Klabu tano zilizotikisa usajili Ligi Kuu 2024/25

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 01:37 PM Jul 22 2024
news
Picha: Yanga
Prince Dube.

DIRISHA la usajili limezidi kunoga, timu zote 16, zimekuwa zikifanya usajili kulingana na mahitaji ya vikosi vyao.

Hata hivyo, baadhi ya timu zimeonekana kusuasua kwenye soko la usajili, zingine zikisajili wachezaji wa kawaida tu, wengine bila makeke, lakini zipo klabu ambazo zimekuwa zikifanya usajili ambao umeshtua mashabiki wa soka nchini na kuwa gumzo kwenye vyombo vya habari.

Hapa tunakuletea klabu tano ambazo pamoja na kufanya usajili wake kwa kujiimarisha kwa mapungufu ya msimu uliopita, lakini umeonekana kuwa tishio na kusumbua vichwa vya mashabiki wa soka nchini. 

1. Simba

Msimu uliopita si tu kupata ubingwa, ilishindwa hata kuipata nafasi ya pili ili kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika. Matokeo yake ikaangukia Kombe la Shirikisho Afrika kwa kushika nafasi ya tatu.

Kutokana na hilo, yamefanyika mabadiliko makubwa sana kwenye kikosi cha Simba. Imeondoa wachezaji wengi hata wale ambao walionekana tegemeo na kusajili wachezaji wengi wa ndani na nje ya nchi.

Kuelekea msimu ujao, imesajili wachezaji wapya 13, saba wageni na waliobaki ni wazawa.

Ndiyo klabu ambayo usajili wake umeonekana kutikisa zaidi kwenye dirisha hilo kutokana na wingi, pamoja na aina ya wachezaji ambao ingawa si maarufu au mastaa sana kwenye soka la Tanzania, lakini wameonekana kufanya vema waliokotoka ikiwamo wengi kuwa ma MVP (wachezaji wenye thamani zaidi) kwenye ligi zao.

Jushua Mutale kutoka Power Dynamos ya Zambia, Steven Mukwala akitokea Asante Kotoko ya Ghana, Jean Charles Ahoa (Stella Adjame, Ivory Coast), Debora Fernandes Mavambo (Mutondo Stars, Zambia) na Augustine Okajepha (Rivers United, Nigeria) na Valentin Nouma (FC Saint Eloi Lupopo, DRC).

Wachezaji sita wazawa waliotangazwa mpaka sasa ni Lameck Lawi kutoka Coastal Union, Abdulrazack Hamza (Super Sports, Afrika Kusini), Valentino Mashaka (Geita Gold), Omari Omari (Mashujaa FC), Kelvin Kijili (Singida Black Stars) na Awesu Awesu (KMC). Kwa mujibu wa baadhi ya viongozi wao ni kwamba huenda idadi ikaongezeka. 

2. Yanga

Haikusajili wachezaji wengi msimu huu kutokana na kutopoteza wachezaji wake muhimu walioipatia mafanikio msimu uliopita, lakini wachache iliyopata saini zao ni wale mastaa katika soka la Tanzania.

Hilo limefanya usajili wa Yanga nao kuwa wa kushtua, na hasa ilipomsajili Clatous Chama kutoka Simba.

Ni usajili ambao ulizua mshtuko na mashangao mkubwa kutoka kwa baadhi ya mashabiki, wengine walioona kama ni ndoto.

Wakati mjadala mkubwa ukiendelea, ikamtambulisha Prince Dube kutoka Azam FC, na usajili huo kuendelea kuwa gumzo. Wachezaji wengine waliotangazwa na Yanga ni Chadrack Boka kutoka Klabu ya  FC Saint Eloi Lupopo, Duke Abuya raia wa Kenya na golikipa Khomein Aboubakar (Singida Black Stars), Aziz Andambwile (Singida Fountain Gate), pamoja na Jean Baleke (Al Ittihad, Libya), ambaye pamoja na kwamba Yanga haijamtambulisha mpaka sasa, lakini amejitambulisha mwenyewe kwa kufunga bao la kufutia machozi juzi katika mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Augsburg ya Ujerumani iliyochezwa nchini Afrika Kusini, Yanga ikipoteza kwa mabao 2-1. 

3. Azam

Kwa mara ya kwanza baada ya misimu 10, imepata tena nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika.

Baada ya kuipata nafasi hiyo ambapo mara ya mwisho ilikuwa msimu wa 2013/14, hivyo Azam FC ikaamua kufanya usajili mkubwa ambao nao ukawa gumzo kwenye mijadala ya soka.

Imefanya usajili wa straika Jhonier Alfonso Blanco, akitokea kwenye Klabu ya Rionegro Aguilas na kiungo mkabaji, Ever Meza wa Leonnes FC, wote ni raia wa Colombia na klabu wanazotoka ni za nchini humo, beki wa kati Yoro Mamadou Diaby (Stade Malien de Bamako, Mali), pamoja na kiungo mshambuliaji kutoka timu hiyo hiyo, Franck Tiesse, wote wakiwa ni raia wa Mali.

Azam pia imesajili Adam Adam kutoka klabu ya Mashujaa FC na kiungo mshambuliaji wa Kimataifa wa Mali, Cheickna Diakite (Real Bamako), kabla ya juzi kufunga usajili wake kwa kiungo mkabaji Mamadou Samake kwa mkataba wa miaka miwili akitokea kwa miamba ya Algeria, CR Belouizdad ya Algeria. 

4. Singida Black Stars

Imefanya usajili ambao unaonekana ni kama wanaitaka nafasi ya tatu au ya nne kwenye Ligi Kuu msimu ujao, lakini kama watakuwa wapo 'siriasi', wanaweza hata kushika nafasi ya pili au ubingwa kabisa.

Kwanza kabisa imemshuka kipa namba moja kutoka Timu ya Taifa ya Sierra Leone, Mohammed Nbalie Kamara, aliyekuwa akiichezea Horoya ya Guinea.

Halafu ikaenda Ivory Coast katika Klabu ya Asec Mimosas na kumsajili beki wa kati Anthony Tra Bi Tra, ikawasajili Edward Manyama na Ayoub Lyanga kutoka Azam, Kennedy Willson (Simba), Metacha Mnata (Yanga), Ibrahim Imoro (Al Hilal, Sudan) na Joseph Guede (Yanga). 

5. Dodoma Jiji FC

Baada ya kunusurika kushuka daraja au kwenda 'play off', ikaponea katika mechi za mwisho na hasa baada ya Simba kuifunga JKT Tanzania mabao 2-0 katika mechi ya mwisho, ikiinusuru timu hiyo yenye Makao Makuu jijini Dodoma na kuwapeleka maafande katika mechi za mchujo, kuelekea msimu ujao inaonekana imejifunza kitu.

Nacho ni kufanya usajili wa wachezaji mahiri, wakubwa na wenye uwezo. Ni moja kati ya timu za madaraja ya kati iliyofanya usajili mkubwa ulioshtua wengi.

Imemtwaa kipa mahiri aliyoibeba sana Kagera Sugar msimu uliopita,  Allain Ngeleka, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Pamoja naye, imewatwaa Ibrahim Ajibu kutoka Coastal Union, Reliants Lusajo (Mashujaa FC), Dickson Mhilu ambaye amewahi kuichezea Simba, akitokea Kagera Sugar na wengineo.