Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kimeandaa kambi maalum ya uchunguzi wa afya kwa wananchi, itakayofanyika katika Kampasi ya Mloganzila kuanzia Februari 26 hadi 27, 2025, kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni.
Akizungumza na waandishi wa habari, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Appolinary Kamuhabwa, amesema kambi hiyo inalenga kutoa uchunguzi wa magonjwa mbalimbali, yakiwemo macho, masikio, pua na koo, kinywa na meno, saratani ya matiti na shingo ya kizazi, homa ya ini, pamoja na tezi dume kupitia vipimo vya damu.
Aidha, sambamba na uchunguzi huo, wataalamu wa MUHAS watatoa elimu kuhusu madhara ya matumizi holela ya dawa na usugu wa dawa mwilini, magonjwa ya kuambukiza, utengenezaji na ukarabati wa vifaa tiba, uchakataji wa taarifa za afya kwa kutumia akili mnemba, pamoja na lishe bora.
Prof. Kamuhabwa ameongeza kuwa kutakuwa na maonyesho maalum ya afya na elimu, yakionesha mafanikio katika sekta ya afya na elimu, zikiwemo tafiti mpya, ubunifu wa kiteknolojia, na juhudi zinazofanywa na MUHAS katika kuboresha huduma za afya nchini.
Katika kuimarisha mazingira ya mafunzo, huduma za afya na tafiti, MUHAS pia itaweka jiwe la msingi kwa ujenzi wa Ndaki ya Tiba (College of Medicine) na Shule ya Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) katika Kampasi ya Mloganzila.
“Mradi huu ni hatua muhimu katika kupanua miundombinu ya chuo, kuongeza udahili wa wanafunzi, na kuboresha ubora wa mafunzo kwa wanataaluma wa sekta ya afya,” ameongeza Prof. Kamuhabwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED