Chama cha National League for Democracy (NLD) kimesema kuwa, licha ya changamoto na madhila iliyopewa katika ushirikiano wa kisiasa, hakitasita kushiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Kauli hiyo imetolewa jana, Februari 23, 2025, na Katibu Mkuu wa chama hicho, Doyo Hassan Doyo, wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kamati Kuu ya chama hicho uliofanyika Buguruni, Ilala, jijini Dar es Salaam.
Doyo alisisitiza kuwa, licha ya kauli ya Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Tundu Lissu, aliyesema "No reforms, no election", NLD haijaunga mkono msimamo huo. Badala yake, chama hicho kitaendelea kuwaeleza wananchi sera zake ili kupata ridhaa ya kushika nafasi mbalimbali za uongozi kupitia sanduku la kura.
Akizungumzia ushirikiano wa vyama vya upinzani katika kukabiliana na CCM kwenye Uchaguzi Mkuu ujao, Doyo alieleza kuwa NLD ni miongoni mwa vyama vilivyoathirika na Muungano wa UKAWA mwaka 2015.
"Vyama vya siasa vipo 19, ikiwemo NLD. Sisi hatuendi msituni wala hatususii uchaguzi, bali tunaenda kuwaeleza wananchi sera zetu ili watupe ridhaa ya kuwaongoza," alisema Doyo.
Alieleza kuwa mwaka 2015, vyama vya NLD, CUF, CHADEMA, na NCCR-Mageuzi viliungana kwa lengo la kuiondoa CCM madarakani, lakini NLD ilidhurumiwa kwa kuwaondoa wagombea wake wa nafasi mbalimbali za uchaguzi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taifa wa NLD, Mfaume Khamis Hassan, wakati akifungua mkutano huo, ameomba serikali inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuwapatia ajira za kudumu walimu wanaojitolea.
Aidha, Mwenyekiti huyo amewataka Watanzania kuendelea kudumisha amani ya nchi na kuepuka vyama vya siasa vinavyohamasisha uvunjifu wa amani.
Katika hatua nyingine, Mfaume amempongeza Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuteuliwa kuwa mgombea wa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku akimtakia kila la kheri katika safari yake hiyo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED