Rais azindua lami kilomita 107 hadi Bandari Kassanga, neema kwa mizigo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:50 AM Jul 19 2024
Dk. Samia Suluhu Hassan, alipozindua Barabara ya Sumbawanga - Matai hadi Bandari Kasanga.
Picha: IKULU
Dk. Samia Suluhu Hassan, alipozindua Barabara ya Sumbawanga - Matai hadi Bandari Kasanga.

JUZI Jumatano, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, akahitimisha ziara yake iliyochukua siku saba mikoa ya Rukwa na Katavi na jana akakanyaga ardhi ya mkoani Songwe, kuanzia mji mdogo wa mpakani, Tunduma.

Huko Rukwa alikotoka, amewaachia zawadi kwa kuzindua barabara ya lami umbali kilomita 107. 14, kutoka Manispaa ya Sumbawanga – Matai hadi Bandari ya Kasanga, ambayo nayo imekarabatiwa kwa kina, kazi iliyokamilika miaka michache tu iliyopita.

Hiyo bandari nayo katika nafasi yake ni ‘bidhaa mpya’ mahali hapo ikihudumia mataifa jiorani kama Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na Zambia, ikinufaisha uchumi wa nchi kwa ujumla.

Uzinduzi wa Rais, ukaambatana na rai yake kwa wananchi kuitunza barabara hiyo kwa manufaa ya kızazi kilichoko na kijacho, akinena:

“Kabla ya barabara hii kujengwa, nimeambiwa usafiri kuelekea bandarini ilikuwa inachukua hadi siku nzima, lakini baada ya barabara hii kujengwa, ni masaa mawili tu umefika Bandarini Kasanga.”

Akaendelea: “Niwaombe Wananchi na Kalambo (wilaya) na wasafirishaji wote kutunza miundombinu ya barabara, kwa kuacha kulima au kufukua fukua pembezoni mwa barabara kwani kufanya hivyo, kunasababisha kuharibika kwa haraka barabara zetu.”

Akawafafanulia, kwamba ni barabara inayowarahisishia usafiri na usafirishaji wa mazao na mifugo kutoka mkoani Rukwa kwenda maeneo mingine ya nchi jJirani, kama Rwanda, DRC na Burundi.
 
 “Tunaenda kukuza uchumi wa biashara kati yetu na nchi jirani na wananchi wa Kalambo (wilaya yenye Bandari Kassanga) ni wakulima wazuri sana. 

“Sasa mtapata urahisi wa kusafirisha na sio Kalambo peke yake, mazao yatakayolimwa ndani ya mkoa wa Rukwa na Katavi yatapata urahisi wa kusafirishwa,” anasema Dk. Samia.

Rais akawataka wakazi kutofanya shughuli za kijamii kama kilimo na kuchimba pembezoni mwa barabara, nao wakimhakikishia watalinda miundombinu hiyo inayojengwa na serikali.

“Ujenzi wa barabara ni gharama sana. Ukijenga kilomita moja ya barabara, ni sawa na kujenga vituo vitatu vya afya, pamoja na kuweka vifaa tiba ndani yake. Kwa hiyo, niwaombe sana tutunze barabara zetu,” anasema Dk. Samia.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mohamed Besta anaeleza miradi hiyo iliyozinduliwa imekamilika Aprili mwaka huu, akiainisha imegahrimu shilingi bilioni 150.5 inayojumuisha ujenzi, ushauri na fidia kwa wenyeji, kazi iliyotekezwa na mkandarasi kampuni ya Kichina.

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa naye akatoa ufafanuzi kuwa, barabara ya Sumbawanga - Matai hadi Bandari Kasanga, inaunganishwa na nyingine  inayokarabatiwa ya Matai - Tatanda - Kasesya yenye kilomita 50.

Hiyo inatarajiwa ikikamilika, itarahisisha usafiri na usafirishaji kutoka mpakani Kasesya Zambia, akisema Rais ameshatoa fedha za kuanza kazi hiyo.

KWANINI KASSANGA?

Bandari ya Kasanga iliyopo wilayani Kalambo mkoa wa Rukwa, ujenzi wake nao ulikamilika mwishoni mwa mwezi Aprili, 2020. Hiyo ni miongoni mwa bandari zinazomilikiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), katika Ziwa Tanganyika 

Hiyo ni bandari ya kimkakati iliyoko kwenye mpaka wa Zambia na DRC na ya pili kwa ukubwa kwenye Ziwa Tanganyika, nyuma ya Bandari Kigoma.

Kimsingi, Bandari ya Kasanga ni mji mdogo ulioko wilayani Kalambo, Kusini-Magharibi wa Tanzania, mwambaoni mwa Ziwa Tanganyika, ikiwa na historia ndefu tangu utawala wa ukoloni wa Ujerumani, ikibatizwa jina la Bismarckburg.

Katika Sensa ya Watu na Makazi nchini mwaka juzi, wakazi wa mji mdogo Kasanga, walihesabiwa kuwa 13,281 na pana umbali wa kilomita 67 kutoka makao makuu ya wilaya ya Kalambo.

Hivi sasa, mji wa Kasanga umejengwa na Soko la Kimataifa la Samaki Kasanga na kuna mpango wa kufunga vyumba baridi vya kuhifadhi samaki, Kasanga na eneo la Muzi, kunufaisha  vijiji jirani vitanufaika, huku kuiunganishwa na nchi jirani DRC, hata kufungua maradufu  njia hiyo, ikitajwa hadi sasa malori mengi ya mizigo kwenda nchi hiyo jirani, kutoka bandarini Dar es Salaam. 

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, anataja miradi mingine ya barabara iliyokamilika mkoani Rukwa ni ya Tunduma (Songwe) hadi Sumbawanga, kilomita 220 na Sumbwanga - Kanazi – Kizi – Kibaoni (km 151.6), zote ni za kiwango cha lami.

 Mtendaji Mkuu wa (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, anasema ujenzi wa barabara hizo ni mwendelezo wa malengo ya serikali kujenga barabara kiwango cha lami, hadi sasa  kilomita 802.55 zimekamilika, kati ya hitaji kilomita 1,286, sawa na asilimia 62.40.

Aidha, Bashungwa anaeleza mkakati wa serikali katika mwaka uliopo fedha 2024/25 mkoani Rukwa  ni kuanza usanifu wa barabara ya Laela - Mwimbi - Kizombwe (Km. 93).