Kilio bei ya ufuta, ghafla kilivyogeuka tabasamu kwa wakulima Mkuranga

By Yasmine Protace , Nipashe
Published at 08:11 AM Jul 19 2024
Gari likishusha ufuta katika ghala kwa ajili kuuzwa mnadani katika mkoa wa Pwani.
PICHA: YASMINE PROTACE.
Gari likishusha ufuta katika ghala kwa ajili kuuzwa mnadani katika mkoa wa Pwani.

KATIKA kuhakikisha wakulima wananufaika na mazao yao kupitia minada, serikali imekuwa ikiboresha mazingira ya minada yake, ili wakulima waweze kunufaika nayo.

Awali, wakulima hao walilalamika hawanufaiki nayo kutokana na kuuzwa kiholela kutokana na kutokuwa na usimamizi sahihi. 

Hivyo, serikali imeweka taratibu za minada ,ikiwamo na kuwapatia wakulima ruzuku za pembejeo kwa ajili ya kuzalisha kilimo na chenye tija. 

Serikali ilianzisha mnada kwa njia ya mfumo unaoitwa TMX, ambayo wakulima waliulalamikia mfumo huo kwao wanunuzi na kusababisha mazao kuuzwa kwa bei ndogo au kutonunuliwa. 

Hata hivyo, baada ya kuulalamikia mfumo huo, serikali ikachukua hatua za haraka kuboresha, sasa wakulima hao katika baadhii ya maeneo walikiri ahueni ya bei inayoongezeka, kwa wanunuzi wanaofika maghalani. 

Hiyo ikashudiwa katika Msimu wa Tano wa Mnada wa Ufuta, ambako Nipashe ilikuwapo katika mnada wa Kingoma wilaya Mkuranga, mkoani Pwani, ufuta ukiuzwa wote uliokusanywa ghalani. 

Meneja wa Chama cha Ushirika Mkoani Pwani (CORRECU), Hamis Mantawela, anasema huo ni mnada wa tano wa ufuta kufanyika hapo, ambako zaidi ya tani 1,000 za mazao zilikusanywa na kuuzwa. 

" Tani 1,195,189 zimekusaywa Mkuranga na kuuzwa kwa kilo moja shilingi 3500.3" anasema Mantawela. 

Anaongeza kuwa ni wajibu wa wakulima wa ufuta kuleta ufuta katika minada miwili iliyosalia ili waweze kuuza. 

Matawela anasema, kwa sasa bei ya ufuta imepanda tofauti na minada ya nyuma, kilo moja iliuzwa shilingi 301,17 huku mnada wa nne ufuta uliuzwa shilingi 3,280.13. 

Anasema serikali imetoa mafunzo ya siku tatu ili viongozi wa vyama vya amccos kujua jinsi ya kuitumia mifumo hiyo. 

" Mafunzo yaliandaliwa ya siku tano,lakini yamefanyika ya siku tatu,hayo yaliyobakia ya siku mbili yataendelea," anasema. 

Anaongeza kuwa, mafunzo hayo yatasaidia hata katika mnada wa mbaazi ambao utafanyika hivi karibuni. 

Meneja huyo anasema, mnada usaswa umebaki utakaofanyika mara mbili, hivyo anawaonya watakaouza ufuta kwa njia za panya watachukuliwa hatua, akionya “viongozi wa vyama vya ushirika wasifurahie ufuta kutoroshwa.” 

" Wapo watu waliogoma kuleta ufuta katika mnada wanategemea mnada uishe ili wautoreshe ,tutakaa katika vizuia ili kuwakamata wale wanaotaka kuutorosha ufuta," anasema. 

Anaongeza kuwa, atakayekamatwa anatorosha ufuta, atalipishwa faini ikiwamo kuchukuliwa gari na ufuta aliobeba. 

Kwa mujibu wa Mantawela. baada ya mnada wa ufuta, unaofuata ni mnada wa mbaazi na kisha utafuata mnada wa korosho. 

Anasema wataanza kutembelea mashamba ya mbaazi, ili kujua idadi ya mbaazi zilizopo katika mashamba. 

" Maghala yataendelea kuwapo, ila kama mbaazi hazipo ni jukumu la viongozi kusema,"anaeleza, huku akiwa na ushauri kwa wakulima kuleta ufuta mnadani na endapo watausubiri mnada wa mwisho,  hatari yake bei inaweza kuwa mbaya na wakashindwa kunufaika na mauzo kama ilivyo sasa. 

" Wakulima wajue mnada wa mwisho huwa una mambo mengi sana, unaweza ufuta usifike idadi ile ambayo unajua ndio mlioikusanya maana kunakupasuka mifuko ufuta ukamwagika chini na kufanya kilo kupungua, hivyo nawashauri wakulima msifiche ufuta majumbani mkauleta mnada wa mwisho," anasema. 

Mwenyekiti wa CORECU mkoa wa Pwani, Mussa Mng'eresa, anawaasa wakulima kuwa bei ya ufuta imepanda na vyema wapelekwe mavuno yao katika vyama hivyo, kufanyike biashara ya mavuno yao. 

Anasema, awali biashara ya ufuta ilishuka sana na ghafla kutoka kilo shilingi 4000 hadi shilingi 3000. 

Omary Mussa, Mwenyekiti wa AMCCOS Kibaoni, anasema bei ya ufuta imepanda na kuna tabia ikiwa chini, wakulima huwa hawajitokezi katika maghala kuleta ufuta wao.