Tume Uratibu Dira, sikieni jambo la wanawake hawa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:26 PM Jul 17 2024
Dk. Amina Msengwa kutoka Tume ya Mipango na Uratibu wa Dira 2050, akizungumza wakati wa kupokea maoni ya wanawake.
PICHA ZOTE: MWANDISHI WETU
Dk. Amina Msengwa kutoka Tume ya Mipango na Uratibu wa Dira 2050, akizungumza wakati wa kupokea maoni ya wanawake.

“TUNAFURAHIA dira ya maendeleo ya taifa 2050, jinsi ilivyo shirikishi na jumuishi inayokusudia kumfikia kila mmoja, aeleze Tanzania anayoitamani. Ni jambo la kihistoria.”

Anasema Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), Salma Haji Sadat, akizungumza na Nipashe baada ya kongamano la kitaifa la wanawake kuchangia maoni ya Dira ya  Taifa 2050, mwishoni mwa wiki iliyopita.

Kongamano hilo linaloandaliwa na Mfuko wa Udhamini wa Wanawake (WFT), Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF) linawakutanisha wanawake  na wajumbe wa Tume ya Mipango na Uratibu wa Dira ya Taifa, Dar es Salaam.

Salma, anasema ni dira jumuishi yenye mawazo ya wengi na mambo bora ambayo yakiwekwa kwenye vipaumbele vya taifa huenda yakaleta Tanzania bora zaidi hata kabla ya kufikia 2050.

Hata hivyo, ana angalizo kwa Tume ya Kuratibu Maoni ya Dira kuwa Tanzania lazima ikomeshe rushwa na kufanya mikakati ya kupata fedha za ndani kuendesha miradi ya maendeleo na ujenzi wa nchi.

Anatamani dira inayoondoa rushwa ili mamilioni ya pesa za miradi yanayoibwa kila mwaka yasichotwe yatumiwe kuondolewa wananchi umaskini.

Aidha, dira inayolinda na yenye uchungu na rasilimali za nchi ili zisiporwe na kumalizika badala yake zilete maendeleo kwa kila mmoja.

“Rasilimali ziwape watu maji safi, umeme, elimu bora, barabara za kutosha, chakula na fedha wasilie hali ngumu na umaskini”.

Salma anagusia elimu, kuwa dira iifikishe Tanzania kwenye elimu bora si kukariri maandiko badala yake wajifunze zaidi mambo ya kukuza na kuendeleza kada (professions) kama ualimu, uhandisi, kilimo na uandishi wa habari, akisema ndivyo wanavyofanya China na mataifa ya Korea, Malaysia na Indonesia.

VIJANA KAA LA MOTO

Salma Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar, anagusia utitiri wa vijana usiona na tumaini, akisema ni kundi kubwa zaidi na linaloendelea kuongezeka kila siku kwa idadi, hivyo serikali ifanya kila mbinu kutatua kero zao maana wako nyuma zaidi.

Anashauri iwekwe mikakati yenye kuleta mabadiliko ya haraka ili kubadili maisha yao maana ni wengi wakiachwa bila ajira, elimu, mikopo, misaada wala kuendelezwa wanaweza kuwa changamoto kubwa kwenye taifa.

“Tutumie teknolojia na maarifa kuwawezesha kubadili maisha yao, wawe na kazi wapate fedha, waingizwe kwenye kilimo, ufundi na teknolojia ili kuwanyanyua kwani ni kundi kubwa, liangaliwe kwa jicho pevu.” Anaeleza. 

Pili Kuliwa ni Mratatibu wa Shirika la Tumaini Jipya la Wanawake Kilwa (TUJIWAKI), anasifu dira shirikishi inayowapa wengi nafasi ya kutoa maoni yao kuanzia mikaoni, mijini, vijijini, akisema haijawahi kufanyika tangu uhuru.

Anataka dira iangalie ulinzi wa watoto Bara na Visiwani kwa sababu wanatelekeza, kuwaacha watunzwe na ndugu au wazee wasio na kipato na wengine kuishi kwenye mazingira magumu na ya kihalifu, ngono na dawa za kulevya.

Anaeleza kuwa kuna kizazi cha watoto wengi wenye umri wa chini ya miaka 15 ambao hawasomi, wasio na malezi, waliofanyiwa ukatili ambao wamesambaa karibu kila mahali.

“Tusipofanya hivyo ikifikapo 2050 tutakuwa na vijana wengi wasiojua kusoma kabisa, wasiojitambua, wahalifu ambao ni mzigo usiobebeka kwa taifa.”

Mkurugenzi wa Chama cha Solidarity for Women and Children with Disabilities (SOWACHIDI), Adeline Mluge, anasifu ushirikishwa wa wananchi kuandaa dira akitaka ifanyike tathmini ya upungufu na  kasoro za kutekeleza dira 2025 inayomalizika.

Mjumbe wa Kamati ya Ufundi ya Mtandao wa Wanawake, Katiba na Uchaguzi, Maria Chale, anasema wanatamani kuwa na Tanzania yenye ulinzi wa makundi ya wanyonge hasa wenye ulemavu na wanaoishi na ualbino.

Wanatamani ije dira inayoweka utaratibu wa kuwa na sheria ya kuwaadhibu kwa kunyongwa hadharani wanaoua wenye ualbino kwa sababu hayo ni mauaji ya kukusudia na wanaopatikana na hatia hawanyongwi mbali na kuhukumiwa na kubakia magerezani.

Maria anashauri sheria iangalie masuala ya ushahidi kwenye kesi za mauaji ya albino, badala ya kuendelea kueleza kuwa kesi ya mauaji ni lazima jamhuri itoe ushihidi usioacha shaka dhidi ya mshukiwa wa mauaji.

Aidha, anazungumzia uendeshaji kesi za mauaji ya albino kuchelewa kupindukia akisema kuwe na utaratibu wa kuziharakisha zimalizike mahakamani na haki itendeke.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Vivian Women, Vivian Ugulumu, anasema shirika lao linatamani kuona dira 2050 inayoifikisha Tanzania kwenye elimu bora na yenye wataalamu na wahandisi wa kutosha wazawa.

“Watoto wanasoma tena kwa kugharamiwa na serikali msingi na sekondari lakini wanapata elimu bora au bora elimu? Tufanye mabadiliko tuwe na elimu bora kama mataifa mengine Afrika Mashariki ikifika 2050 tuwe bora kielimu.” Anasema.

Akizungumzia wahandisi anasema miaka ijayo ni lazima kuwa na wataalamu wazawa wanaojenga barabara za juu, za mwendokasi na kufanya kandarasi mbalimbali badala ya kutegemea wageni kama ilivyo sasa.

Katibu wa Chama cha Wasioona (TLB), Wilaya ya Kisarawe, Asha Magendo, anasema wanatamani kuona Tanzania inayoongozwa na dira inayoheshimu wanaoishi na ulemavu.

Anasema miaka 60 ya uhuru hakujawa na juhudi za kutosha kuwathamini na kuwaheshimu, mfano kwenye hospitali hakuna dirisha wala dawati kwa ajili yao.

“Usafiri wa umma hakuna anayewajali, ajira, wakiwa benki na vyoo vya umma au kwenye hoteli na migahawa hakuna anayetujali,” anasema akitaka dira inayokuja iwe na Tanzania inayoheshimu wanaoishi na ulemavu.

Nice John ni Mjumbe wa Chama cha Wanaoishi na Ualbino (TAS) Wilaya ya Ilala, anasema dira inayokuja isisahau huduma muhimu kwa wanaoishi na ualbino kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

“Dira inapoangalia makundi maalumu ihakikishe wenye ualbino wanapewa kofia, mafuta, miwani na tiba ya ngozi kutokana na jua kali na joto kutokana na mabadiliko ya tabianchi.”

Vifaa hivyo vipatikana kwa kila mmoja anayehitaji kupitia Bohari ya Dawa (MSD) na sensa yao ifanyike iwatambue na kuwahudumia kwenye hospitali zote.

Nice anapendekeza kuwapo na madaktari bingwa wa ngozi na macho kwenye vituo vya afya mijini na vijijini ili kusaidia wanaoishi na ualbino.

“Tunatamani kuwa na dira inayozungumzia kuelimisha jamii kuhusu uelewa wa masuala ya ulemavu. Watu wafahamu sababu za ulemavu wowote na kuwaunga mkono kwa kukataa unyanyapaa,” anaongeza Nice.