Wasiojulikana wafukua kaburi, waondoka na mwili

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:18 PM Feb 25 2025
 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Shadrack Masija.
Picha: Mtandao
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Shadrack Masija.

JESHI la Polisi mkoani Rukwa linawasaka watu wasiojulikana kwa tuhuma za kufukua kaburi na kisha kuondoka na mwili wa marehemu Julius Ladislaus (24), aliyefariki dunia Novemba mwaka jana.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Shadrack Masija alisema jana kuwa Julius alifariki dunia Novemba mwaka jana wilayani Chunya, mkoani Mbeya na mwili wake kusafirishwa hadi mkoani Rukwa ulikozikwa katika kijiji cha Lunyala, wilayani Nkasi.

Alisema kuwa Februari 14 mwaka huu, watu wasiojulikana walikwenda na kufukua kaburi na kuchukua mwili wa marehemu na kuliacha sanduku na kaburi likiwa wazi, huku mwili wa marehemu wakiondoka nao.

Kamanda Masija aliwaomba wananchi walio na taarifa juu ya watu waliofanya kitendo hicho, kutoa taarifa katika kituo cha polisi ili wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Alisema polisi wanaendelea na uchunguzi wa kina juu ya tukio hilo ambalo linahusishwa na imani za kishirikina na kuwasihi wananchi kuachana na imani hizo ambazo katika kipindi hiki zimepitwa na wakati.

Katika tukio lingine, Kamanda Masija alisema polisi wanamtafuta mtu ambaye hadi sasa hajajulikana anayetuhumiwa kuhusika na kifo cha mwanamke aliyekutwa amefariki dunia katika nyumba ya kulala wageni mjini Namanyere.

Alisema kuwa Februari 19 mwaka huu, mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 19, akiwa na kijana wa kiume ambaye hajajulikana, waliingia katika nyumba ya kulala wageni na kuchukua chumba.

Kamanda Masija alisema kuwa usiku huo, mwanamume huyo alikimbia baada ya kudaiwa kumuua kwa kumnyonga mwanamke aliyekuwa naye chumbani na mpaka sasa haifahamiki aliko.

Hivyo, ametoa wito kwa wananchi kutoa taarifa za haraka kwenye mamlaka za serikali kwa ajili ya hatua mbalimbali za kisheria kuhusiana na mauaji hayo.