Wachezaji 6 wanaoweza kutwaa Ballon d'Or 2024

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:31 PM Jul 22 2024
Lamine Yamal (kushoto) na Rodri wakiwa na tuzo zao, mchezaji bora kinda wa michuano ya Euro na mchezaji bora wa mashindano hayo.
PICHA: MTANDAO
Lamine Yamal (kushoto) na Rodri wakiwa na tuzo zao, mchezaji bora kinda wa michuano ya Euro na mchezaji bora wa mashindano hayo.

WACHEZAJI watakaoteuliwa kuwania Tuzo ya Mchezaji Bora wa Dunia watatangazwa Septemba 4, mwaka huu. Msimu wa 2023-24 na mashindano makubwa ya msimu huu wa majira ya joto ni mambo yatakayozingatiwa.

Vinicius Junior wa Real Madrid na Jude Bellingham, wameshindwa kutwaa mataji ya kimataifa wakiwa na Brazil kwenye Copa America na England kwenye Euro 2024, bila shaka hilo limefungua mlango kwa wachezaji wengine pia.

BBC Sport inawaangalia wachezaji sita wenye uwezo wa kushinda tuzo hiyo Oktoba 28, mwaka huu, mjini Paris nchini Ufaransa. 

Vinicius Junior (Real Madrid, Brazil)

Amecheza michezo 49, amefunga mabao 26, amepiga pasi za mwisho 11, makombe ni La Liga, Ligi ya Mabingwa Ulaya na Super Cup.

Winga wa Real Madrid, Vinicius mwenye umri wa miaka 24, amekuwa akitajwa kuwania tuzo ya Ballon d'Or kwa muda mrefu baada ya kuisaidia timu yake kushinda La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Alimaliza msimu akiwa mfungaji bora wa Real Madrid kwa mabao 24 na pasi za mabao 11.

Kama Brazil ingeshinda Copa America pengine angekuwa na uhakika wa kutwaa tuzo hiyo - lakini walitolewa katika robo fainali kwa mikwaju ya penalti na Uruguay, mchezo ambao Vinicius aliukosa kwa sababu ya kufungiwa baada ya kupewa kadi mbili za njano katika hatua ya makundi.

Mbrazil wa mwisho kushinda Ballon d'Or alikuwa Kaka mwaka 2007, na Neymar pekee ndiye aliyemaliza katika nafasi tatu za juu tangu wakati huo. 

Rodri (Manchester City, Hispania)

Amecheza michezo 63, amefunga mabao 12. Ametoa pasi za mwisho za magoli 14. Makombe aliyobeba ni Ligi Kuu England, Uefa Super Cup, Klabu Bingwa Dunia na Euro 2024.

Kiungo wa kati Rodri mwenye umri wa miaka 28, ana mataji manne ya Ligi Kuu England, Uefa Super na Klabu Bingwa Dunia akiwa na Manchester City, na kisha Euro 2024 akiwa na Hispania.

Alitoka nje ya uwanja akiwa ameumia wakati wa mapumziko kwenye fainali ya Euro dhidi ya England, lakini tayari alikuwa amefanya vya kutosha kutangazwa mchezaji bora wa michuano hiyo.

Hakuna mchezaji wa Manchester City ambaye amewahi kushinda Ballon d'Or akiwa na klabu hiyo. 

Jude Bellingham (Real Madrid, England)

Michezo aliyocheza ni 54. Mabao kafunga 27. Katoa pasi za mwisho 16. Makombe aliyoshinda ni La Liga, Ligi ya mabingwa Ulaya na Super Cup.

Kiungo wa kati wa England Bellingham mwenye umri wa miaka 21, alikuwa na msimu mzuri akiwa na Real Madrid kutokana na uhamisho wa msimu uliopita kutoka Borussia Dortmund.

Alimaliza akiwa na mabao 23 - ikiwa ni pamoja na ushindi wa dakika za lala salama katika mechi zote mbili za La Liga akiwa na Real Madrid- na pasi za mwisho 13 kwa klabu yake waliposhinda Ligi ya Hispania na ile ya Mabingwa Ulaya.

Wakati wake wa kuvutia zaidi kwenye Euro 2024, ulikuwa mpira wa juu wa dakika za majeruhi, bao alilofunga dhidi ya Slovakia hatua ya 16-bora.

Kama angeiwezesha England kushinda katika fainali dhidi ya Hispania, huenda angekuwa mshindi wa kwanza wa Ballon d'Or kutoka England tangu Michael Owen mwaka 2001. 

Dani Carvajal (Real Madrid, Hispania)

Michezo aliyocheza ni 54. Mabao aliyofunga ni saba. Pasi za mwisho alizotoa ni nane. Makombe ni LaLiga, Ligi ya Mabingwa Ulaya, Super Cup na Euro 2024.

Beki wa kulia Carvajal mwenye umri wa miaka 32, ni mmoja wa wachezaji 12 waliocheza na kushinda fainali za Ligi ya Mabingwa Ulaya na Ubingwa wa Euro katika msimu mmoja.

Aliifungia Real Madrid bao la kwanza katika ushindi wa fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Borussia Dortmund - na pia aliifungia Hispania dhidi ya Crotia katika mechi ya makundi ya Euro 2024.

Kama atashinda atakuwa beki wa pembeni wa kwanza kushinda Ballon d'Or.

 Lamine Yamal (Barcelona, ​​​​Hispania)

Michezo aliyocheza ni 64. Mabao aliyofunga ni 10. Pasi za mwisho alizotoa ni 14. Kombe ni Euro 2024.

Winga wa Barcelona, Yamal tayari alikuwa na msimu mzuri kwa kijana mwenye umri wa miaka 16, wakati akicheza mechi 50 za klabu, akafunga mabao saba na pasi za mwisho saba.

Kwenye Euro 2024, aliufanya msimu wake kuwa wa kuvutia zaidi kwa mchezaji wa umri wake.

Pasi za mwisho nne nchini Ujerumani zilikuwa muhimu kwenye rekodi ya michuano hiyo ya Ulaya - na alifunga bao zuri katika ushindi wa nusu fainali dhidi ya Ufaransa ambalo liliingia kwenye historia.

Mchezaji huyo mwenye umri mdogo zaidi, mfungaji mabao na mshindi katika michuano ya Ulaya - alitimiza umri wa miaka 17, siku moja kabla ya fainali - alitajwa kuwa mchezaji bora chipukizi katika mashindano hayo.

Gwiji wa Brazil, Ronaldo de Lima akiwa na umri wa miaka 21, mwaka 1997, ndiye mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kushinda Ballon d'Or. 

Lionel Messi (Inter Miami, Argentina)

Michezo 39 amecheza. Mabao 28 amefunga. Amepiga pasi za mwisho 17. Kombe ni Copa America.

Messi mwenye umri wa miaka 37, ndiye mchezaji aliyefanikiwa zaidi katika historia ya Ballon d'Or, akishinda mara nane - ikiwa ni pamoja na mwaka jana, baada ya kuiongoza Argentina kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia.

Alifunga bao moja pekee katika ushindi wa Argentina msimu huu wa majira ya joto, dhidi ya Canada katika nusu fainali ya Copa America, alitoka nje baada ya jeraha kwenye fainali. Kwa ujumla alicheza chini ya kiwango chake.

Messi hajashinda taji lolote akiwa na Inter Miami hadi sasa.