Hivi ndivyo mfumuko wa bei unavyokuwa

By Salome Kitomari , Nipashe
Published at 04:06 PM Feb 25 2025
Ofisa wa Sera na Uchumi katika Kurugenzi ya Tafiti na Sera za Uchumi, Dominic Mwita.
Picha: Salome Kitomari
Ofisa wa Sera na Uchumi katika Kurugenzi ya Tafiti na Sera za Uchumi, Dominic Mwita.

Ofisa wa Sera na Uchumi katika Kurugenzi ya Tafiti na Sera za Uchumi, Dominic Mwita, amesema mfumuko wa bei hupima ongezeko la bei kwa bidhaa 383 zinazotumiwa na kaya za Kitanzania, huku bidhaa moja kama mafuta ikihusiana moja kwa moja na mabadiliko ya bei za bidhaa nyingine.

Akizungumza wakati wa uwasilishaji wa mada kuhusu mfumo wa utekelezaji wa sera ya fedha kwa njia ya riba, ulioanza Januari 2024, Mwita amefafanua kuwa kupungua kwa mfumuko wa bei hakumaanishi kushuka kwa bei ya bidhaa, bali inaashiria kuwa kasi ya ongezeko la bei imepungua.

"Kwa mfano, ikiwa mfumuko wa bei wa Januari  ni asilimia 3.1, maana yake ni kwamba kwa wastani, bei za bidhaa zinazotumiwa zaidi na Watanzania zimeongezeka kwa asilimia hiyo. Kama ulikuwa asilimia 4 na ukashuka hadi 3, haimaanishi kuwa bei za bidhaa zimepungua, bali zimeongezeka kwa kasi ndogo," amesema Mwita.

Amesema mfumuko wa bei unahesabiwa kwa kulinganisha mabadiliko ya bei kati ya vipindi viwili tofauti, mara nyingi ndani ya mwezi au mwaka, kwa kukusanya bei za bidhaa mbalimbali kila mwezi. Alieleza kuwa tathmini hiyo hufanywa kwa kuzingatia mahitaji ya msingi ya familia, huku mfumuko wa bei ukihusiana kwa kiasi kikubwa na uzalishaji wa bidhaa na hali ya uchumi kwa ujumla.

Katika kufafanua zaidi, Mwita amesema kuna bidhaa zinazopimwa kwa karibu ili kubaini mwenendo wa bei, kama vile:

Mchele.

  • Chakula: Mchele, unga wa mahindi, nyama ya ng’ombe
  • Matumizi ya mkaa.
  • Nishati: Umeme, kuni, mkaa

Nyumba.

  • Huduma nyingine: Kodi za nyumba, usafiri, ada za shule, ukarabati wa nyumba, mavazi na afya

Ameongeza kuwa mchango wa bidhaa kwenye mfumuko wa bei hutegemea kiwango cha matumizi ya kaya katika bidhaa husika. Hata hivyo, kuna bidhaa ambazo zina sehemu ndogo katika matumizi ya kaya lakini zinaongezeka kwa kasi kubwa, hivyo athari yake kwa mfumuko wa bei huwa ndogo.

Kuhusu usimamizi wa mfumuko wa bei, Mwita amebainisha kuwa kuna sababu zinazoweza kuathiri bei ambazo zipo nje ya uwezo wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kama vile ukame au wadudu waharibifu wa mazao. Katika hali kama hizo, serikali hutumia mbinu za kisera, kama vile ruzuku kwenye bidhaa muhimu kama mafuta, ili kudhibiti mfumuko wa bei.

"Mfumuko wa bei hutokea pale ambapo kuna pesa nyingi kwenye mzunguko kuliko mahitaji halisi ya uchumi. Serikali haifanyi maamuzi ya kuchapisha fedha kiholela kwa sababu fedha nyingi kwenye mzunguko husababisha kupanda kwa bei za bidhaa na kupungua kwa thamani ya pesa," amesema Mwita.

Kwa mujibu wa Mwita, kiwango cha mfumuko wa bei Tanzania ni chini ya asilimia 5, huku vigezo vya kikanda vikionesha kuwa nchi za SADC zinapaswa kuwa na mfumuko wa bei wa kati ya asilimia 3 hadi 7, wakati nchi za EAC zinatakiwa kuwa na kiwango cha asilimia 8.

Mwita amesema ukuaji wa uchumi wa Tanzania unategemea usimamizi mzuri wa sera mbalimbali, ikiwa ni pamoja na sera ya fedha, sera ya kibajeti, na sera za sekta kama kilimo, biashara na viwanda.