JICHO SIKU YA WANAWAKE; Miongo mitatu Tanzania ikitembea

By Gaudensia Mngumi , Nipashe
Published at 09:11 PM Feb 24 2025
iongozi wa TWCC, Mercy Sila (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji, Mwajuma Hamza, wakionyesha vazi linalozalishwa na kiwanda kinachomilikiwa na wanawake
Picha: Mtandao
iongozi wa TWCC, Mercy Sila (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji, Mwajuma Hamza, wakionyesha vazi linalozalishwa na kiwanda kinachomilikiwa na wanawake

KILA mwaka Machi 8 ni maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani. Ni wakati ambao wanawake huangalia nyuma kutathmini maendeleo yaliyopatikana katika sekta zote iwe kisiasa, kiuchumi, elimu na taaluma, afya na maendeleo ndani ya jamii.

Pengine wapo wanaohoji kwanini wanawake? Sababu zipo mojawapo mifumo kandamizi ndani ya jamii. Ni mila potofu mfano mwanamke haruhusiwi kurithi, anapigwa, kubakwa, kurithi wajane, kutumikishwa na kuuawa.

Yote yalihitaji kampeni na hamasa kubadilisha mitizamo ya kidunia ili kuwapa wanawake heshima ya utu wao, ulinzi na nafasi ya kuchangia maendeleo.

Moja ya juhudi hizo ni Mkutano wa Beijing 1995 huko China, uliotoa maazimio ya kubadilisha mifumo kuwaondolea wanawake umaskini, kuwapa elimu bora, afya, kuwezeshwa kiuchumi, kimadaraka na kumwezesha mtoto wa kike. 

Katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake mwaka huu, dunia inamulika miaka 30 baada ya Mkutano wa Beijing. Serikali na wadau wanatazama mafanikio, matarajio, matatizo na changamoto zinazowakabili wanawake sasa. 

Kinachopewa kipaumbele ni je, maazimio yaliyopitishwa Beijing yametekelezwa? Au bado safari ni ndefu? Vipi mafanikio yameanza kujitokeza. Kuna tofauti zipi zinazojionyesha wazi, kwa upande wa wanawake, miaka 30 baada ya Beijing, hali ilikuwaje wakati huo na hivi leo kipi cha kujivunia?

TANZANIA NA BEIJING

Kwa Tanzania mengi yamefanyika kutekeleza maazimio ya Beijing, yanayosimama na kauli mbiu ya mkutano iliyojinasibu “Kuwezeshwa wanawake ni kuwezesha jamii ya kimataifa”. Yapo mengi kwenye kulinda haki za wanawake na kutetea usawa wa kijinsia.

 Mfano, Tanzania ina Rais mwanamama Samia Suluhu Hassan, ambaye ameongoza taifa kwa ujasiri. Akichukua uongozi baada ya kifo cha mtangulizi wake John Magufuli. Ameleta mageuzi yanayoboresha maisha, kukuza uchumi na kuleta amani akisimamia michakato ya kuwa na demokrasia pana na maendeleo.

Mathalani, ujasiri wake unaonekana kwenye kusimamia miradi ya mabilioni ya fedha, ya kimkakati iliyoachwa na serikali ya awamu ya tano, anaelekeza nguvu zaidi, ambapo pengine watu walihofu itakwama.

Mfano ni Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere linalogharimu trilioni 6.5, ujenzi daraja la Busisi trilioni 0.7 likiunganisha Mwanza na Geita. Ipo reli ya SGR inayogharimu trilioni 10.7 akitafuta fedha na kukamilisha kazi kama mipango ilivyoelekeza.

Amethibitisha kuwa wanawake wanaweza na juhudi zaidi za kuwawezesha wanawake kwenye uongozi zimeonekana wakiongoza bunge, wizara nyeti ikiwamo ya Ulinzi.

Beijing +30 inashuhudia kuinuliwa wanawake kila mahali eneo la muhimu ni kwenye maamuzi na uongozi wa kisiasa, katika Bunge la Tanzania kuna wabunge 392 kati yao wanawake ni 148, ambayo ni asilimia 37, inasema Ofisi ya Bunge.

Wakati kwa upande wa Zanzibar idadi yao katika Baraza la Wawakilishi (BLW) ni 29 , wanaume wakiwa 49, ni kwa mujibu wa Ofisa Uhusiano wa BLW Hamid Haji Choko. Ni mafanikio katika kufikia utekelezaji wa Maazimio ya Beijing na Protokali ya Mapato ya Umoja wa Afrika inayoagiza usawa wa kijinsia kwa kiwango cha uwiano wa 50/50 wanawake kwa wanaume. 

KIUCHUMI

Biashara na uwekezaji ndiyo habari ya dunia ya sasa. Uwezeshaji wanawake kibiashara na kiuchumi ili kuuza nje na ndani, juhudi zimefanyika kwa Tanzania.

Kwa mfano kuna VIKOBA karibu kila mahali nchini ili kuweka akiba na kukopa fedha kwa ajili ya wanawake kujiendeleza.

Aidha, kipo chama cha kibiashara cha Tanzania Womens’ Chamber of Commerce (TWCC), chenye wanachama karibu nchi nzima. 

Katika muktadha huo wakati wa Beijing mwaka 1995 mambo haya yakuwapo. Huenda hapakuwa na wanawake wanaofahamika wafanyabiashara.

Leo hii TWCC inaimarisha ushiriki na ushindani wa wanawake kwenye maeneo mbalimbali ya bishara, uchumi na uwekezaji.

Mapema mwezi huu chemba ya wanawake wafanyabiashara inazindua mpango wa ‘Twende Sokoni Afrika,’ unaofunza, kuwapa maarifa ya kibiashara, uwekezaji na kuwafikisha wanawake wa Tanzania kwenye Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA), anasema Mkurugenzi Mtendaji wa TWCC, Mwajuma Hamza.

Kwa kuanzia chemba itawafunza wanawake vinara 50 watakaokwenda kwenye soko la pamoja la Afrika, yenye zaidi ya watu bilioni 1.2.

Anaamini AfCFTA itawafanya wanawake wa Tanzania na Afrika kuwa sehemu ya eneo huru la biashara bora duniani.

Licha ya juhudi hizo mitaji na ushirikishwaji wanawake wa vijijini inahitaji kufanyiwa kazi zaidi.

ELIMU WAMEONGEZEKA

Serikali ya awamu ya tano iliasisi sera ya kugharamia elimu watoto wote hawalipi ada tangu chekechea hadi kidato cha nne. Maamuzi hayo ya kimapinduzi yanamaliza mgogoro kwani wazazi na walezi walijiuliza nani asomeshwe mtoto wa kike au wa kiume?

Wanamtandao wa Wanawake na Dira, wanakiri kuwa kumekuwako na mafanikio ya kupunguza au kuondoa pengo la jinsia tangu kufanyika Mkutano wa Beijing na kufikia maazimio  mfano kwenye  elimu  kuanzia  shule za awali, msingi, sekondari hadi vyuo vikuu. 

Kumekuwako pia na kuboresha miundo mbinu, ujenzi wa madarasa mapya, kuongeza vyuo vya elimu, vikuu na jitihada za kuboresha mitaala. Ujenzi wa bweni za wasichana ni eneo

lingine lililowezesha ongezeko la ushiriki wa watoto wa kike katika kupata elimu bora.

Mtandao wa wanawake na dira, unaochambua mafanikio na mapengo ya kijinsia katika dira inayomalizika na mpya inayoandaliwa ya 2050 wanasema kwa kipindi cha miaka mitatu (2017-2019) kumekuwa na usawa kwenye usajili wa watoto, mfano wa watoto wenye miaka 7-13 wa shule za msingi, wasichana walikuwa asilimia 78 na wavulana asilimia 73.

Aidha, waliosajiliwa sekondari kidato cha kwanza hadi cha nne wasichana walikuwa asilimia 45.7 na wavulana asilimia 45.7. Kadhalika waliomaliza sekondari wasichana walikuwa asilimia 39.3 na wavulana asilimia 33.6.

Ila kukawa na upungufu, kwa upande wa kidato cha tano na sita, asilimia kubwa zaidi ya wavulana wanasajiliwa ukilinganisha na wasichana. Wavulana katika ngazi hii ni asilimia 60 ukilinganisha na asilimia 40 wasichana.

Kiwango cha wasichana wanaojiunga na vyuo vikuu kimeongezeka na kufikia asilimia 35.4. Katika vyuo vikuu na vya kati, pengo la jinsia ni kubwa zaidi. Kwa mfano, katika mwaka wa masomo wa 2020-2021, zaidi ya wanafunzi 206,000 walihitimu vyuo, vijana wa kiume wakiwa ni asilimia 57.

Zaidi, pia serikali ya awamu ya sita inasimamia sera ya‘re-entry’ inayowarejesha shuleni wasichana wote waliokwama kumaliza masomo kutokana na vikwazo. Ni juhudi ambazo zinaonyesha Tanzania inatembea na maazimio ya Beijing.

MIKOPO 4:4:2

Suala la kutoa mikopo kwa ajili ya maendeleo ni jambo linalowaingiza wanawake kwenye mikopo umiza au kausha damu. Si rahisi kupata fedha na hata wanawake wanapoomba pesa kwenye taasisi za kifedha hasa benki ni ngumu kwa vile hawana dhamana. Ni mali isiyohamishika kama ardhi, magari na majengo.

Juhudi zimefanyika na mikopo ya halmashauri inayotoa asilimia nne  kwa wanawake na vijana na asilimia mbili kwa wanaoishi na ulemavu ni juhudi za kuwainua wanawake kiuchumi kama maazimio ya Beijing yanavyoelekeza.

Lengo ni kupunguza au kuondoa mapengo ya jinsia kiuchumi na kuwawezesha wanawake ambao wengi ni maskini katika maeneo mengi kama biashara, kumiliki vitega uchumi na kuingia ubia kwenye biashara.

SHERIA KIUPENDELEO 

Sheria ya Ununuzi wa Umma (Public Procurement Amendment Act, 2016), inawapa wanawake, vijana na wenye mahitaji maalumu upendeleo kwamba asilimia 30 ya kazi za manunuzi au zabuni za umma ziachiwe kundi hilo.

Lengo ni kuwawezesha kufanyakazi na serikali kwenye zabuni ili  kuwainua kiuchumi na kibiashara. Ni hatua za makusudi za kuwezesha kushirikiana na serikali kuwawezesha kiuchumi.

CHANGAMOTO

Baadhi ya wanawake mijini na vijijini wanakabiliwa na ukatili wa kijinsia, kupigwa na wenza hata kuuliwa. Hunyimwa fursa kama nafasi za uongozi mfano kwenye ubunge au udiwani wanakumbana na vikwazo, zipo mila potofu mfano ndoa na mimba utotoni, waruhusiwi kurithi ardhi, pia upatikanaji mikopo ya kibiashara ni mgumu.

Serikali inakumbushwa kurekebisha Sheria ya Ndoa ya 1971 ambayo Mahakama Kuu na Rufani zimeagiza baadhi ya vifungu kandamizi vifutwe. Kuna Sheria ya Kazi na Mahusiano Kazini ambazo ni kikwazo kwa sababu inaendeleza ajira za watoto nayo itupwe jicho.

Mwisho 

PICHA: 

V. PICHA: MWANDISHI WETU