Simulizi yenye utata mauaji kinamama Kenya, maswali ya umma yametawala, kuliko majibu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:59 AM Jul 18 2024
Mtuhumiwa wa mauaji, akiwa chini ya ulinzi.
PICHA ZOTE: MTANDAO.
Mtuhumiwa wa mauaji, akiwa chini ya ulinzi.

KUKAMATWA kwa mshukiwa wa mauaji ya Kenya kumezua hisia kali kote nchini, baadhi ya watu wakihoji undani wake.

Polisi wanasema, Collins Jumaisi Khalusha (33), alikiri kuwaua wanawake 42, lakini siku ya Jumanne wakili wake akaiambia mahakama kuwa aliteswa ili kukiri mauaji.

Ni tukio la kutatanisha, baada ya ugunduzi wa mabaki ya miili tisa iliyokatwa vipande, kuwekwa kwenye mifuko, kufungwa kwa kamba na kutupwa kwenye machimbo ambayo hutumika kama jaa la taka karibu na Kituo cha Polisi mtaani Mukuru, jijini Nairobi.

Kuna malalamiko, baadhi ya watu hawaelewi vipi polisi hawakuweza kugundua kuwapo miili iliyotupwa wastani mita 100 kutoka waliko, Mtaa wa Mabanda wa Mukuru Kwa Njenga.

Kaimu Mkuu wa Polisi Douglas Kanja, Jumapili akatangaza kwamba, maofisa wa Kituo cha Polisi Kware, karibu na eneo la tukio wamehamishwa.

Mamlaka inayosimamia utendakazi wao, ilisema inafanya uchunguzi kubaini ikiwa polisi walihusika kwa namna yoyote na mauaji hayo.

Familia ya Josephine Owino, aliyetoweka inasema alimjia ndotoni’ mmoja wao na kuwaelekeza kwenye jalala hilo.

Diana Keya, ndugu wa marehemu huyo, akasema kwamba familia iliwalipa vijana kupekua taka katika jalala hilo, hata kuibua mkasa wa kuwapo miili tisa iliyoharibika vibaya, ikipatikana Ijumaa wiki iliyopita. Ilikuwa imefungwa kwenye mifuko ya plastiki kwa kutumia kamba.

Taarifa za awali za polisi zilisema "kisa hicho kiligunduliwa na wakazi.”  Alipoulizwa baadaye Mkurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Mohamed Amin akajibu "Sisi sio waotaji na hatuamini ndoto."

Polisi wanasema, miili iliyopatikana ilikuwa katika hatua tofauti za kuoza, hata ikiashiria waathiriwa walikuwa wameuawa kwa nyakati tofauti.

Pia, polisi wanasema mshukiwa anayeitwa Khalusha, amekiri kuwaua wanawake hao kwa kipindi cha miaka miwili, ushahidi ambalo sasa unatiliwa shaka.

Jambo lisilo wazi ni iwapo mabaki yalitupwa wakati huo au hivi karibuni. Hussein Khalid, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Haki Afrika, analaumu maelezo ya polisi kuhusu matukio hayo yalikuwa na "maswali mengi".

Mtazamo huo wa maswali, pia unahusu polisi walivyofanikiwa kumkamata mshukiwa chini ya siku tatu, baada ya kupatikana miili hiyo, ingawa kabla hawakuwahi kutilia shaka tukio lolote lisilo la kawaida katika muda wa miaka miwili.

Jumatatu wiki hii, polisi walisema Khalusha alikamatwa kwenye baa akitazama mechi ya fainali ya michuano ya Euro 2024.

Walionyesha kwenye vyombo vya habari baadhi ya vitu vinavyosemekana kupatikana kwa nyumba ya mshukiwa,- pia karibu na mahali aliko kulipatikana simu 10, vitambulisho na nguo za ndani za kike.

Polisi wanasema, walifuatilia aliko Khalusha baada ya kupata simu ya mmoja wa waathiriwa wake.

 WAATHIRIWA JE?

Ni mwili mmoja tu uliotambuliwa hadi sasa, Roseline Ongogo mwenye umri wa miaka 24 na ndugu yake Emmanuel Ongogo, anayeeleza kwamba alitoweka Juni 28 mwaka huu, alipotoka nyumbani kwenda kutafuta kibarua.

Anasema familia yake ilienda chumba cha kuhifadhi maiti cha City, Nairobi ilipopata habari kuhusu miili iliyopatikana Mukuru.

Walimtambua, kwa sababu alikuwa na nguo aliyokuwa amevalia na msongo wa nywele aliyokuwa nayo wakati alipotoweka.

Polisi pia wanadai kuwa mke wa Khalusha, alikuwa mwathiriwa wake wa kwanza na wanasema kitambulisho chake kilipatikana, kuwa miongoni mwa vitu vingine vinavyodaiwa kuwa vya waathiriwa.

Familia ya Owino, inasema kuwa iliota kuhusu aliko na wakawa wanasubiri uchunguzi wa kipolisi.

MTAZAMO USALAMA

Kupatikana miili hiyo kumeibua kumbukumbu ya mauaji ya kinyama ya mwezi Januari mwaka huu, ya msichana Rita Waeni aliyekuwa na umri wa miaka 20.

Mwili wake uliokuwa umekatwa vipande ulipatikana katika nyumba ya kupanga kwa makazi ya muda mfupi jijini Nairobi. Kesi hiyo bado haijatatuliwa.

Kifo hicho kilisababisha maandamano nchini kote kupinga kuongezeka kwa visa vya mauaji ya wanawake na unyanyasaji dhidi yao.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International, lilisema zaidi ya mikasa 500 vya mauaji ya wanawake yalirekodiwa nchini Kenya kati ya 2016 na 2023.

Ikadai miili yote iliyopatikana jalalani, saswa na mkasa wa sasa unachukua msukumo ni ya wanawake. Kuna viongozi wachache wa makundi ya wanawake wakusanyika katika chumba cha kuhifadhi maiti, waliiomba serikali kuharakisha uchunguzi na kukomesha ukatili wa aina hiyo.

Alipoulizwa polisi walikuwa wakifanya nini kushughulikia kesi za mauaji ya wanawake na unyanyasaji dhidi ya wanawake, Msemaji wake Resila Onyango, akafafanua hawezi kushughulikia suala hilo, kazi ya polisi ni "kulinda maisha na mali ya kila mtu."

·                      Kwa mujibu wa BBC.