VINARA wa Ligi Kuu England (EPL), Liverpool watacheza na Paris St-Germain katika hatua ya 16-bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Wapinzani wao wa karibu kwenye mbio za ubingwa wa EPL, Arsenal wao wametupwa mdomoni mwa PSV Eindhoven ya Uholanzi na Aston Villa wakipewa Club Brugge.
Mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Real Madrid - ambao waliwaondoa Manchester City katika awamu ya mchujo – watavaana na wapinzani wao wa jiji moja, Atletico Madrid.
Miamba mingine ya Ulaya, Bayern Munich watakutana na wapinzani wao wa kwenye Ligi Kuu ya Ujerumani, Bundesliga, Bayer Leverkusen katika mechi ya Wajerumani watupu.
Itakuwa mara ya kwanza kwa Liverpool kucheza na PSG katika michuano ya Ulaya tangu msimu wa 2018-19, wakati 'Wekundu' hao walipotawazwa kuwa Mabingwa wa Ulaya kwa mara ya sita kwenye historia yao.
Washindi wa mechi hiyo watacheza na kati ya Aston Villa au Club Brugge katika robo fainali, huku Arsenal wakikutana na washindi mara 15 Real Madrid au Atletico Madrid katika hatua ya nane bora - iwapo wataifunga PSV.
Mechi za hatua ya 16-bora ya mikondo miwili zitachezwa kuanzia Machi 4 hadi 5 na mechi za marudiano zitapigwa Machi 11 hadi 12, mwaka huu.
Droo kamili ya 16-bora
Club Brugge v Aston Villa - Mechi ya kwanza Machi 4, marudiano Machi 12.
Real Madrid v Atletico Madrid - Mechi ya kwanza Machi 4, marudiano Machi 12.
Borussia Dortmund v Lille - Mechi ya kwanza Machi 4, marudiano Machi 12.
PSV Eindhoven v Arsenal - Mechi ya kwanza Machi 4, marudiano Machi 12.
Feyenoord v Inter Milan - Mechi ya kwanza Machi 5, marudiano Machi 11.
Paris St-Germain v Liverpool - Mechi ya kwanza Machi 5, marudiani Machi 11.
Bayern Munich v Bayer Leverkusen - Mechi ya kwanza Machi, marudiano Machi 11
Benfica v Barcelona - Mechi ya kwanza Machi 5, marudiano Machi 11.
Liverpool, Villa wanaweza kukutana
Vinara wa Ligi Kuu England, Liverpool dhidi ya Mabingwa Watetezi wa Ufaransa PSG ni mchezo utakaokuwa na hisia za kuvutia.
PSG walionekana kuondoka kwenye kinyang'anyiro hicho kabla ya kuchelewa kwa kiwango kizuri kuwafanya kumaliza katika nafasi ya 15 katika awamu ya ligi.
Walipoteza mbele ya Arsenal kabla ya kuwalaza Manchester City na ikakutana na Wafaransa wenzao kwenye hatua ya mchujo Brest ambapo walishinda kwa jumla ya mabao 10-0.
PSG wana Ousmane Dembele, mmoja wa wafungaji mabao bora barani Ulaya hivi sasa, akiwa na mabao sita kwenye mashindano ya msimu huu.
Liverpool haijashinda mechi yoyote kati ya tano zilizopita ya ugenini dhidi ya Klabu za Ufaransa, tangu ushindi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Marseille mwaka 2008.
"Katika hatua hii ya mashindano, ubora wa mpinzani utakuwa wa kiwango cha juu sana na kwa PSG tumetoa timu na klabu yenye asili halisi ya Ulaya," anasema kocha wa Liverpool, Arne Slot.
"Walifuzu kwa hatua ya 16-bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mtindo wa ushindi mkubwa dhidi ya Brest na walikuwa na matokeo mazuri katika awamu ya ligi, wakiwashinda Stuttgart, Manchester City, Girona na Salzburg."
Iwapo Liverpool watakifunga kikosi cha kocha, Luis Enrique, basi watacheza na wapinzani wao wa Ligi Kuu England, Aston Villa, mnamo Aprili mradi tu wawashushe mabingwa watetezi wa Ubelgiji Club Brugge, ambao walimaliza katika nafasi ya 24 katika awamu ya ligi kabla ya kuishinda Atalanta katika mchujo wa awamu ya mtoano.
Hata hivyo, Club Brugge, waliwashinda Villa katika awamu ya ligi, moja kati ya vichapo viwili pekee ilivyopata timu hiyo ya kocha Unai Emery.
"Nina furaha sana kwa sababu tutafurahia wakati huu na mashabiki wetu," alisema Emery baada ya droo hiyo.
Wapinzani wa Arsenal, PSV Eindhoven, ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Uholanzi, ambao waliwashinda vijana wa Liverpool mabao 3-2 mnamo Januari na kushika nafasi ya 14 katika awamu ya ligi.
'Washikabunduki' wameifunga PSV mara tatu katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, na ushindi wao wa hivi karibuni zaidi wa kushinda 4-0 nyumbani msimu uliopita.
"Tunajua tunachokabiliana nacho," anasema Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta.
"Tumecheza dhidi yao, ni timu nzuri sana. Unapokuwa katika hatua hii kila timu ni nzuri sana."
Robo fainali 2 (PSV Eindhoven/Arsenal au Real Madrid/Atletico Madrid) dhidi ya washindi wa robo fainali 1 (Paris Saint-Germain/Liverpool au Club Brugge/Aston Villa)
Washindi wa robo fainali 3 (Benfica/Barcelona au Borussia Dortmund/LOSC Lille) dhidi ya washindi wa robo fainali 4 (Bayern Munich/Bayer Leverkusen au Feyenoord/Inter Milan).
Fainali itapigwa hapa
Fainali ya Ligi ya Mabingwa msimu huu wa 2024/2025, itapigwa kwenye Uwanja wa Allianz Arena mjini Munich nchini Ujerumani Mei 31, 2025.
Hii itakuwa fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kuchezwa chini ya mfumo mpya.
Huu ni msimu wa 70 wa mashindano haya, na msimu wa 33 tangu ilipobadilishwa jina kutoka Kombe la Klabu Bingwa Ulaya hadi Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Bingwa atacheza na mshindi wa Europa League kuwania taji la UEFA Super Cup 2025.
Hii itakuwa fainali ya pili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kuandaliwa kwenye Uwanja wa Allianz Arena, ya kwanza ilifanyika mwaka wa 2012.
Kwa ujumla, itakuwa fainali ya tano ya Ulaya kufanyika mjini Munich, huku fainali za 1979, 1993, na 1997 zikifanyika Uwanja wa Olympiastadion.
Katika fainali nne za awali zilizochezwa Munich washindi walikuwa (Nottingham Forest mwaka 1979, Marseille mwaka 1993, Borussia Dortmund mwaka 1997 na Chelsea mwaka 2012).
Fainali hii pia itakuwa ya tisa kufanyika nchini Ujerumani, ikiwa pia ilifanyika Stuttgart mwaka wa 1959 na 1988, Gelsenkirchen mwaka 2004 na Berlin mwaka 2015, na kufikia rekodi ya fainali tisa za Kombe la Ulaya zilizofanyika Italia na Hispania.
Uwanja wa Allianz Arena hapo awali ulikuwa mwenyeji wa mechi kwenye Kombe la Dunia la FIFA la 2006, na ulichaguliwa kama uwanja wa mwenyeji wa Euro 2020 na Euro 2024.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED