Katambi asimikwa kuwa ‘Chifu Gudiliwa’

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 02:37 PM Feb 25 2025
Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na watu wenye Ulemavu, akisimikwa na wazee kuwa Mtawala na kupewa jina la Chifu Gudililwa
Picha: Mtandao
Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na watu wenye Ulemavu, akisimikwa na wazee kuwa Mtawala na kupewa jina la Chifu Gudililwa

BARAZA la Ushauri la Wazee Kata ya Oldshinyanga, wamemsimika Mbunge Patrobas Katambi ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu, kuwa Mtawala na kupewa jina la Chifu Gudiliwa yaani ‘Ndeleji’.

Jina hilo likiwa na maana ya mfuatiliaji na mtatuzi wa changamoto za wananchi katika kuwaletea maendeleo.

Usimikwaji huo umefanyika jana, ukiongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Kata ya Oldshinyanga, Stephano Tanu.

Tanu akizungumza kabla ya Katambi kusimikwa na Mzee Idd Pyalimi, amesema wazee wameridhishwa na kazi kubwa ambayo anaifanya mbunge huyo na kwamba, Shinyanga haijawahi kuwa na Mbunge ambaye anaguswa na maisha ya wananchi na kutatua kero zao.

"Katambi ametuheshimisha sana, hivyo sisi wazee tunamsimika na kumpatia taji la utawala, ili aendelee kuwa kiongozi wetu tena na kutuletea maendeleo zaidi, sababu shinyanga ya sasa siyo ile ya zamani imepiga hatua kubwa kimaendeleo," amesema Tanu.

Katambi asimikwa kuwa ‘Chifu Gudiliwa’
Mzee Iddi Pyalimi, mara baada ya kumaliza kumsimika Mbunge Katambi, walimpatia jina la Chifu Gudiliwa ‘Ndeleji’, ili aendelee kufuatilia masuala ya maendeleo na kutatua kero mbalimbali za wananch.

Katambi, amewashukuru wazee hao kwa kumsimika pamoja na kumpatia jina la Chifu Gudililwa ‘Ndeleji’ na kwamba jina hilo amelipokea, huku akiahidi kuendelea kuchapa kazi zaidi na kuwaletea maendeleo.

"Wazee wangu mmeniheshimisha sana na kunipatia nguvu ya kufanya kazi usiku na mchana,ili niwatumikie wananchi wa Shinyanga na kuwaletea maendeleo zaidi," amesema Katambi.

Amesema ndani ya miaka minne ya ubunge wake ametekeleza ahadi ambazo aliahidi kwa wananchi katika sekta mbalimbali ikiwamo ya elimu, afya, maji, umeme na miundombinu ya barabara.