MKAPA 1938-2020 Dira 2050 itimize maono ya mwasisi Mkapa kuwapa wanawake maisha bora aliyokusudia

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:12 AM Jul 24 2024
Wanawake wakifurahia mafanikio wakati wa kongamano la  kuchangia maoni ya uandishi dira mpya 2050. PICHA: MWANDISHI WETU
PICHA: MWANDISHI WETU
Wanawake wakifurahia mafanikio wakati wa kongamano la kuchangia maoni ya uandishi dira mpya 2050. PICHA: MWANDISHI WETU

RAIS Benjamin Mkapa ni moja ya viongozi waliokuwa na nia ya kuibadilisha Tanzania ili kufikia maendeleo endelevu na hata msamiati ‘endelevu’, ulioanza kusikika wakati wa uongozi wake.

Ndizo zama msisitizo wa matumizi ya sayansi na teknolojia, maisha bora, ushirikishwaji jamii na uchumi shindani ulipopata msukumo zaidi.

Taifa linapomkumbuka Rais wa Awamu ya Tatu, Hayati Mkapa, linaendelea kutoa maoni kuandaa dira ya maendeleo ya 2050, baada ya kutekeleza dira ya 2025, iliyotayarishwa wakati wa uongozi wake.

Ili kuandaa dira na uelekeo mwingine wa taifa, wadau mbalimbali wakiwamo wanawake ambao idadi yao ni kubwa zaidi, wanachambua dira inayoelekea ukingoni na kuona jinsi inavyotakiwa kufanyiwa maboresho ili ijayo iwe ya usawa wa kijinsia na ilete maisha bora kwa wote Mkapa aliyoyatamani.

Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, mwakani inafikia ukingoni na kikubwa ilikuwa na uelekeo wa kukuza biashara ya mauzo ya nje na kuongeza au kuimarisha ushindani wakati inamalizika.

Wanawake wanaotoa maoni kuhusu utekelezaji wa dira hiyo wanaangazia uhalisia wa maisha bora kwa kila Mtanzania na iwapo idara iliwanufaisha.

Wanaainisha kuwa katika kuandaa Tanzania bora na maisha mazuri, wmeachwa nyuma kiasi kwamba umaskini wa taifa umevikwa sura ya mwanamke maskini wa kijijini.

Wanaona kuwa wanawake wamezidi kuwa na maisha duni japo ndiyo washiriki wakuu wa uzalishaji mali na chakula na kulifanya taifa kujitosheleza kwa chakula asilimia 120.

Rose Marandu, ni Mkurugenzi wa Mfuko wa Udhamini wa Wanawake (TWF), unashirikiana na wadau wakiwamo Mtandao wa Jinsia Tanzania TGNP kufanikisha kongomano la kitaifa la kukusanya maoni ya wanawake kuelekea uandishi wa dira mpya 2050.

Rose anasema asilimia 51 ya wanawake wameachwa kwenye uzalishaji wa kisasa, wakibakia ndani ya sekta isiyo rasmi tena ni wachuuzi, wafanyabiashara ndogondogo zisizo na mitaji wala sifa ya kukua.

Akizungumza kwenye kongamano hilo hivi karibuni, anaeleza kuwa hawana mikopo, badala yake wanategemea ile ya vikoba na kaushadamu ambayo siyo fedha nyingi za kukuza wala kupanua biashara zao.

Aidha, kwa kuangalia dira hiyo inayomaliza muda wake anagusia suala la chakula kuwa licha ya taifa kujitosheleza kwa chakula, udumavu wa watoto wa chini ya miaka mitano ni mkubwa.

Anasema udumavu na utapiamlo ni tishio hata katika mikoa wazalishaji wakuu kama Njombe na Katavi kiwango kikizidi kile cha taifa.

“Licha ya kujitosheleza kwa chakula kwa asilimia 130 mwaka 2024/25 kwa mujibu wa Wizara ya KIlimo, asilimia 20 ya familia hazina uwezo wa kumudu chakula cha kutosha chenye virutubisho cha kuwawezesha kuwa timamu na kushiriki maendeleo ya nchi.”

Akizungumzia elimu ambayo pia ni takwa la dira hiyo ya 2025, anasifu juhudi za kuongeza usawa wa kijinsia katika kuandikisha na kudahili wanafunzi shuleni na vyuoni.

Idadi yao imeongezeka kuanzia shule za awali, msingi, sekondari na vyuo vikuu, anasema.

Kwa mfano, Rose anasema mwaka 2017 usajili wa watoto shule za msingi ulifikia asilimia 89.6 wasichana wakati wavulana walifikia asilimia 86.

Kadhalika, kiwango cha kujiunga na vyuo vikuu idadi ya wanawake imeongezeka na kufikia asilimia 34.5, hata hivyo ana angalizo kuwa utoro, mimba za utotoni na unyanyasaji kijinsia. 

Anasema pengo la kijinsia linaonekana kwenye dira inayomaliza muda wake kwa sababu watoto wengi wanaotakiwa kuwa shuleni hawako darasani kutokana na unyanyasaji kingono na utumikishwaji kwa upande wa wavulana.

Rose anasema wanawake wanataka makosa hayo yarekebishwe ili elimu bora ipatikane isiwe ‘elimu cheti’ bali kupata maarifa ya kupambana na mabadiliko na changamoto za dunia ya sasa na kubadilisha maisha ya wanawake.

Rose anakumbusha kuwa dira inayomaliza muda haikuweka usawa wa kijinsia kuwa suala mtambuka mbali na kulitaja kwenye maisha bora kwa kila Mtanzania. 

Anasisitiza bado uwakilishi wa wanawake kwenye uongozi na siasa haujakaa sawa wanapata nafasi kwenye bunge kupitia viti maalumu na siyo mambo jumuishi ya kuhakikisha taifa linafikia uwakilishi wa 50/50.

Kadhalika, wanawake wanaona kwamba mchakato wa kupata viti maalumu siyo wa uwazi, lakini japo unawapa ubunge unawanyima nafasi za kuwa Waziri Mkuu na pia kupata fedha za mfuko wa maendeleo ya jimbo.

Akichambua pengo la usawa wa kijinsia kwenye kumiliki rasilimali, ajira na kuwa na uwezo wa ushindani kwenye dunia ya sasa, Mkurugenzi wa WFT, anasema 

“Dira haijawezesha wanawake kumiliki rasilimali kwa mfano ni asilimia nane pekee wanaomiliki ardhi. Ajira ni shida, walioajiriwa sekta ya umma ni wachache sana na yote hayo yanahitaji kufanywa upya kwenye dira ijayo.”

Aidha, “Takwimu zinaonyesha kuwa kwenye kilimo wanawake ni asilimia 54, wanaume ni 44, kwenye ajira sekta ya umma ni asilimia 48 wakati wanaume ni asilimia 68, kwenye mashirika ya umma ni asilimia 18 pekee. Tunajiuliza ajira zinapatikanaje? Kuna vikwazo gani…? Anahoji Rose.

Akizungumzia umiliki wa rasilimali anasema asilimia saba pekee ya wanawake wanamiliki nyumba, wakati asilimia 28 wanamiliki kwa ubia na wanaume jambo linaloongeza hofu kuwa mwanaume akifariki mama anaweza kufurumushwa.

Pia, anasema wanawake asilimia nane pekee wanamiliki ardhi lakini ndiyo wanazalisha mali na wanaolilisha taifa.

UONGOZI / UTAWALA BORA

Rose anazungumzia utawala na uongozi ambako dira ilitamani kila Mtanzania awe kiongozi na ashiriki kwenye kuendeleza taifa na kupiga vita rushwa na uwajibikaji.

Wanawake wameongezeka katika uongozi lakini bado idadi yao ni asilimia 27 kwenye ngazi za juu.

Katika kushiriki uongozi ndani ya jamii hasa kuufikia uongozi kupitia uchaguzi jimboni, mitazamo hasi na rushwa ya ngono imewakwamisha kuchaguliwa.

Kwa ujumla wakati huu wa kuangalia kazi na huduma ya Mkapa katika maendeleo ya taifa suala la kuwa na dira yenye mtizamo wa kijinsia ni muhimu ili kila Mtanzania mtoto hadi mzee, mwenye ulemavu na viungo kamili afikie maisha bora hayati Mkapa aliyoyatamani kuwapatia ifikapo 2025.