Zelensky: Nipo tayari kuuachia urais ili Ukraine ijiunge na NATO

By Enock Charles , Nipashe
Published at 12:47 PM Feb 24 2025
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky.
Picha: Mtandao
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky.

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky amesema yuko tayari kuachia urais wake ili kufanikisha amani, huku Ukraine ikitimiza miaka mitatu tangu kuvamiwa rasmi na Urusi, Februari 24, 2025.

"Iwapo mnahitaji niondoke kwenye kiti hiki, nipo tayari kufanya hivyo. Na pia naweza kufanya hivyo ili Ukraine kuwa mwanachama wa NATO," alisema rais huyo wa Ukraine alipoulizwa swali katika mkutano na waandishi wa habari.

Kauli yake imekuja baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kumuita Zelensky "dikteta" mapema wiki hii.

"Sikuudhika [na kauli hiyo], lakini dikteta angeudhika," Zelensky alijibu Jumapili, akisisitiza kuwa alichaguliwa kidemokrasia mnamo Mei 2019.

Zelensky alisema kwa sasa amejikita katika masuala ya usalama wa Ukraine na kwamba si ndoto yake kubaki madarakani kwa muongo mmoja.

Sheria za Ukraine zinakataza kufanyika kwa uchaguzi wakati kukiwa na vita, hali ambayo imekuwepo tangu Urusi ilipoanzisha uvamizi wake Februari 2022.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya na dunia wanatarajiwa kuelekea Kyiv leo Jumatatu kuonyesha mshikamano wao na Ukraine na kujadili hali ya usalama. Waziri Mkuu wa Hispania Pedro Sanchez, Rais wa Baraza la Ulaya Antonio Costa, na Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen ni miongoni mwa wale wanaotarajiwa kushiriki mkutano huo ana kwa ana.

Chanzo: Bbc Swahili