SHIRIKA la World Wildlife Fund (WWF), limepeleka kwa wananchi wa vijiji vinne vya Alaililai, Gelai Lumbwa, Noondoto na Orpurkeri katika Wilaya ya Longido, mkoani Arusha, miradi ya kiuchumi ya unenepeshaji wa mbuzi, ili kuwasaidia wananchi hao kuwa na kipato mbadala,kitakachowasukuma kuachana na shughuli za kibinadamu zinazoharibu uhifadhi.
Uwezeshaji huo wa kuongeza kipato kwa jamii ya kifugaji ya Kimasai, unatekelezwa na WWF, kupitia Mradi wake wa ‘Land 4 Life.’
Akizungumza na wana vijiji hao mwishoni mwa wiki, wakati wa hafla ya kukabidhi mbuzi 326 kwa vikundi vya wajasiriamali wa ufugaji, Msimamizi wa Mradi wa SOKNOT (Southern Kenya, Northern Tanzania), Prof. Noah Sitati, alisema WWF inatamani kuona maisha ya jamii hiyo ya Kimasai yakibadilika kiuchumi, kupitia unenepeshaji wa mbuzi watakaouzwa kila baada ya miezi minne.
“Tunataka tukija kuwatembelea tuone maisha ya watu yamebadilika, tunataka tuone watoto wameweza kwenda shule na afya za watu ziko vizuri. Kwa sababu kuna kipato wanapata kupitia mradi wa unenepeshaji mbuzi kibiashara. Nimepita huko barabarani sijaona mkaa; hii inamaanisha kwamba mnatunza mazingira.
“Kwa jamii ya kifugaji ya Kimasai hiki sio kitu kigeni kwenu, sema ni ile mnatakiwa kupata elimu zaidi ili muweze kuboresha hii mifugo iwasaidie katika maisha yenu. Tunataka kuona vijana wengi wanajiajiri kupitia mradi huu, na pia wanawake ambao ni wengi zaidi wanufaike kiuchumi.”
Prof. Sitati, alisema katika Kijiji cha Lumbwa, kila kikundi kimepewa mbuzi 15, ambapo asilimia 90 ni madume (beberu) na majike ni asilimia 10 kwa ajili ya uzalishaji wa maziwa.
Alisema vikundi vilivyonufaika katika Kijiji cha Lumbwa, kwa kupata jumla ya mbuzi 75, ni Napokie, Enyorata, Noongishu, Memusi na Nodupoi.
Mshauri wa Masuala ya Biashara wa WWF, Frank Damson, unenepeshaji huo wa mbuzi, ni sehemu ya uhamasishaji uhifadhi na kuiwezesha jamii kwenye masuala ya kipato.
Kwa mujibu wa Damson, Kijiji cha Alaililai, vikundi vilivyonufaika ni Naraposho na Esupati Mazingira ‘C’
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Simon Oitesoi, akizungumzia mradi huo alisema: “Kwa kweli tumepokea mradi huu kwa furaha kubwa sana. Kwa sababu, vikundi vingi vinataka kuja kujifunza kwetu jinsi ya kufuga kibiashara; kwa kunenepesha na kuuza kwa wakati. Vikundi hivi, vitaanza kuuza mbuzi walionenepeshwa mwezi Julai mwaka huu na watatunza fedha, kwa ajili ya kununua mbuzi wapya mwezi Novemba.”
Mmoja wa wanufaika wa mradi huo, Steven Mollel, ambaye ni Mwenyekiti wa Vikundi vya Kijiji cha Lumbwa, aliishukuru WWF kwa kuwaanzishia mradi huo na kutoa elimu kwa vikundi kuhusu ufugaji mbuzi, kwa lengo la kuinua uchumi wa vikundi hivyo na mwananchi mmoja mmoja.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED