Vurugu Kituo cha Mwendokasi Kimara Temboni, abiria ashambuliwa

By Imani Nathaniel , Nipashe
Published at 12:48 PM Feb 25 2025
Afisa wa Mwendokasi ambaye jina lake halikupatikana akimpiga teke abiria baada ya kutokea vurugu hizo leo.
Picha:Imani Nathaniel
Afisa wa Mwendokasi ambaye jina lake halikupatikana akimpiga teke abiria baada ya kutokea vurugu hizo leo.

Vurugu zimeibuka katika Kituo cha Mabasi ya Mwendokasi cha Kimara Temboni, baada ya kile kinachodaiwa kuwa ni ukiukwaji wa utaratibu wa kupanga mstari kwa abiria.

Tukio hilo limetokea leo Februari 25,2025 majira ya saa 2:40 asubuhi ambapo lilianza pale abiria walipovunja mstari rasmi wa kupanda kwenye magari hayo na kuanzisha mstari mwingine baada ya basi walilokuwa wakilikimbilia kujaa. Hali hiyo ilisababisha mvutano kati ya abiria na maafisa wa usafiri wa mabasi hayo, huku baadhi ya abiria wakidai kuwa hawawezi kupangiwa namna ya kupanda kwenye basi.

Katika purukushani hizo, abiria mmoja alijeruhiwa baada ya kupigwa na maafisa wa Mwendokasi wakishirikiana na dereva wa basi hilo lililokuwa kituoni hapo lenye namba za usajili T 544 DWR.

1

Mwandishi wa Nipashe Digital, alikuwa mmoja wa abiria katika kituo hicho na kushuhudia tukio hilo. Mmoja wa abiria alijaribu kutuliza hali kwa kuwaomba maafisa hao pamoja na dereva wampeleke abiria huyo waliokuwa wakimshamulia kituo cha polisi badala ya kumpiga. Dereva wa basi hilo alishuka kwenye gari na kumkaba abiria uyo aliyetoa shauri, jambo lililozua taharuki zaidi.

Tukio hilo limezua mjadala kuhusu changamoto za huduma ya Mwendokasi, ambapo abiria wengi wamekuwa wakilalamikia ucheleweshaji wa magari na msongamano mkubwa wa abiria hasa wakati wa asubuhi.

Aidha, kumekuwa na malalamiko kuhusu tabia ya baadhi ya maafisa wa taasisi za umma kujichukulia sheria mkononi na kutumia nguvu kupita kiasi, jambo ambalo linakinzana na misingi ya utoaji wa huduma kwa wananchi.