Umoja wa Walimu Wasio na Ajira Tanzania (NETO) umethibitisha kuwa Mwenyekiti wao, Joseph Kaheza, ambaye alikuwa anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Geita, amepewa dhamana.
Katika taarifa kwa umma iliyotolewa leo Februari 25, 2025, na Katibu Mkuu wa NETO, Daniel Mkinga, imeelezwa kuwa Kaheza alikuwa akishikiliwa kwa ajili ya uchunguzi uliokuwa ukiendelea.
"Tunawashukuru Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), vyombo vya habari, na wote waliowezesha ndugu yetu kupata uhuru wake. Sasa yuko salama na anaendelea na majukumu yake," amesema Mkinga.
Aidha, amesisitiza kuwa NETO si chama cha siasa na hakihamasishi migomo, bali ni jukwaa linalotetea ajira kwa walimu wasio na ajira.
"Tunaendelea kuiomba Serikali itoe ajira kwa walimu wote waliohitimu kati ya mwaka 2015 hadi 2023, kwani uhaba wa walimu bado ni changamoto, huku wahitimu wakizidi kuongezeka," ameongeza.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED