Mtaalamu muonja chai pekee EAC, elimu aliyopata darasani Uingereza mwaka mzima

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 07:00 AM Jul 19 2024
Richard Mwakangale (kushoto), akizungumza jambo katika Banda la Bodi ya Chai Tanzania (TB) kwenye Maonyeshoya 48 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DITF).
PICHA: CHRISTINA MWAKANGALE
Richard Mwakangale (kushoto), akizungumza jambo katika Banda la Bodi ya Chai Tanzania (TB) kwenye Maonyeshoya 48 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DITF).

Mzee Richard Mwakangale, ni miongoni mwa waonja chai (tea taster) wachache kuwapo nchini. Kwake kuonja chai iliyopikwa kwa takribani vikombe 1,000 ni jambo la kawaida.

Kwenye sekta ya chai amekuwamo kwa takribani miaka 30 akijipatia ujuzi London nchini Uingereza na aliporejea nchini, akawa tegemeo kati ya waonja chai wachache nchini. 

Mzee Richard (74), sasa ni mstaafu, ingawa bado hayuko mbali na taaluma yake. Amebaki akiishi nayo, kudadisi unywaji chai na vigezo vyake, huku ikibaki kiburudisho kikubwa nyumbani kwake na kwa wageni wanaomtembelea.  

Amekutana na Nipashe kwenye Maonyesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DITF), yaliyohitimishwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, Julai 13 mwaka huu. 

Katika Banda la Bodi ya Chai Tanzania (TBT), kwenye maonyesho hayo, alifanya mazungumzo ya kina kuhusu zao la chai na mnyororo wake iliko shambani hadi mezani, ikidumu kuwa mlo na kiburudisho kikubwa duniani. 

Kazi aliyoifanya kwa takribani miongo mitatu, inasadifu maisha yake, akiwa nyumbani kwake chai anayokunywa inapoletwa mezani, hubaini mara moja ubora wake, majani na daraja lake.  

Asiporidhika nayo, huchukua hatua ya kuleta majani mapya dukani yakiwa yenye ladha aipendayo, vigezo ubora. 

Mbali na maelezo yake, Bodi  ya Chai nchini ina maelezo ya wazi na rasmi kuhusu zao hilo hususan kiafya, kwamba kisayansi mtu anayekunywa chai kabla ya kuungwa sukari, faida zake ni takribani tisa mojawapo ni kuimarisha afya ya akili.  

Kwa Mzee Mwakangale, yafuatayo ndio mazungumzo yake na Nipashe, maswali na majibu, walipokuwa katika Viwanja vya Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara – Sabasaba, Dar es Salaam. Fuatilia: 

SWALIi: Mara nyingi zao la chai halifahamiki kiundani, ila umaarufu wake upo mezani. Je, chai ni nini? 

JIBU: Zao la chai lina mnyororo mrefu tangu shambani linapolimwa hadi kuwa chai inayonywewa. kwa ujumla, chai ni zao lenye thamani na kilimo chake huchagua mazingira. 

Zao la chai kisayansi linaitwa ‘camellia sinesensis’. Hili ndio jina la chai. Na mti wa chai unadumu sana. Ukishapanda unafanya ‘prooning’ ili mtu aweze kuchuma majani yake vizuri.  

Zao la chai linaweza kudumu hata miaka 100 (karne moja). Nakumbuka kuna mashamba Kimbila, Tukuyu (Mbeya), ambayo tangu mimi nasoma shule ya msingi na mpaka leo bado yapo. 

Shina la mti wa chai linaweza kuwa kubwa kama mguu, lakini linapofanyiwa ‘pruning’ (kupunguza majani) huku juu haliendelei kuwa kubwa. Ila kama halifanyiwi prooning, linaweza kuwa kubwa kama mti. 

Zamani zao la chai lilipandwa kwa mbegu, lakini siku hizi wanapanda kwa kile kinachoitwa ‘propagative vegetation’ yaani unachukua tawi la chai unaliotesha, halafu linakuwa mti wa chai. 

SWALI: Kwanini majani ya chai yanawekwa katika madaraja pale linapouzwa sokoni? 

JIBU: Ubora wa chai unaanzia shambani. Inategemeana na ‘spishi’ (aina) au familia ya aina gani ya ule mti. Kuna chai ambazo zinaitwa ‘chrono’ ukiipanda chai inakuwa nzuri sana. 

Sababu nyingine ya ubora wa chai, ni udongo tunaita ‘Soil PH’. Udongo una maana sana katika ubora wa chai. Jambo lingine ni mvua, chai hustawi kwenye mvua, pia hutegemea na mwinuko (attitude). Chai ambayo imepandwa katika mwinuko mrefu, inakuwa na ladha nzuri sana na ‘flavoured’. 

Chai inapokuwa shambani inachumwa kwa mkono na huchumwa majani mawili na sindano au unachuma ‘soft bunji’, majani fulani malaini. Lakini siku hizi, wanachuma majani kwa kutumia vifaa maalum vya kuchumia. Hii inapoteza ubora wa chai, kwa sababu majani yanayochumwa na kifaa hicho mengi si yale yenye viwango au vitatu yaani, hesabu ya majani mawili na sindano. Ukichuma chai kwa mkono na kifaa, ubora ni tofauti. 

Pia kwenye zao hili shambani, wakulima wamegawanywa kwa makundi mawili; wadogo na wakubwa. Mkulima mdogo shamba lake ni ekari tano hadi 10. Mfano sisi nyumbani kwetu kwa Mzee Mwakangale (John Mwakangale- Tukuyu), shamba letu ni la mkulima mdogo.

 SWALI: Baada ya chai kuvunwa kutoka shambani, hatua gani hufuata? 

JIBU: Chai ikivunwa inapimwa uzito ni kiasi gani ili atakapolipwa ijulikane ni malipo ya chai kiasi gani. Chai ikishavunwa shambani au ikichumwa inatakiwa ipelekwe haraka kiwandani. 

Kwanini iende haraka kiwandani. Chai ina rangi ya kijani yaani lile jani lake kitaalamu ni ‘green pigment’. Ile green pigment inatokana na ‘chromophyll’ ndio inafanya jani liwe la kijani. Ukiichukua jani na ukalivunja ndani, kuna ‘enzyme’ ambayo inakula ule ukijani na kubadili kuwa rangi ya kahawia. 

Kwa hiyo mara tu jani linapochumwa tu likimbizwe kiwandani kabla halijaanza kubadilika kuwa kahawia. Inapocheleweshwa majani, yanaweza kutupwa kwa sababu ubora wa chai umepotea. Mara nyingi tu majani yatatupwa, kwa sababu hii. 

Jani likiwa kiwandani linafanyiwa ‘withering’ kunakuwa na kitu mfano wa kitanda au kichanja, majani yanatandazwa yenye kilo 1,600 hadi 2,000. Hii ni hatua ya kukausha jani, kuondoa maji kwa sababu unaweza kupima jani kumbe uzito ule ni kutokana na maji. 

SWALI: Je, kuna tofauti kati ya chai ya kijani (green tea) na chai nyeusi (black tea)? 

JIBU: Tofauti ya chai nyeusi na kijani. inatokana na hatua za uandaaji kiwandani. Chai nyeusi ni baada ya kufanyiwa ‘withering’, lakini chai ya kijani ikitoka shambani wanaifanyia ‘steaming’ kuua enzyme na kuzifanya jani kubaki na ukijani wake. 

Chai ya kijani ni maarufu zaidi kwa Wachina, wanatumia zaidi na wengine. 

Hatua ya kunyausha jani lililotoka shambani katika kitanda au kichanja hicho, huchukua takribani saa 16 kwa kutumia upepo kama feni, ingawa ukaushaji wa asili wa jani la chai ndio hatua nzuri zaidi ikilinganishwa na hii inayotumiwa ya ‘withering’. Lakini kufanikisha ukaushaji wa asili ni ngumu kwa sababu kunakuwa na kilo nyingi za majani. 

Baada ya kukausha inafuaa hatua ya kukamua juisi kutoka jani, kitaalamu inaitwa ‘rotorvane’ kisha inapelekwa katika mashine ya CTC kirefu chake ni ‘Crushing Tearing & Curling’ kama vile wakinamama wanavyo ‘curl’ nywele zao. 

Baada ya hapo inapelekwa ‘fermenting’ hii ni hatua muhimu na isipofanyika vizuri chai haiwezi kuwa nzuri.  

Ukiweka muda mrefu tatizo na muda mfupi tatizo, lazima uzingatie muda maalum. Itafuata hatua ya ‘dryer’ kuikausha chai ikitoka hapo inakuwa nyeusi. 

Baada ya hatua hizo inakuja hatua za madaraja inaitwa ‘sorting’ na madaraja hayo ni la kwanza ambalo ni BP1 (browser pekoe one); PF1 (pekoe fanning one); PD (pekoe dust); Dust One; Fanning na BMF (broken mixed fanning). 

Madaraja haya ndio huamua soko na mahitaji yako. Zamani kulikuwa na masanduku. Unaifunga katika sanduku, lakini sasa hivi kuna ‘bags’ au tea bags na begi moja huchukua kilo 50 hadi 60 inategemeana. Mfano ‘PD’ huingia nyingi zaidi katika begi. 

SWALI: Njia gani hutumika katika kuiuza chai ambayo pengine hufika hadi soko la nje? 

JIBU: Kuna njia nyingi za kuuza chai, moja ni kwenye mnada wa kimataifa, upo Mombasa (Kenya) na hivi sasa nasikia Tanzania umeanzishwa mnada Kurasini. 

Na mnada wa Mombasa ni mkubwa sana zinakuja chai dunia nzima na nimehudhuria sana kwenye mnada huo. Chai zinasafirishwa hadi katika ghala na mtu wa ghala anatoa sampo kwa madalali ambao nao wanaonja (tasting) wanaithaminisha chai na kisha wanapanga bei kulingana na kile alichokionja. 

Kwa ‘tea tasting’ ndio maana yake hii na inauzwa kwa dola huko Mombasa. Baada ya kupanga bei wanaisajii chai mfano ‘Katumba tea’ ina daraja hili PF1 nauza shilingi 100 kwa kilo’...mnada utaendelea kwa ushindani kila mmoja anataja bei ya juu yake, mwingine shilingi 140 au 90. Muuzaji akiona bei mbaya anaiondoa (withdraw) mnadani, ili akauze pembeni asipate hasara. 

Hatua nyingine ya kuiuza ni kuuza moja kwa moja, unaweza ukapeleka Ulaya, au kwa tea blenders, kama Chai Bora nao wanakwenda kui-brand (kuipatia kundi) na kuweka nembo zao. 

Chai huwa inachukua unyevu haraka sana, ni lazima uifunike, yaani ina ‘hygroscopic’. Mara nyingi, vifungashio vya chai huwa ndani vina aluminium ili maji yasiingie ndani. 

 Kama vile kahawa ukiiacha wazi utakuta inaganda. Chai isipotunzwa hivyo kwenye kifungashio ubora wake hupungua.

Ubora wa chai ni mnyororo kuanzia shambani. 

SWALI: Unapozungumzia muonja chai ‘tea taster’ ina maana gani kwa lugha rahisi? 

JIBUu: Katika kuonja chai zipo hatua nne na lengo ni kuangalia ubora, ila ubora huanzia shambani. Kunakuwa na vikombe maalum vya kuonjea chai labda ni vya TBT au blenders, ni vya udongo na vyeupe. 

Kuna kikombe, mfuniko kwa kila kikombe, kipimia majani (mizani maalum wa chai) na bakuli dogo. 

Unachukua hicho kipimo, unaweka katika kikombe, majani, unachukua maji yaliyochemshwa, unaweka maji katika kikombe. Uingereza tulikuwa tunaonja chai hadi vikombe 1,000 chai ya dunia nzima!  

Na hata nikionja vikombe 1,000 najua tofauti, kila chai daraja lake na ilikotokea ina alama yake nyuma labda, hii Tanzania, Rwanda. Baada ya dakika sita majani ya chai, maji katika kikombe utafunua. Maji utamwagia katika bakuli, makapi tutaweka kwenye mfuniko na chai nzuri hung’aa kama senti tano au kama kopa. Ukiweka juu tu kwenye bakuli lazima ing’ae. 

Halafu unaangalia jani lenyewe limetengenezwaje? Kwa macho utajua hii nyeusi, kahawia tuna teminoloji zetu kama za kidaktari.  

Mimi muonjaji ndio natoa maoni na kuipa thamani chai. Unarudi katika ule mchuzi wa chai, ukiangalia sana ni kama manjano hivi vitu ambavyo vinaleta ladha. Kama vile mchele wa Kyela, utakuta mchuzi wa chai mzito au mwepesi na rangi yake je?  

Tutaweka na maziwa kidogo, ili unye rangi kwa sababu wapo watumiaji wanaotumia maziwa na majani. Utajua hii ni nzuri. 

Baada ya hapo unaweka bei. Unakuta katika uonjaji upo pekee yako au mko wengi. Matokeo ya uonjaji ndio unaona daraja la chai na ubora wake kwa sababu kuna chai, ambayo ukiionja unajua kabisa hii ilipitia hatua ya kuungua. Kumbuka kila unapoonja unatema, unatema eneo maalum, kisha huonjwa nyingine hata 1,000. 

Mfano chai inayolimwa India milima ya Himalaya ndio bora zaidi, inaitwa ‘darjeeng’ ni ghali duniani ni nzito ukiweka katika kikombe inanukia kama vile ina moshi. Kuna chai inaitwa ‘Assam tea’, na kuna nyingine pia inalimwa Kusini mwa India ukiweka kwenye kikombe nyepesi ila bora. 

Ukienda Sri Lanka chai yake ukiweka katika kikombe inang’aa kama dhahabu, ina njano nyingi. Nimeonja zote hizo hii inatemea na ilivyolimwa kwenye milima hali ya hewa. 

Kwingine kwenye chai nzuri Rwanda inalimwa kwenye milima, chai Burundi nayo sawa, Kenya, Malawi pia nzuri na Tanzania tunajitahidi.  Utengenezaji, aina ya mmea, udongo, hali ya hewa, kulima kwenye miinuko, vinachangia ubora wa chai. 

Nilikuwa Uingereza nikiona na kujifunza chai aina mbalimbali katika mnada. Kilimo cha chai lazima kiwe jirani na kiwanda, kulinda ubora. Ndio maana magari ya kiwanda huzifuata chai shambani.  

SWALI: Kwanini chai ni muhimu kwa binadamu?  

JIBU: Chai ni muhimu na katika soko chai inawekwa kulingana na mahitaji ya watu. Tunakunywa chai kwa sababu ya ‘caffein’ ila ni ndogo ikilinganishwa na iliyomo kwenye kahawa. Wataalamu wanasema ‘caffein’ inasaidia katika mfumo wa fahamu, labda kichwa kinauma, ukinywa inasaidia.  

Pia, katika mfumo wa hewa au umechoka, inasaidia hata katika mfumo wa moyo.  

SWALI: Je, uonjaji chai ni fani inayosomewa darasani au unatumia uzoefu? 

JIBU: Kuonja chai ‘tea tasting’ nilikwenda Uingereza mwaka 1975 na masomo haya yalifadhiliwa na British Council. Serikali ya Uingereza ilinipeleka kusoma kwa mwaka mmoja. Nilikuwa nakaa na madalali wa chai London huko wakanifundisha namna ya kuonja chai. 

Baadae, nikaenda Brooke Bond ni kampuni kubwa na wataalamu wakubwa wa chai duniani. Kampuni tangu miaka ya 1800. 

Baada ya hapo nikarudi Tanzania, Watanzania waliopata nafasi ya kwenda huko ni wanne tu, nikiwamo mimi. Wengine wameshafariki. 

Awali mwaka 1972 niliajiriwa Mamlaka ya Chai nikiwa Manager Trainee katika kiwanda cha Majani ya Chai Lupembe, Njombe na baada ya hapo ndio nikaenda kujifunza ‘tea tasting’, ni taaluma ndogo katika mambo ya chai.

 Mwaka 1975 nilikwenda kusomea Tea Tasting and Marketing (uonjaji chaio na masoko yake).  

KILIMO CHA CHAI 

Zao la chai ni miongoni mwa mazao ya kimkakati nchini, likianzia mwaka 1902 kutoka kwa Mjerumani, kwa mujibu wa Bodi ya Chai Tanzania. 

Mwaka 1903, likaanzia kupandwa Nyanda za Juu Kusini kama vile Tukuyu wilayani Rungwe, Njombe, Ludewa, Kilolo na Mufindi. Kadhalika Tarime, Korogwe, Kushoto, Bukoba, Kilimanjaro na Muheza. 

Nchini kuna viwanda 24 vya usindikaji, kati ya hivyo vikubwa ni 22 na vilivyosalia vidogo. Umiliki wa ubia ni katika viwanda vinne. Viwanda hivyo vinaweza kusindika tani 69,455 za chai kavu kila mwaka. 

Uzalishaji chai kutoka kwa wakulima kwa sasa nao ni tani 37,000 kwa mwaka huku, asilimia 38 kati ya mahitaji hayo yalizalishwa na wakulima wadogo. 

Asilimia 85 ya chai zilisindikwa nchini na kuuzwa moja kwa moja kupitia soko la Mombasa, Kenya kazi inayofanywa na madalali. Asilimia 15 iliyosalia ni kwa matumizi ya ndani. 

TBT inafafanua kwamba, chai ni kinywaji cha pili kinachonywewa kwa wingi baada ya maji. Ina virutubisho na madini ya manganese, zinki, potassium, vitamini B na E, pia kemikali iitwayo ‘polyphenol’ inayozuia uwezekano wa kupata saratani na kiharusi. 

Pia, chao inaimarisha meno, mmeng’enyo wa chakula, huongeza umakini inapambana saratani ya matiti, ngozi, tumbo na ngozi, huku utafiti ukionyesha inakata kiu na vikombe sita hadi nane kwa siku, huongeza maji mwilini sawa na idadi hiyo ya vikombe.