Kambi Fistula yaanika magumu ya wagonjwa, ikiwaachia neema maisha mapya kinamama 24

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 07:50 AM Jul 18 2024
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga Dk.Luzila John akisikiliza ushuhuda wa aliyefanyiwa upasuaji.
PICHA:MARCO MADUHU.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga Dk.Luzila John akisikiliza ushuhuda wa aliyefanyiwa upasuaji.

UGONJWA wa fistula unaelezwa kuwakumba wanawake, wanaotokwa na haja ndogo na kubwa muda wote.

Hali hiyo imekuwa ikisababisha wanawake kushindwa kufanya shughuli zao mbalimbali za kiuchumi, kutokana na kukwepa aibu ya kutokwa na haja ndogo na kubwa muda wote.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake, kutoka Hospitali ya Rufani Bugando jijini Mwanza, Dk. Elieza Chibwe, akiwa katika safu ya waliopiga Kambi mkoani Shinyanga kutoa huduma ya matibabu bure ya upasuaji ugonjwa wa fistula, anautakia ni ugonjwa wa aibu na na fedheha kwa mwanamke.

Anasema tatizo la fistula ni kubwa kwa wanawake, na husabishwa na uchungu pingamizi anapokuwa mjamzito, katika uwazi unaounganisha njia ya uzazi na sehemu ya haja kubwa na ndogo, kusababisha kutokwa kinyesi na mkojo muda wote.

“Matibabu ya fistula ni upasuaji tu, na tunataka hadi kufikia 2030 tatizo la Fistula liwe limekwisha kabisa,” anasema Dk. Chibwe.

MGONJWA ANENA

 Mwanamke mmoja (jina tunalo), anaelezea namna ugonjwa huo fistula ulivyomtesa ndani ya miaka 38, akisema kwa kipindi hicho hajaweza kufanya shughuli za kumuingiza kipato, akikwepa aibu hiyo kutokwa na haja kubwa na ndogo muda wote.

Anasema ilifikia kipindi haja kubwa inaanza kutoka, hivyo akaishi kwa tabu, huku mwanamke mwingine anasema yeye alipatwa na tatizo hilo la mwaka 1995, na kwamba muda kidogo mume wake alimkimbia, kutokana na kushindwa kuvumilia tatizo lake.

“Ugonjwa huu ni mbaya sana una mdhalilisha mwanamke na ulifanya mume wangu akanikimbia na kunitekeleza, uzuri tatizo hili lilinipata katika ujauzito wangu wa pili na mtoto alifariki na sasa nina mtoto mmoja wa kwanza ambaye ndiye ananisaidia na kuniuguza,” anasema.

“Tunashukuru Kambi hii ya Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake kutoka Bugando, kwa kutupatia tiba ya matibabu bure ya upasuaji wa ugonjwa huu wa Fistula, na sasa hali yangu inaendelea vizuri,” anaongeza.

Kambi hiyo ya Madaktari Bingwa Nane wa Magonjwa ya Wanawake kutoka Bugando, ilikaa kwa muda wa siku Tano mkoani Shinyanga, ikiwafanyia upasuaji wagonjwa wa fistula bure jumla wanawake 24. 

Mwakilishi kutoka Shirika la Americares Dk. Jonas Kagwisage, wafadhili wa kambi hiyo, anasema kwa sasa wamefanya kambi hiyo kushirikiana na Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake wa Bugando. 

Anasema wameifanya kwa muda wa siku Tano, wamefanikiwa kuwafanyia wa wagonjwa wa fistula wanawake 24, na kuwarejesha katika hali zao za kawaida.

 Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto Mkoa wa Shinyanga Halima Hamis, anasema tatizo la fistula linakumba zaidi wanawake wanaojifungulia nyumbani bila ya msaada wa wataalamu wa Afya.

 Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga Dk. Luzila John, anasema hospitali hiyo haina daktari bingwa mtaalamu wa upasuaji wa ugonjwa fistula, na kwamba hao hutibiwa Bugando Jijini Mwanza.

 Anasema, kupitia Kambi hiyo ya madaktari bingwa wa magonjwa ya wanawake kutoka Bugando, baadhi ya madaktari wao wamashajengewa uwezo na watakuwa wakitoa tiba hiyo ya fistula.

 Diwani wa Mwaaza Juma Nkwabi Kata ambayo ipo Hospitali hiyo ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, anaiomba serikali ipeleke madaktari bingwa katika hospitali hiyo, wa kutoa tiba ya fistula kwao.