Taasisi za umma nunueni bidhaa kwenye kampuni za ndani: RC Mtanda

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 01:49 PM Feb 25 2025
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda akikata utepe kuzindua yadi hiyo.
Picha: Vitus Audax
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda akikata utepe kuzindua yadi hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, amezitaka sekta za umma na binafsi kuhakikisha zinatoa kipaumbele kwa kampuni za uzalishaji za ndani katika manunuzi ya vifaa vya ujenzi, ili kusaidia kuongeza ajira kwa Watanzania na kuchochea mzunguko wa uchumi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa yadi mpya ya uuzaji wa mabati ya kampuni ya ALAF katika eneo la Buzuruga, jijini Mwanza, Mtanda alisisitiza kuwa kuunga mkono wazalishaji wa ndani ni njia bora ya kukuza fursa za kiuchumi kwa wananchi wa rika mbalimbali.

"Tunapaswa kujenga utamaduni wa kununua bidhaa za ndani kutoka kwa wazalishaji wetu, kama kampuni ya ALAF, ambayo ina ubia wa moja kwa moja na serikali. Kwa kufanya hivyo, tunachangia utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya taifa," alisema Mtanda.

Aliongeza kuwa, licha ya kampuni hiyo kusimamiwa na wawekezaji kutoka Sweden, serikali ina hisa kubwa kupitia kampuni tanzu ya Safari Group, hivyo manunuzi kutoka ALAF yanachangia mapato ya serikali na maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Biashara wa ALAF, Sateesh Yamsani, aliahidi kuwa kampuni hiyo itaendelea kuunga mkono shughuli za maendeleo nchini kwa kuzalisha bidhaa bora, zinazodumu kwa muda mrefu na kumpa unafuu mtumiaji.

"Tuna uwezo wa kusambaza bidhaa za kutosha na kwa wakati kupitia matawi yetu mbalimbali nchini, bila kupunguza ubora," alisema Yamsani.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Safari Group, Anders Lindgren, alisema yadi hiyo mpya ya ALAF inakuwa moja kati ya mamia ya yadi zilizosambaa nchini kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi.

Aliongeza kuwa Tanzania inaendelea kukua kwa kasi, hasa katika sekta ya maendeleo, hali inayowavutia wawekezaji kutokana na mazingira mazuri ya uwekezaji na amani inayotawala nchini.