi na mabeki wawili, akaruka juu zaidi yao na kuupiga kichwa mpira ukaenda kujaa wavuni katika mchezo uliomalizika kwa wenyeji kushinda mabao 3-0. Mpaka sasa ndiyo bao pekee kwenye Ligi Kuu lililofungwa kwa kichwa, nje ya boksi. Straika huyo ameihama timu hiyo kipindi cha dirisha dogo la usajili na kwenda kujiunga na Klabu ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
5# Shomari Kapombe - Simba
Beki wa kulia, Kapombe ndiye beki aliyesababisha penalti nyingi kwenye Ligi Kuu na kuipa faida timu yake ya Simba.
Katika mchezo wa Jumatano iliyopita dhidi ya Namungo FC, Kapombe aliiwezesha timu yake kupata penalti mbili, ambazo zote alifanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari.
Mpaka sasa ameipatia timu yake penalti nne. Alifanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari, kwenye mchezo dhidi ya JKT Tanzania na KenGold.
6# Yoro Diaby - Azam FC
Hili ndilo bao lililofungwa kwa umbali mrefu zaidi kuliko yote kwenye Ligi Kuu Tanzania mpaka sasa.
Wakati bao la Bwenzi likiwa linashikilia rekodi ya kufungwa katikati ya uwanja, Yoro Diaby ya Azam FC, aliivunja rekodi hiyo, Februari 15, mwaka huu, alipofunga bao akiwa kwenye robo tatu ya Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Alipiga faulo akiwa kwenye nusu ya uwanja upande wa lango la Azam, ambayo haikuonekana kama inaweza kuwa na madhara makubwa, lakini akafunga bao la pili, dakika nane kabla ya mechi kumalizika, timu yake ikishinda mabao 2-0 dhidi ya Mashujaa FC.
Mchezaji mmoja wa Mashujaa alicheza faulo ambayo kwa umbali wa zaidi ya mita 70 hivi ilionekana ya kawaida tu, lakini mpigaji alikuwa amegundua kipa Patrick Muntary alikuwa amesogea sana langoni, ndipo alipofanya maamuzi magumu ya kuupiga juu, moja kwa moja langoni. Na kweli akafanikiwa kulenga shabaha, mpira ukajaa wavuni, bao ambalo nalo linatajwa kuwa huenda likampa tuzo mwishoni mwa ligi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED