Dk. Biteko alipoibua njia ya ufanisi na mafanikio katika sekta nishati

By Reubeni Lumbagala , Nipashe
Published at 06:20 PM Apr 02 2024
news
MAKTABA
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dotto Biteko.

“TUNAFANYA haya katika kusaidia wananchi kero zao mbalimbali ili tutakapokufa watu wasitutafute kwenye makaburi yaliyonakshiwa na marumaru, bali kwenye mioyo ya wale ambao walinufaika na sisi kutokana na haya tunayoyafanya.”

Maneno hayo maarufu yaliwahi kusemwa na mfanyabiashara na kiongozi mashuhuri wa zamani wa Morocco, Abu Abdullah Muhammad Ibn Battutah. Hiyo kwa mbali, inafanana na kauli aliyoitoa wakati fulani Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi kwamba ‘Maisha ni historia tu, basi jitahidi uwe historia nzuri.”

Swali libaki kwa kiongozi katika ofisi ya umma, anadhani kutokana na utumishi wake, hata kabla hajaondoka duniani, itakuwa historia nzuri?  Atagusa mioyo ya watu watakaokuwa wanakumbuka utumishi wake uliotukuka? 

Chama cha TANU (Tanganyika African National Union) kilichofanya kazi kubwa ya kuleta ukombozi Tanganyika (sasa Tanzania Bara), kiliweka ahadi zake ambazo wanachama na viongozi wake wa wakati huo na sasa CCM wanapaswa kuzielewa, kuziishi na kuzitendea. 

Mathalani, moja ya ahadi za mwanachama wake ni isemayo: “Cheo ni dhamana, sitatumia cheo changu wala cha mtu mwingine kwa faida yangu.”

Kimsingi, ahadi hiyo inalenga kuwakumbusha watumishi, watendaji na viongozi kuwa nafasi walizo nazo si zao, wala za kudumu, bali ni utumishi wa umma kwa muda tu, hivyo wanawajibika kuwatumikia wananchi kwa ufanisi.

Msisitizo wake hapo ni kwamba, haja ya kupeana dhamana na kamwe wasitumie nafasi zao au za watu wengine, kwa manufaa yao binafsi pekee. 

Licha ya kuwa ahadi hiyo ni ya wanachama CCM, lakini anaitaja inapaswa kufanyiwa kazi na yeyote anayekabidhiwa ofisi ya umma. 

Kwa mtumishi au kiongozi anayelewa vyema ahadi hiyo na kuifanyia kazi kikamilifu, utumishi wake unaleta manufaa na faida nyingi kwa wananchi na taifa na daima atakumbukwa na kizazi cha sasa na kijacho. 

Kuishi katika ahadi hiyo inatakwa ni kuwatumikia wananchi kwa kuhakikisha maslahi na haki zao wanazipata kwa wakati na kamwe hatakuwa sehemu ya kukwamisha na kuzuia kabisa haki kupatikana bali kuiwezesha kupatikana.

Siku chache zilzopita, akasikika Sheikh mmojawapo akiwaambiwa waumini wa dini yake wanaoendelea na mfungo, akisema kwamba muumini anayemfurahisha sana Mwenyezi Mungu, ni yule ambaye watu wengi wananufaika naye. 

Kwamba unavyopendwa na Mungu, kadri watu wengi wanavyonufaika naye, ndivyo pia anakuwa Jirani na baraka za hapa duniani na maiosja ya baadaye. 

NAIBU WAZIRI MKUU

Ni katika hilo, ndipo anapongezwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Dotto Biteko, ambaye kila mara amekuwa akisisitiza uwajibikaji, uzalendo na moyo wa dhati wa kuwatumikia wananchi, kwani kwa kufanya hivyo, kero za wananchi zinatatuliwa.

Vilevile ukatajwa ni mustakabli wa kufikiwa mipango na malengo ya nchi unatimia kwa wakati. Mathalani, hivi karibuni Dk. Biteko akifungua Mkutano wa Tano wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Nishati, akaisisitiza kuwa cheo ni dhamana, hivyo watumishi wa Wizara ya Nishati wakiwamo Tanesco wawahudumie wananchi, ili nchi iweze kusonga mbele kimaendeleo.

 “Yaani wewe kuwa mtu wa Tanesco au kuwa mtu wa Wizara ya Nishati, unaonaje fahari kuabudiwa na kutukuzwa kwa sababu ya cheo ambacho kwanza sio chako, ni cha watu…

“Hivi vyeo vyote mlivyo navyo, kikiwaemo cha kwangu sio vya kwetu ni ‘temporary’ (vya muda mfupi) kwa ajili ya ‘ku-service’ (kuhudumia) wakati ule. Kwanini msijifanyie marafiki kwa vyeo mlivyo navyo? 

“Kwanini mnajitengenezea maadui kwa vyeo mlivyonavyo? Unafanya Tanesco ambalo ni shirika zuri la nchi linaonekana ni shirika ambalo ni baya la hovyo. Akisimama mtu wa Tanesco mahali popote, watu wanaanza kucheka utafikiri kasimama ‘comedian’ (mchekeshaji), kwa nini? 

‘Ni kwa sababu ya ‘character’ (tabia) za watu wa mle ndani. “Kumpelekea mtu nguzo mpaka akupe hela, na wananchi wapo wanaojua kushawishi.

“Atakushawishi kwa haraka zake anakwambia, ‘bwana nisaidie niwekee nguzo hapa haraka kuna milioni hapa.’

“Siku nguzo imesimama atakumbuka milioni yake na atakwenda kwa wengine kuwaambia wale jamaa hawapeleki nguzo mpaka milioni, unahangaika hapa, mimi nilivyomgonga milioni, mbona kesho yake ilifika. Tunaonekana wote humu wapiga dili,” anasema.

Hapo anatoa rai kwamba, viongozi wote wanaochaguliwa au kuteuliwa, wana jukumu la kuwatumikia wananchi wanaowaongoza na kuhakikisha nafasi walizo nazo zinakuwa daraja la kufanikisha maendeleo badala ya kukwamisha.

Pia, anahimzia kuwapo wanaoelewa vyema dhana ya ‘cheo ni dhamana’, hivyo kwa wakati walionao wa kuwatumikia wananchi, wanatimiza wajibu wao kikamilifu na kwa moyo wa uwajibikaji na uzalendo mkubwa. 

Anatumia methalli na usemi; “cheo ni kama koti la kuazima ambalo kwa kuwa lieazimwa, ni lazima likarudishwa kwa wenyewe. Hivyo, lahitaji unyenyekevu katika kuwatumikia wananchi.” 

Eneo jingine analolitaja Dk. Biteko, ni kuwapo baadhi watu ambao kwao cheo ni fimbo ya kuwachapa wengine, hivyo anawataka kuuonyesha umuhimu wa nafasi zao kuwakwamisha wengine. 

Anakumbusha kuwa, viongozi wanaotumia nafasi zao kuwaumiza wengine wanapaswa kubadilika, kwani cheo ni dhamana. 

Vilevile anasema kwa watumishi wa umma waliopewa dhamana kuwatumikia wananchi, wapo wanaowajibika, pia wapo wanaokwamisha wengine kwa nafasi walizonazo. 

Ni nafasi inakumbusha mshahara wanaolipwa viongozi wanavyofurahia, hata usafiri wanatumia (kama upo), vinatokana na kodi za wananchi wanaovuja jasho kuwatumikia. 

Kimsingi, anawachambua waajiri wao halisi, kuwa ni wa wananchi na si watu kusukumwa, bali wanatakiwa wautumikie umma. 

Kwa lugha nyingine, ni ufafanuzi kwamba walioko kwenye ofisi za umma wajue wao ndio watumwa wa wananchi na si kufikiri kwamba wananchi wanapaswa kuwatumikia wao. 

Biteko alipokuwa Waziri wa Madini, alishawakumbusha wakurugenzi ndani ya wizara hiyo kuacha kuwanyima magari watumishi wa ngazi za chini pindi wanapokuwa na ziara za kikazi, bali magari husika wayatumie kwa wakati kufanakisha kazi ya msingi, wasikwamishe maendeleo.

Inakumbuishwa mara zote, huduma bora kwa wananchi ni mkazo unaohimizwa na Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi mahiri wa Dk. Samia Suluhu Hassan. 

·      Mwandishi ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko wilaya ya Kongwa, mkoani Dodoma. Kwa maoni, piga simu: +255 620 800 462.