Malipo kidijitali yaonekane kupaisha mapato serikalini

By Dk. Felician Kilahama , Nipashe
Published at 10:04 AM Jul 24 2024
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba.
Picha: Maktaba
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba.

MWAKA wa fedha 2023/2024 umemalizika serikali ikitarajia kutumia Shilingi trilioni 49.35 kutimiza mipango mbalimbali ya maendeleo kwa bajeti iliyoanza mwezi huu.

Kwa ujumla hiki ni kiasi kingi cha fedha wananchi wanategemea mafanikio mengi yatakayoboresha huduma za afya katika kipindi hicho kilichoanza Julai 1, 2024 hadi Juni 30 mwakani.

Pamoja na ongezeko la bajeti 2024/2025, bado ni mipango na utekelezaji rasmi utategemea upatikanaji wa kodi na mapato mengine ya serikali, kwenye hazina chombo mahususi kinachosimamia masuala ya mapato na matumizi ya fedha za serikali.

Kwa kushirikiana na vyombo vingine hususani Benki Kuu, TRA, serikali za mitaa na taasisi za umma.

Bunge pia kupitia kamati zake za kisekta, huwajibika kufuatilia matumizi ili yaendane na kile lilichopitishwa ukiwamo muswada wa fedha ambao ukisainiwa na Rais, unakuwa sheria ya fedha ili makadirio na matumizi ya fedha yapate nguvu ya kisheria. 

Katika kutekeleza bajeti hii serikali inasisitiza kuweka mkazo wa matumizi ya mifumo ya kielektroniki ikiwa ni pamoja na kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) (ICT), kukusanya mapato.  

Pia kutumia mfumo wa serikali wa kielektroniki wa malipo ya (GePG) kwa wizara na taasisi nyingine pamoja na namba ya udhibiti katika miamala yote ya kiserikali na matumizi zaidi ya mashine za kielektroniki za EFD, ili kuongeza ufanisi wa kukusanya kodi na tozo mbalimbali.

Hiyo ni mifano michache ya ambayo kiuhalisia ikitumiwa vizuri inaweza kuongeza mapato ya serikali kwa kiasi cha kutosheleza mahitaji ya taifa kila mwaka bila kuhangaika kukopa. Hata kwa kulazimika kukopa iwe ni wa kiasi kidogo,

Tunajiuliza tunakopa kila mwaka ili kufanya kitu gani cha lazima? Iwapo nia ni kutaka Watanzania waende kwenye mwezi, wengi tutasema hilo siyo hitaji la msingi kulazimika kukopa. 

Lakini vipaumbele vya taifa vikiwa vyenye kuinua maisha ya wengi serikali ikope, iwapo nguvu zimepwaya na pawepo sababu za kuridhisha. 

Hata hivyo, kufanya kazi kwa bidii na kila Mtanzania kuwajibika ipasavyo; nchi ina utajiri mwingi rasilimali kama ardhi na watu ili kufikia maendeleo.

Kiuhalisia taifa bado liko kwenye kuhangaikia maendeleo halisi na endelevu kwa wananchi wake. Kwa kiasi fulani limepiga hatua lakini bado hali ni tete na hasa ikizingatiwa ukubwa wa nchi na ongezeko la watu pamoja na mifugo.

Taifa fulani, linaweza likasifiwa kwa kuwaletea maendeleo watu wake lakini ukiangalia ukubwa wake na namba ya watu bado utaona kuna tofauti na nchi yenye eneo kubwa kama Tanzania. 

Mathalani, taifa lenye eneo dogo rasilimali zake pia ni haba ukilinganiswa na lenye eneo kubwa kama Tanzania, yenye rasilimali tele tena ikipatikana na Bahari ya Hindi kwa zaidi ya kilomita 1,000, ikimiliki rasilimali zilizomo ndani ya ukanda wa kilomita 200 baharini kutoka ardhi inapoishia.

Kuna mikoko takribani hekta 150,000, zenye ikolojia ya kuzalia samaki na viumbe bahari wengine wengi. 

Kimsingi mapato ya serikali yanatokana na wananchi na wawekezaji kwa kulipa kodi, kadhalika, uwezo wa kulipa kodi ni kutokana na kipato kinachotokana na matumizi ya ardhi kuzalisha mali kupitia kilimo na ufugaji, matumizi mbalimbali ya maliasili zilizopo na biashara.

Pia, upo utalii, ujasiriamali, uwekezaji wa namna mbalimbali na huduma. Watanzania tunapoiweka serikali madarakani tunatarajia itumikie na kutuletea maendeleo tunayotarajia.

 Kwa upande mwingine ni wajibu wetu kuhakikisha tunaiwezesha kwa kulipa kodi na tozo kufanikisha utekelezaji wa mipango kupata maendeleo tunayoyatarajia.

Wengi tungependa kulipa kodi ili ndoto zetu kimaendeleo ziweze kutimizwa, mathalani, tumeshuhudia wengi wakimiminika kutumia usafiri wa reli-mwendokasi ya SGR kwenda Morogoro ikiwa ni ishara njema ya matokeo ya juhudi za serikali.

Kwa uzoefu tulionao changamoto za kulipa kodi zimekuwa zikijitokeza sababu viwango vya kodi na tozo pamoja na ukusanyaji unavyofanyika; lakini siyo kuwa watu hawataki kulipa.

 Kadhalika, walipakodi wanapokuwa hawaoni  kinafanyika kunajitokeza sintofahamu kwamba nalipa kodi ili iweje? Iwapo matumizi ya fedha hizo yanapokuwa hayakisi viwango vya maendeleo; kunakuwapo na vinyogo kwenye kulipa lakini haitekelezi kilichotarajiwa kutokana na ubadhirifu au upotvu wa fedha za umma kwa kukosa usimamizi madhubuti. 

Ni imani yangu kuwa iwapo kutakuwapo na usimamizi madhubuti na uwajibikaji wa pamoja na viwango vya kodi na njia za makusanyo pia zikawa rafiki, hakuna shaka wengi watapenda kulipa kodi kwa maendeleo ya nchi yao. 

Ikumbukwe watu wengi tunaoishi mijini maisha yanategemea bidhaa za madukani yawe madogo kwa makubwa –‘supamaketi’ pia kwenye masoko ya bidhaa za shambani na viwandani kama Kisutu Dar-Es-Salaam, Kingalu, Morogoro na Mwanjelwa Mbeya. 

Wanaouza bidhaa madukani wanatakiwa watumie mashine za kielektroniki za EFD, TRA inasisitiza, “ukinunua dai risiti; ukiuza toa risiti.”

Hata hivyo, uzoefu unaonyesha kuwapo kukengeuka kuhusu matumizi ya mashine hizo muhimu za kufanikisha kupata mapato.

Ukinunua bidhaa kwenye maduka makubwa mpokea fedha anapofungua sehemu ya kuweka fedha, hapohapo risiti inajitokeza kupitia mfumo uliounganishwa na kompyuta ya mauzo.

Risiti inaonyesha mchanganua wa kiasi kilicholipwa na VAT anayokatwa kulingana na thamani ya bidhaa alizonunua na ndipo ‘dai na toa risiti’ inapofanikisha.

Kwenye biashara za mitaani, na maeneo mengine yenye mikusanyiko mikubwa ya wajasiriamali na wateja wengi mijini na majijini, matumizi ya utaratibu kama huo si kwa viwango tarajiwa. Walio na EFD ni wachache, utaratibu wa kudai risiti ni kero mno hadi kununiana. 

Tatizo ni kukwepa VAT muuzaji akisema usipodai risiti bei ni kiasi fulani ukidai risiti utalipa zaidi mteja atakubali kulipa bila risiti.  

Tusidanganyane kwa asilimia 18 VAT inayotozwa uzalendo haupo. Ikipungua kwa kiwango ambacho kitawafanya Watanzania kuwa wazalendo haina shida hata wauzaji watapata bidhaa kwa gharama nafuu, muuzaji na mteja tupata risiti bila vikwazo. 

Vilevile, tutasema ‘watumishi wa TRA ni wenye ukwasi’ hata kama mishahara yao ni mikubwa, tukumbuke ni binadamu wenye udhaifu kama wengine.

Pia dunia imezingirwa na bidhaa nyingi, hatarishi na za kutamanisha kupindukia’. Bila kuimarisha mifumo ya kielektroniki, pamoja na sera, sheria na kusimamia ipasavyo; serikali itaendela kupoteza fedha nyingi hata kama kutakuwapo na miamala mingi.

Matumizi ya kielektroniki pamoja na miamala kupitia mashine zinazotumiwa na binadamu, ni rahisi kughushiwa. 

Wataalamu wanaohusika, kwa ujanja wanao uwezo wa kutoa miamala batili yenye kuwanufaisha wachache badala ya wengi maana miamala halisi haitawasilisha fedha hazina.

 Kwa msemo wa mitaani fedha ya umma inapigwa kiwiko pia inachukua muda mrefu kugundua udanganyifu hivyo, hasara inakuwa kubwa kiasi cha kuzorotesha huduma za kijamii na maendeleo yanayotarajiwa.

 Serikali iwe macho kuhusu matumizi ya kielektroniki, na panapogundulika ubadhirifu, hatua kali kiutawala na kisheria zichukuliwe bila kukawia na kwa misingi ya uwajibikaji.