NGONO MTANDAO: Matangazo, picha zashamiri kwa kasi

By Waandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:49 AM Jun 25 2024

Maumbile ni kivutio kinachoweza kutumiwa na mabinti kuvuta wateja mitandaoni.
PICHA: MTANDAO
Maumbile ni kivutio kinachoweza kutumiwa na mabinti kuvuta wateja mitandaoni.

MAENDELEO ya sayansi na teknolojia yanachangia kukuza uchumi na kuibua mambo mengi ya kisasa yakiwamo yanayopotosha, kama kuchochea ngono mitandaoni.

Leo maisha yamebadilika huduma kuanzia tiba, elimu, biashara, mitindo ya mavazi, magari na uwekezaji wa aina zote hufanikishwa na mtandao.

Zama hizi za kujifunza au kupata elimu na ujuzi mbalimbali lakini pia kuuza na kununua mitandao, zinawaibua wale wanaofanyabiashara za  ngono pia, wakisaka na kupeana miadi na wale wanaotaka kushiriki matendo hayo, iwe nje au ndani ya nchi.

Mambo hayo ya kufanya biashara rasmi za ngono kwenye nyumba au madanguro, yalishamiri zaidi Ulaya na Amerika na kwa Tanzania si jambo linalokubalika tena ni jinai kuwa na madanguro na kuuza ngono hadharani.

Wenye biashara hizo nao wako mitandaoni wakitangaza popote duniani kusaka wateja au kuwaalika kutembelea madanguro yao.  

Kuiga mbinu hizo na kutumia mitandao kumechangia kuibua wadau kutoka Tanzania nao wakisaka wateja, wanunuzi, wauzaji na hata  maajenti,  wanaofanyakazi hiyo mitandaoni . Inadaiwa kuwa kwa baadhi ya mabinti wanaojiuza na maajenti wanaosaka wateja wao wasichana ni chanzo cha kipato.

Miji mikubwa kama Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya, Zanzibar ni maeneo ambayo unaweza kupata biashara ya aina hiyo ikiendelea watu wakitumia simu za kujinadi na kujitangaza pamoja na kuweka gharama zao na maeneo ya wanakopatikana.

Mitaani bado kuna wanaouza miili yao mfano jijini Dar es Salaam Ubungo Riverside, Buguruni  Kimboka, Sinza, Afrika Sana, Posta na Kariakoo ni sehemu zinazoongoza kwa watu wanaofanyabiashara hizo nyakati za usiku.

Lakini biashara ya ngono mtandaoni inavyoelekea inakua siku baada ya siku kutokana na maendeleo ya teknolojia ambayo huenda ikiwaondoa kina dada hao mitaani wakabaki kufikia wateja kwa njia ya Facebook, WhatsApp, Instagram, TikTok, Telegram, Snapchat  na X au tweeter  na Youtube. 

Utafiti unaofanywa na Nipashe unabainisha kuwa  wengi wananunua na kuuza  ngono mtandaoni tena bila kificho.

 Imebainika kuwa wanawake kuanzia miaka 20 hadi miaka 35 ndiyo wanafanya biashara ya aina hiyo ambayo wanadai ina faida kwao, wakati wa mahojiano na gazeti hili.

“Wafanyabiashara wengi wa ngono wanajitangaza kupitia mitandao, mfano wanaweza kukutana na watu mashuhuri duniani na kupata fedha zaidi . Kwa mfano kwa kutumia...” anasema mmoja wa wahusika.

Wanataja baadhi ya mitandao wanayoitumia na kwamba siyo ile inayoruhusiwa nchini kwa mfano VPN.

“Biashara hiyo inafanywa kwa njia ya siri sana ambayo watu hutumia simu janja kuingia katika tovuti wanazofanya mambo hayo kwa kutumia mtandao binafsi kuepusha kukamatwa,” anaongeza.

Wapo wanaopeleka picha na vivutia ngono mbalimbali ili kuvuta wateja sehemu mbalimbali ili wazichague na kuwasiliana, anaeleza zaidi.

Mitandao ya kijamii imekuwa na jukumu  katika ukuaji wakazi ya ngono mtandaoni, kwa mujibu wa maelezo yake.

Wahusika wanafafanua kuwa kutokana na mmomonyoko wa maadili mitandao hiyo huruhusu wafanyabiashara ya ngono kufikia wateja popote walipo.

Akizungumzia tatizo hilo la biashara hiyo mitandaoni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Mtandao wa Jeshi la Polisi, Joshua Ishekazoba, anasema  kuwa serikali inapinga vikali biashara hiyo.

“Kwanza kuweka picha za utupu kwenye mitandao ya kijamii ni kinyume cha sheria. Hivyo kwa wale wanaojihusisha na biashara ya ngono mtandaoni wajue kuwa wanakwenda kinyume na sheria za nchi.”

Kwa mujibu wa sheria ya usalama wa mtandao ya mwaka 2017 adhabu yake ni  kifungo cha miaka mitano jela au faini ya Shilingi milioni 20 au vyote kwa pamoja.

Anaitaka jamii kutoa taarifa za matendo hayo wanapowajua wahusika ili washtakiwe.

Mwanasaikolojia Rajab Ali, mhitimu wa elimu ya saikolojia, kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anazungumzia mienendo hiyo akisema mara nyingi wanaofanya biashara hiyo  wanafanyiwa ukatili wakikutana na hao wateja wa mitandaoni.

 “Wanaofanya biashara hiyo mara nyingi hupata misukosuko na  msongo wa mawazo japo hawawezi kukuonyesha ila ni wathirika wakubwa sana wa afya ya akili  na  wakati mwingine baadhi hufanya maamuzi mabaya na magumu,” anasema Ali.

Baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam, wanasema katika jamii yenye maadili watu wamekuwa  na mtazamo kuwa biashara hiyo haifai  na kwamba inawadhalilisha wanawake na vijana wanaojipandisha kwenye majuu ya biashara ya ngono.

Mwanafunzi wa sekondari  Mariam Omary, anasema kuwa wanawake wanaofanyabiashara hiyo hawajithamini na kuwahimiza kusaka  njia mbadala ya kupata riziki.

ANaonya kuwa kuishi  biashara hiyo kunaweza kusabaisha magonjwa ya aina mbalimbali na athari za kiafya na kiakili.

“Inawapasa wabadilishe mtazamo ili kuacha hiyo biashara maana jamii yetu haiwachukulii vizuri na hawakubaliki. Ni kuvunja maadili ya taifa na heshima yetu,” anaesema Mariam. 

Vivyo hivyo Zakaria Katoto, mwanajamii anayetumia mitandao kwa shughuli mbalimbali, anasema kuwa serikali inapaswa kuweka mkazo na kukataza mambo ili kujenga jamii iliyo bora kwa vizazi vyote.

Licha ya wanaohusika  kukubaliana na kuwepo mambo hayo  wajue kuwa kuna hatari na changamoto zinazotokana na kazi hiyo. Kwa Tanzania waojihusisha na biashara za ngono wengi wanakabiliwa na ubaguzi, unyanyapaa, chuki na hata kuchukiwa na baadhi ya watu mitaani.

Takwimu  za  Tume ya Kudhibiti UKIMWI  (TACAIDS), zinaonyesha kuwa vijana wengi wenye umri wa miaka 16 hadi 24 wameambukizwa  VVU na UKIMWI, kwa hiyo ni vyema kujilinda na kujihami ikiwamo kuacha ngono za mitandaoni.

IMEANDALIWA NA NEEMA KASSIM, PAULO PETER, FLORA FRANCIS, EDNA MBWILO & TWAIBA SWALEHE -SJMC