Mchome wa CHADEMA kuzungumza na wanahabari leo

By Enock Charles , Nipashe
Published at 11:42 AM Feb 25 2025
Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Jimbo la Mwanga, mkoani Kilimanjaro, Lembrus Mchome.
Picha: Mtandao
Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Jimbo la Mwanga, mkoani Kilimanjaro, Lembrus Mchome.

Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Jimbo la Mwanga, mkoani Kilimanjaro, Lembrus Mchome, anatarajia kufunguka kinachoendelea ndani ya chama hicho ikiwemo kile anachodai ni mpango wa kufukuzwa katika chama.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Mchome mwenyewe anatarajia kuzungumza na waandishi wa habari leo kueleza masuala kadhaa ikiwa ni pamoja na kile alichodai ni mpango wa yeye na wenzake kufukuzwa ndani ya chama hicho.

"Mkutano huo utatoa picha ya kinachoendelea katika chama, ukiwepo mpango wa kufukuzwa na viongozi wa juu wa chama hicho kufuatia ukiukwaji mkubwa wa katiba ya chama hicho uliofanywa katika Uchaguzi Mkuu sanjari na uteuzi wa viongozi watano wa Kamati Kuu wa CHADEMA." imesema sehemu ya taarifa yake.

"Mchome anatoka hadharani kuzungumzia jinsi viongozi hao wa CHADEMA, chini ya Mwenyekiti wa Taifa Tundu Lissu na Makamu wake John Heche, walivyoamua kusigina Katiba yao, huku wakikataa kukosolewa na wanachama wanaotofautiana kimtazamo."

"Lissu na viongozi wenzake wa CHADEMA wamejinasibu kama moja ya watu wanaopenda kuikosoa serikali, licha ya wao kushindwa kuvumilia wanapokosolewa katika uendeshaji wa chama chao."

Tayari Mchome ameshawasilisha barua katika ofisi ya Msajili wa Vya Siasa nchini kuhoji uhalali wa viongozi walioteuliwa na Mwenyekiti wa Chama hicho, Tundu Lissu akiwemo Katibu Mkuu, John Mnyika.