KAACHA KUONA ANA WIKI TATU CHUO KIKUU...Rukia; kapoteza fani mazingira, kanasa utangazaji

By Beatrice Moses , Nipashe
Published at 10:10 AM Oct 10 2024
Rukia Mohamed, akitumia simu yake
Picha: Beatrice Moses
Rukia Mohamed, akitumia simu yake

“PENYE njia pana njia,” ni msemo unaothibitishwa na Rukia Mohamed, kijana aliyekumbwa na mkasa wa ulemavu, hata akashindwa kuona wiki tatu tu baada ya kuanza masomo Shahada ya Kwanza ya Sayansi Mazingira, katika Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) mwaka 2021.

Ni tukio liliomwachia wakati mgumu akitaka tamaa kimaisha, hasa alipofikiria njia panda ya kuendelea na masomo yake. 

Hata hivyo, leo hii Rukia ni mwanafunzi wa mwaka wa pili Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC), zao la jitihada na kutokata tamaa.

Anataja mbadala wa teknolojia ya kisasa ya mawasiliano, ilimpa mwanga mpya kuwa na nafasi ya kuendelea na masomo hayo, ingawa amelazimika kubadili fani kutoka mwana- mazingira hadi dira kuwa mtangazaji kwenye vyombo vya habari.

MKASA ULIVYOKUWA 

Rukia ambaye sasa yuko katika mafunzo kwa vitendo katika ofisi za Chama cha Waandishi Wanawake (TAMWA), Dar es Salaam, Nipashe imemshuhudia akifanya mafunzo ya vitendo kwenye mfumo wa mtandao ‘Online’ akiwa na sauti nzuri, pia uwezo bora wa kuelezea jambo.

Anasimulia alikotoka kwamba, zilikuwa wiki tatu zinakamilika tangu kuanza masomo (mwaka wa kwanza) SUA, siku hiyo alijikuta anachelewa kuamka pasipo kutarajia, kila alipofumbua macho akabaki anaona giza.

Akahisi bado hakujakucha hadi mwanafunzi wenzake alipogonga mlango wake kumuuliza kulikoni bado amelala, Rukia anamsimulia mwandishi katika ofisi za TAMWA, kwamba:  

“Nikamwambia mbona naona bado hakujakucha, baada ya kuamka nikagundua kwamba macho yangu ndiyo yamepoteza uwezo wa kuona. Nikaanza kulia, akanisaidia taarifa zikapelekwa kwa uongozi wa chuo, nikaruhusiwa kuondoka kwa ajili ya matibabu.”

 Anaeleza awali kabla ya kukumbwa na tatizo hilo, alikuwa na changamoto kushindwa kuona mbali, hivyo alikuwa anavaa miwani iliyomsaidia kumudu kuona vyema. 

Hivyo, baada ya tukio hilo akarejea nyumbani kwao Dar es Salaam, akapokelewa hospitalini kuchunguzwa na daktari, aliyemjulisha kuwa ‘retina’ (ngozi ya jicho) ndiyo imeachia, anatakiwa kufanyiwa upasuaji kwa gharama shilingi milioni 4.8.   

Rukia anasema ilikuwa kubwa kwao na hawakuweza kuipata wakati huo, hasa alikuwa anamtegemea mama yake, ambaye hakuwa na kipato cha uhakika. Baba yake alishafariki tangu mwaka 2018.   

Kijana huyo anasimulia baada ya kupoteza uwezo wa kuona, mama yake alidumisha ukaribu naye, kumsaidia wakati wote, hivyo akapambana kuuza baadhi ya vitu vyake upasuaji ufanikiwe.  

Ni upasuaji uliokuwa na hatua tofauti hadi kukamilika. Awali alianza kuona mwanga, giza na mtu akiingia ndani anamtambua kimaumbile, siyo sura halisi, kwa sababu aliona ukungu. 

“Kwa watu niliowatambua, hata asipozungumza natambua huyu ni nani. Baada ya miezi kadhaa, hali ilibadilika upande nikawa naona giza nikarejea tena.

“Daktari alinieleza kuwa mafuta yametumika kuweka hiyo retina yalikuwa mepesi, maji ya jicho yalifanya yalainike zaidi na kuyatenganisha, hivyo nilipaswa kufanyiwa upasuaji wa pili,’’ anasema. 

Rukia anafafanua gharama yake ilikuwa shilingi milioni 2.8 na baada ya ‘kuwalilia’ madaktari walipunguza hadi shilingi milioni 2.5 milioni, japo anakiri ilikuwa changamoto kuipata. 

 Rukia anaielezea Nipashe namna mama yake aliungana na dada yake, pia bibi mzaa mama wakauza baadhi ya vitu, ndipo fedha ikapatikana akafanyiwa upasuaji tena.

Hata hivyo, anasema awamu hiyo haikuwa na mafanikio, akieleza: “Upasuaji wa pili ulikuwa Mei mwaka jana, nilipata maumivu ya kichwa ya mara kwa mara hadi Septemba ndipo presha ikashuka na kuwa ya kawaida.”

Anaeleza daktari wake baada ya uchunguzi, akamwambia kuwa ‘retina’ ilishika vizuri baada ya upasuaji, lakini presha ya macho imesababisha mishipa ya fahamu kushindwa kutafsiri ipasavyo. 

Rukia anasema katika matibabu yake, aliambiwa anaweza kupona akienda kutibiwa nje ya nchi kwenye vifaa vya teknolojia ya juu ya utabibu, lakini akakwama gharama kubwa, wamejaribu kuomba msaada wa kuchagiwa fedha, lakini hakufanikiwa.

Baada ya kubaini haki hiyo, akaamua kutafuta uwezekano wa kurejea masomoni, changamoto ikawa kutojua lugha ya maandishi ya ‘nukta nundu’ inayotumiwa na wasioona. 

Pia, ni wakati alilazimika kwenda SUA kuomba kuhairisha muhula wa masomo, alikojibiwa isingewezekana, pia hata suala la kumhamisha ikawa ni changamoto, kwa sababu hakuwa na matokeo yoyote ya mitihani chuo haponi, hakuwahi kuifanya. 

Rukia anasema katika harakati zake kutafuta suluhisho aendelee na masomo, akafika katika Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro (MUM), alikokutana na anayetambulisha kwa jina moja la Mhando, aliyesimulia mkasa wake, akimpa taarifa zenye matumaini. 

Anasema, Mhando alimweleza Chuo Kikuu cha Dar es Saaam (UDSM), wangempokea na nafasi ya kuendelea kimasomo, kwa sababu kuna kitengo maalum kuhudumia wanafunzi wenye mahitaji maalum, hivyo akampa namba za simu za watu wawili awasiliane nao kufanikisha hatua hiyo.  

“Nilipompigia mtu wa kwanza alikuwa ni mwanamke, alijibu kwa kifupi kuwa hawezi kunisaidia, hakuna utaratibu wa kuhamishwa bila kuwa na matokeo,” anasimulia, akiitaja ni jibu lilikomkatisha tamaa, hata azma ya kumpigia simu mtu wa pili.

Rukia anasimulia kwamba, mdogo wake alimtia moyo kujaribu kuwasiliana na mtu wa pili, aliyemtaja kwa jina Dk. Lucas Kija, akinena, alivyokutana na faraja: 

“Alizungumza nami kwa upendo, huku akinifariji kwamba kama nina nia ya kusoma, basi niondoe hofu. Akanielekeza namna nzuri ya kufuata utaratibu wa kuhamishiwa UDSM, huku akinitia moyo kuwa hata kama sina matokeo ya kuonyesha, hiyo inatokana na yaliyoikuta hivyo nisaidiwe, kweli nilifanikiwa.”

AANZA KUJITEGEMEA

Rukia anaeleza akaanza kwenda kuhudhuria masomo ya awali kujifunza kutumia kompyuta kwa kuwa hakujua kutumia ‘nukta nundu’. 

“Nilijifunza kwa bidii, baada ya kufanikiwa kujua kutumia alimwomba mama yake amnunulie, akimjulisha kuwa tayari ameweza kuwasiliana hadi kuandika ujumbe wa maneno au kumpigia simu. 

“Mama alifurahi aliniambia nimtumie ‘sms’, nilipomtumia alifurahi sana. Kwangu simu na kompyuta vinanisaidia katika masomo yangu.

“Pia, nafuatilia mambo yanavyoendelea ulimwenguni kwenye mitandao ya kijamii ili kupata taarifa muhimu, pia napata burudani kwa kusikiliza vichekesho mbalimbali,” anasema.  

Msomi huyo anaeleza mbali na kumudu teknolojia, mama yake amemsaidia kumudu maisha ya kujitegemea, akimwongoza kufanya shughuli mbalimbali, ikiwamo kupika, kukata mboga, usafi, ikiwamo kupiga deki au kufua mwenyewe.  

Meneja wa Kituo cha Kuhudumia Wenye Mahitaji Maalum UDSM, Dk. Sara Kisanga, anasema Rukia alipokewa na kuanza kupewa ushauri wa kisaikolojia, kumfanya akubaliane na kilichomkuta, baada ya hapo akaanza kufundishwa kutumia kompyuta akiwa na hali yake ya kutoona. 

“Katika kituo hiki mafunzo hayo yanatolewa na wasioona wenzao ambao wamefuzu vyema mafunzo na wanauelewa mzuri wa matumizi ya teknolojia hiyo,” anasema, akijivuna alielewa vizuri na ana bidii kujifunza, hata akamudu kutumia kompyuta masomoni.

Dk. Kisanga anaeleza UDSM wapo makini katika kuhudumia wenye mahitaji maalum kulingana na uhitaji, wanahakikisha anakuwa salama na watu wa kumsaidia kwenye shughuli zake. 

Ni watu anaowataja wameandaliwa mazingira mzuri ya kwenda masomoni, kuna bajaji maalum wamepewa namba za madereva, kwa kuwa chuo ni kikubwa wanatumia usafiri. Pia, wanatumia wanapokuwa kwenye mafunzo ya vitendo. 

“UDSM imeanza kudahili wanafunzi wenye mahitaji maalumu mwaka 1978 na walikuwa wanafunzi wasioona wawili. Mpaka sasa wanafunzi waliodahiliwa wasioona 275, waliomaliza 210 na wanaoendelea na masomo ni 65,” anasema.  

Hadi sasa idadi ya wenye mahitaji malum wanaopokewa UDSM, imekuwa ikiongezeka wanafunzi mfano wanafunzi wasioona walijisajili kwenye masomo kwa mwaka 2022/2023 walikuwa 20, wakati 2023/2024 walikuwa 18, hatua inayoonyesha juhudi kuwawezesha wenye sifa za kusoma elimu ya juu zinazingatiwa vyema hadi kwa makundi maalum.  

“Huduma ya vifaa vya teknolojia kama kompyuta kwa wanafunzi wasioona yalianza mwaka 2008, hadi sasa walionufaika ni takribani 150 ambao wana uwezo wa kutumia vifaa kama kompyuta, ‘Braille Note Takers, Braille Sense na Orbit Reader 20,” anazitaja meneja huyo. 

Dk. Kisanga anasema kituo chao kinakabiliwa na changamoto, baadhi ni wanafunzi wanaotumia ‘nukta nundu’ kutokana na mazoea, wanakwepa kujifunza kutumia kompyuta, hali inayowasababishia changamoto kwenye ajira, kwa kuwa lugha hiyo haitumiki kwenye ofisi nyingi. 

Pia, anasema waajiri wengi wanakwepa kuwaajiri wenye ulemavu kutokana na dhana ya unyanyapaa, ingawaje wahitimu wao UDSM wanakuwa na sifa za kufanya kazi -wameiva kama walivyo wahitimu wengine wa kawaida.  

Ikirejewa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 toleo la mwaka 2023 kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, inahimzia fursa usawa katika utoaji elimu na mafunzo ni muhimu kwa kila Mtanzania kupate fursa hiyo. 

Inahimizwa ushiriki wa jinsia zote katika elimu na mafunzo, kuhakikisha kila Mtanzania anashiriki kuchangia maendeleo hayo na kuzingatia umuhimu huo, serikali imeendelea kutoa elimu na mafunzo kwa kuzingatia usawa kwa makundi yote pasipo kumwacha yeyote nyuma. 

 Vilevile, serikali imekuwa ikishirikiana na wadau wa elimu, kupanua na kuboresha mazingira ya utoaji elimu jumuishi na kumwezesha kila Mtanzania kupata fursa hiyo katika hali halisi ya yanavyopatikanaji rasilimali nchini.