Wananchi Misungwi waomba utatuzi wa migogoro ya ardhi

By Neema Emmanuel , Nipashe
Published at 08:04 PM Feb 24 2025
Wananchi Misungwi waomba
 utatuzi wa migogoro
ya ardhi.
Picha: Mpigapicha Wetu
Wananchi Misungwi waomba utatuzi wa migogoro ya ardhi.

Wananchi wa vijiji mbalimbali wilayani Misungwi, mkoani Mwanza, wameiomba Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kusaidia kutatua aina mpya ya migogoro ya ardhi, inayotokana na watu waliotelekeza maeneo yao kwa miaka mingi kurejea na kudai ardhi hizo.

Katika mkutano wa kampeni hiyo, wananchi walieleza kuwa baada ya ardhi hizo kubaki mapori kwa muda mrefu, uongozi wa vijiji ulizigawa kwa wahitaji wengine ili ziweze kuendelezwa. Hata hivyo, wamiliki wa awali sasa wanarejea na kudai ardhi hizo, hali inayosababisha migogoro mikubwa, ikiwemo mapigano.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ilalambogo, Kata ya Lubili, Malongo Mashinje, amesema kuwa wengi wa wanaorejea hawana nia ya kuishi katika maeneo hayo, bali hutumia madai yao kama njia ya kuuza ardhi na kuondoka tena.

"Wanakuja kwa madai ya kujengea makaburi ya wazee wao, lakini mara wanapomaliza, huanza kudai ardhi waliyotelekeza kwa zaidi ya miaka 40, hali inayoanzisha migogoro mikubwa, wakati mwingine hata mapigano kwa kutumia mapanga. Tunashukuru wataalamu wa sheria mmefika hapa, tunaomba mtufafanulie taratibu za kisheria na mtusaidie kutatua changamoto hii," amesema Mashinje.

Pamoja na migogoro ya watu kurejea kudai ardhi waliyotelekeza, wananchi pia wameeleza kuwa migogoro mingine inatokana na uuzaji holela wa ardhi bila kushirikisha majirani, jambo linalosababisha wanunuzi kuvuka mipaka yao, aidha kwa makusudi au kwa kupotoshwa na wauzaji.

Katika Kijiji cha Mwagimagi, Kata ya Buhunda, changamoto ya watu kurejea kudai ardhi waliyotelekeza pia imejitokeza kwa kiwango kikubwa, na wananchi wamependekeza kuwa kampeni hiyo ifanye mikutano ya mara kwa mara vijijini ili kusaidia kutatua migogoro hiyo.

Aidha, wananchi wameeleza kuwa kuna migogoro ya ardhi ambayo tayari imeshatolewa maamuzi mahakamani, lakini walioshindwa bado wanaendelea kuvamia maeneo husika, hali inayohatarisha amani.

Mmoja wa wananchi, Amos Masanja, amelalamika kuwa licha ya kushinda kesi mahakamani na kufuata taratibu zote za kukazia hukumu, bado mvamizi wake anaendelea kumletea vurugu.

"Mahakama Kuu imenipa ushindi na nimefuata taratibu zote, lakini bado mvamizi wangu anaendelea kufanya fujo. Kwa kuwa wataalamu wa sheria mpo hapa, naomba msaada wa kisheria ili jambo hili lipate suluhisho la kudumu," amesema Masanja.

Wakili wa Kujitegemea, Ally Zaidi, amewaeleza wananchi kuwa kisheria, ardhi inayotelekezwa kwa zaidi ya miaka 12 inaweza kuchukuliwa na mtu mwingine na kuendelezwa kihalali.

"Sheria inaeleza kuwa kama ardhi imetelekezwa kwa zaidi ya miaka 12, mtu mwingine anaweza kuimiliki kisheria kama hakuna mtu aliyejitokeza kudai haki yake ndani ya kipindi hicho. Ikiwa wanasema waliohama wamekaa zaidi ya miaka 40 bila kurudi, basi waliyochukua na kuiendeleza wana haki ya kumiliki ardhi hiyo kwa mujibu wa sheria," amesema Wakili Zaidi.

Wananchi wametaka serikali na wataalamu wa sheria kuingilia kati suala hili ili kuhakikisha migogoro ya ardhi inatatuliwa kwa haki na kudumu, huku sheria zikifuatwa ili kuzuia migongano inayoweza kuathiri amani ya jamii.