TPA yaongeza idadi ya shehena bandarini kwa asilimia 15.23

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 04:07 PM Feb 24 2025
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa
Picha: Mtandao
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa

KATIKA kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, shehena iliyohudumiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imeongezeka kwa wastani wa asilimia 15.23 kwa mwaka, kutoka tani milioni 20.78 mwaka 2021/22 hadi tani milioni 27.55 mwaka 2023/2024.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa, alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio yaliyopatika katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita.

Kadhalika, alisema jumla ya shehena iliyohudumiwa katika Bandari ya Dar es Saalam, iliongezeka kwa wastani wa asilimia 13.38 kwa mwaka kutoka tani milioni 18.67 mwaka 2021/22 hadi tani milioni 23.98 mwaka 2023/2024.

Alisema, ongezeko la shehena limetokea baada ya serikali ya awamu ya sita kukamilisha miradi mbalimbali ya ujenzi na maboresho ya miundombinu ya Bandari nchini, ikiwa ni pamoja na kukamilisha mradi wa maboresho na uendelezaji wa Bandari ya Dar es Salaam (Dar es Salaam Maritime Gateway Project – DMGP), ambao umewezesha kuanza kuja kwa meli kubwa zilizokuwa zinashindwa kuja katika Bandari ya Dar es Salaam kabla ya maboresho na uendelezaji huo kufanyika.