KAMATI ya Siasa na Diplomasia ya Kati ya Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-ISPDC), imekutana jijini Dar es Salaam, kujadili masuala ya usalama wa kikanda, ikiwa ni pamoja na mgogoro unaoendelea katika mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Shelukindo, aliwaeleza waandishi wa habari jana, baada ya kufungua mkutano huo wa ISPDC na kueleza madhumuni na umuhimu wa kikao hicho.
Alisisitiza kuwa mkutano huo ni hatua muhimu katika kushughulikia changamoto za usalama wa kikanda, hasa hali ya mashariki mwa DRC na ni sehemu ya juhudi pana za Wakuu wa Nchi za SADC katika kukuza amani na uthabiti wa kanda.
Shelukindo alifafanua kuwa mijadala hiyo itahitimishwa kwa mapendekezo ambayo yatawasilishwa kwa Baraza la Mawaziri kwa ajili ya uamuzi zaidi.
Pia alitaja kuwa Wakuu wa Nchi wa SADC walishakutana awali kujadili masuala ya amani, ulinzi, na usalama wa kikanda, huku mgogoro wa DRC ukipewa kipaumbele maalum.
Mkutano huo umejumuisha Makatibu Wakuu kutoka nchi zote kumi na sita za SADC kujadili masuala ya diplomasia na usalama wa kikanda.
“Kwa muda wa siku mbili, Makatibu Wakuu wanajadili masuala mbalimbali ya amani na diplomasia. Mwishoni mwa mkutano, watakamilisha mapendekezo ambayo yatapelekwa kwa Baraza la Mawaziri kwa hatua zaidi,” alisema Shelukindo.
Alisisitiza kuwa mazungumzo hayo yanalenga kutoa mapendekezo yanayoweza kutekelezwa ili kuboresha hali ya amani na usalama wa kikanda, hasa kwa kuzingatia mgogoro unaoendelea DRC.
Kamati hiyo inatarajiwa kukamilisha majadiliano yake kesho, huku matokeo ya mkutano yakitarajiwa kutolewa kwa umma.
Shelukindo pia alibainisha kuwa tayari chaguzi zimefanyika katika baadhi ya nchi za SADC, huku Tanzania ikitarajiwa kufanya uchaguzi wake baadaye mwaka huu.
“Chaguzi kama hizi zinaweza kuwa sehemu muhimu ya mazingirya kisiasa ya kanda na zinaweza kuwa na athari kikanda,” aliongeza.
Shelukindo alisisitiza kuwa mkutano wa Kamati ya Ushirikiano wa Amani, Ulinzi, na Usalama ya SADC ni hatua muhimu katika kushughulikia changamoto za usalama wa kikanda, hasa katika mashariki mwa DRC.
Aliongeza kuwa matokeo ya mkutano huo yatakuwa na mchango mkubwa katika kuunda sera za baadaye za amani na usalama ndani ya SADC.
Mnamo Agosti 17 mwaka jana, Rais Samia Suluhu Hassan aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Troika ya Amani, Ulinzi, na Usalama ya SADC.
Uteuzi wake, uliofanyika wakati wa Mkutano wa 44 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliofanyika Harare, Zimbabwe, unampa jukumu la kusimamia na kuratibu masuala ya kisiasa, ulinzi, na usalama wa kikanda ndani ya mfumo wa SADC.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED