Shirika la Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF) jana Februari 24, 2025, limekabidhi vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni 109 kwa vikundi 12 vinavyojishughulisha na kilimo cha mwani katika vijiji vya Jimbo na Kanga.
Hatua hii inalenga kuongeza thamani ya zao la mwani, kuboresha uchumi wa wakulima, na kuhimiza uhifadhi wa mazingira kwa kurejesha mikoko, ambayo ni muhimu kwa mfumo wa ikolojia wa pwani.
Akikabidhi vifaa hivyo, Msimamizi wa Miradi ya Huduma Ndogo za Kifedha kutoka WWF, James Golola, ameiomba Halmashauri kupitia Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kuhakikisha usimamizi mzuri wa vikundi hivyo ili vifaa vilivyotolewa vitumike kwa malengo yaliyokusudiwa.
WWF inatekeleza mradi wa "NORAD MANGROVE", ambao unashirikisha jamii katika uhifadhi wa mazingira kwa njia endelevu. Kupitia mradi huu, jamii inapata fursa ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi huku ikikuza kipato cha mtu mmoja mmoja, hivyo kuinua ustawi wa wakulima wa mwani na jamii kwa ujumla.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED