Mbowe anapoingia katika orodha watekelezaji makubwa siasa nchini

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 06:15 PM Apr 02 2024
Mweyekiti wa CHADEMA, Freman Mbowe (mbele katikati), akiwa katika harakati za maandamano ya chama chake Machi mwaka huu.
MAKTABA
Mweyekiti wa CHADEMA, Freman Mbowe (mbele katikati), akiwa katika harakati za maandamano ya chama chake Machi mwaka huu.

IKO wazi hadi sasa kinapotajwa chama kikuu cha upinzani katika sura ndani na nje ya Bunge, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ndicho kinashika nafasi hiyo.

Swali linapokuja sababu za msingi, kinajijulisha katika idadi ya wanachama wake, hata wabunge ambao kilikuwa nao kwenye ulingo wa bunge kabla hakijakumbwa na changamoto.

 Kwa sasa mshindani kisiasa anayeitoa jasho CCM pale wanapochuana katika ubishani wa kisiasa, nje ya sanduku la kura, bado CHADEMA inashika nafasi hiyo. 

Pale unapochimbwa mzizi wa uimara huo, hapo nafasi ya mwenyekiti wake wa sasa, Freeman Mbowe inaonekana. Pia, inapoaanza safari ya chama hicho tangu zama hizo katika uasisi wake, leo ikiwa miaka 30 na ushee, wengi waliitafsiri CHADEMA kama ‘chama cha wakubwa’ kwa maana ya wale wenye uchumi mzuri. 

Pia, ikasambaa chama hicho kimeegemea sana ufuasi wa Kanda ya Kaskazini kwenye uasisi wake mwaka 1992, ishara yake ikienezwa chama cha matajiri, pia unasaba wake kimeegemea Kanda ya Kaskazini, kilipozinduliwa Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam.

 Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)  na Waziri wa Fedha Mstaafu, Mzee Edwin Mtei ndiye Mwenyekiti wa kwanza taifa wa chama hicho tangu mwaka 1992 hadi 1998, akiwa mwanachama mwenye kadi namba moja. 

Kadi namba mbili ikashikiliwa na Brown Ngwilulupi (marehemu), aliyewahi kuwa Meneja Mkuu wa Kiwanda cha Sigara (TCC).
 
 Mwanasheria na Naibu Gavana Mstafau wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Bob Makani (marehemu) aliyemrithi Mtei tangu 1998 hadi 2004, kuiongoza alikuwa na kadi namba tatu. Kwa kuwa aliwahi kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika, alivuta wanasheria wengi CHADEMA.

 Baada ya Mzee Makani kumaliza muda wake, Mbowe alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho taifa na kila uchaguzi amekuwa akishinda na kujikuta akiendelea kushikilia nafasi hiyo hadi sasa.

 Lakini, nikirudi nyuma kwanza, Mbowe ni nani? Huyu ametoka katika nyumba inayohubiri siasa, baba yake mzee Aikaeli Mbowe alikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya TANU kisha CCM.

 Hivyo, ni wazi Mbowe (mtoto), anaijua siasa, ndio maana akatumia mageuzi ya kisiasa kwenda upande wa pili kama walivyofanya baadhi ya watoto wa waasisi wa TANU akiwamo, Makongoro Nyerere.

 Mbowe huyo huyo, ndiye aliyebadili upepo wa CHADEMA na kusababisha chama kuwa na wafuasi wengi, na kuondoa dhana iliyojengeka kuwa ni chama cha matajiri au Kanda ya Kaskazini, kumfuata Mtei.

 Tangu ashike nafasi hiyo, amekitoa chama kuwa cha watu wa chache kuwa cha wengi, hivyo ni wazi kwamba inaweza kuwa vigumu kumtenganisha Mbowe na kuzaliwa kwa CHADEMA.
 

WAKATI MGUMU 
 

Mbowe anashika nafasi hiyo, wakati wa migongano na migogoro ndani ya vyama vya upinzani vikiwamo vya NCCR- Mageuzi, UMD na vingine vingi vilivyokumbwa na kadhia hiyo kubwa.

 Lakini kinyume chake, ametumia fursa hiyo kuondoa kwamba chama hicho ni cha vigogo na kukileta kwa wengi, wakajiunga nacho kwa kukiona kuwa ndicho chama chenye upinzani wa kweli.

 CCM imewahi kusema kuwa inategemea kura za wanawake kwamba ndio mtaji wao, lakini kwa upande wa Mbowe, akajikita katika vyuo na kuchota wasomi wakiwamo kina Zitto Kabwe, Kalisti Komu na wengine wengi akatengeneza ngoma kubwa.

CHADEMA kimewalea na kuwafikisha hapo walipo, vilevile chini ya uongozi wa Mbowe, kimeonyesha ndicho chama imara huku vingine vikikumbwa na migogoro, kuchoka au kusambaratika na kusababisha baadhi ya wanachama kwenda CCM.

Ndani ya wakati huo, chama hicho kilikuwa kimeshaweka idadi kubwa ya wabunge, nahodha wao akiwa Mbowe Hai, lakini baadaye walipata misukosuko hadi kukosa ubunge, lakini Mbowe ameendelea kuwa imara na kuweka msukumo wa siasa za CHADEMA.

 Aidha, ni kipindi hicho CCM nayo ikawa makini na kuwekeza katika vyuo ikianzia Chuo cha Mzumbe kama ngome yake kuu wakapatikana vijana wakiwamo Dk. Emmanuel Nchimbi ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Amos Makalla na wengine wengi.Pia, kama ilivyo kwa vyama vya siasa, CHADEMA nayo imewahi kupitia magumu wakati fulani kati ya mwenyekiti Mbowe na makamu wake Chacha Wangwe (marehemu).
 
 Ulitokea mpasuko, moja ya safu yake muhimu, kijana aliyekwisha iva kisiasa Zitto Kabwe mpinzani wa CCM na Profesa Kitila Mkumbo wakaondoka huku Prof. Mkumbo akienda CCM.

 Yupo Joseph Selasini aliyejiunga baadaye na chama hicho na kuwa mbunge wa Rombo mkoani Kilimanjaro, lakini naye akaondoka kwenda akiwa na Kalisti Komu wakaenda NCCR- Mageuzi.

 Hivyo, magumu yaliyoikumbuka kambi ya upinzani huwezi kuyatenganisha na Mbowe ambaye ni mwathirika mkuu, ambaye amewahi kuwekwa ndani miezi sita bila dhamana. 

 Ni katika kipindi hicho chote hata kufikia siasa za Tanzania katika siasa za kimataifa, msamiati Mbowe unachukua nafasi.
 
 4R ZA RAIS SAMIA
 
 Itakumbukwa kuwa mwanzo wa awamu ya sita na siasa zake za 4R, utekelezaji wake ulimhusu Mbowe moja kwa moja, kwani siku aliopata msamaha, akawa na mwaliko wa kuteta jambo lao na mkuu wa nchi.

  R ya kwanza  ambayo ni 'Reconciliation', yaani maridhiano au upatanisho, R ya pili ni Resilience', yaani ustahimilivu, R ya tatu 'Reforms', yaani mageuzi na R ya nne ni 'Rebuild', yaani kujenga taifa.

 Falsafa hiyo yenye 4R inagusa kila nyanja, sasa imepita miaka miwili hatujasikia Mbowe akilalamika wala kulaumu haki yake. Hapo historia yake ndefu na hulka vinatoa ishara kuwa 'roll model' wake ni mzee Nelson Maendela, Rais kwanza mweusi wa Afrika Kusini.

 Mzee huyo anasimama katika utashi wake huo licha ya kukaa kwa miongo miwili na ushee gerezani. Hivyo, kikubwa ndani ya utashi wake, daima Mbowe naye hajatoka ndani ya mstari wa anachodai ndani ya siasa za CHADEMA. Mathalani, simulizi za katiba na haki za Watanzania. 

Huku chama hicho kikidumu nje ya mipasuko inayoviathiri vyama vya upinzani, kimekuwa na nguvu thabiti ambayo hakuna wa kukishangaa kwa jinsi kinavyojitanabaisha.

 Mfano, maandamano ya chama hicho yametekelezwa katika majiji manne nchini, huku yakifana. Hapana shaka Freeman Aikael Mbowe anaingia katika orodha ya viongozi bora wa kisiasa nchini.

 Kwanini? Kwa sababu hajawahi kukaa nje ya msimamo wake anaoamini, hulka yake ni chanda na pete ya hayati Nelson Mandela, ambaye hakukata tamaa kupambana hadi nchi yake ilipopata uhuru.