BENJAMINI MKAPA- 1938/2020 Ni kiongozi shujaa ndani na nje asiyeweza kusahaulika

By Restuta James , Nipashe
Published at 09:52 AM Jul 24 2024
Benjamin Mkapa na Rais wa Afrika Kusini Nelson Mandela (kulia) enzi za uhai wao, wakiwa Dar es Salaam, mwaka 1998.
PICHA: MTANDAO
Benjamin Mkapa na Rais wa Afrika Kusini Nelson Mandela (kulia) enzi za uhai wao, wakiwa Dar es Salaam, mwaka 1998.

NI miaka minne tangu Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, afariki dunia Julai 24, 2020.

Kumbukumbu ya kifo chake inafanyika ukiwa umesalia mwaka mmoja kumalizika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, aliyoiasisi, ikiwa na kauli mbiu ya kufikia maisha bora kwa kila Mtanzania.

Katika mahojiano na Nipashe, aliyekuwa mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Donath Olomi, anaelezea safari ya dira hiyo na kazi kubwa iliyofanywa na uongozi wa Mkapa.

Anasema miongoni mwa malengo ya Dira 2025, ilikuwa ni kuwa na taifa la watu walioelimika na wanaotafuta maarifa kupitia elimu.

“Juhudi zimefanyika, changamoto  ni kwenye ubora wa elimu. Watu wengi wanasoma hadi chuo kikuu lakini kiwango cha uelimishaji nina mashaka siyo kile tulichokitaka kwenye dira,” anasema.

Anaongeza kuwa dira ilitamani Tanzania ya watu walioelimika na wanaojielimisha, wanaotumia sayansi na teknolojia kujiendeleza na kufikia uchumi wa kati.

“Utafutaji wa maarifa bado sana. Ni mojawapo ya eneo linalohitaji kufanyiwa kazi. Tunaona watu wanasoma ili kupata vyeti lakini ile tabia ya watu kujielimisha bado. Ni eneo la kuwekewa mkazo kwenye Dira 2050.”

Akiangazia zaidi sekta hiyo, Dk. Olomi anasema imepanuka sana ikilinganishwa na mwaka 2000, akitaja ongezeko la shule za msingi, sekondari, vyuo vya kati na vikuu.

“Tumejitahidi kupanua elimu, japo  tuna changamoto kubwa huko mbele kwa sababu miaka 10 ijayo idadi ya watoto wanaotakiwa kwenda shule itakuwa mara mbili ya sasa, kuna ongezeko la watu hasa vijana na hivyo tunahitaji kupanua wigo wa upatikanaji wa elimu,” anasema.

Anasisitiza pia kuongeza ubora ili wahitimu wanapotoka ngazi moja kwenda nyingine wawe na maarifa ya kutosha.

 “Tumewekeza kwenye miundombinu ni jambo muhimu sana. Lakini kubwa zaidi katika ukuzaji wa jamii na uchumi elimu inayopatikana iwe bora," anasisitiza.

Dk. Olomi ambaye ni mtaalamu wa uchumi, anafafanua kuwa iwe ni elimu inayompa kijana maisha siyo matarajio bila kumpatia zana za kuweza kupambana na maisha na zama hizi ambazo tatizo kubwa la ajira, hivyo elimu imwezesha kijana kujitafuta.

“Katika kutafuta maarifa bado sana. Ni moja ya eneo linalohitaji kuwekewa mkakati kwenye dira 2050 ili tuweze kuwa na taifa la watu walioelimika, wenye maarifa yanayowasaidia wao na dunia,” anasema na kuongeza kuwa elimu iwafanye watu kusoma na kuelimika siyo kupata vyeti.

MAISHA BORA 

Akizungumzia suala hilo, anasema dira inayotimiza miaka 25 mwakani, pamoja na mambo mengine, ililenga kumletea kila Mtanzania maisha bora na kufungua uchumi wa soko ili bidhaa zipatikane kwa unafuu na kiushindani.

“Siyo uchumi wa kati  tulionao…dira ilitaka tuwe juu yake. Hatujafika na mwaka kesho ndio tunamaliza miaka 25, lakini naweza kusema tunapopanga kujiwekea malengo ni lazima yawe makubwa, japokuwa kwenye utekelezaji tunaweza tusiyafikie,” anasema, akigusia kuwa Tanzania ingeweza kuwa mbali zaidi kuliko hapa ilipofikia.

Anagusia miundombinu ya usafiri na usafirishaji pamoja na  huduma za kijamii kama afya, kuwa inahitaji kuimarishwa zaidi dira ijayo, ili kurahisisha upatikanaji wa huduma na mtangamano wa watu na bidhaa yakiwamo mazao na malighafi kutoka sehemu zote za nchi.

Dk. Olomi anasema Tanzania imeendelea, vijijini kuna mabadiliko makubwa zikiwamo nyumba za kisasa, zenye umeme na pia nchi imejitosheleza kwa chakula.

Hata hivyo, anasema mkazo unapaswa kuwekwa ili utoshelevu wa chakula uondoe udumavu kwa watoto, utapiamlo na lishe duni kwa wote.

Takwimu za serikali zinaonyesha kuwa kiwango cha udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano ni kikubwa huku Njombe ukiongoza kwa asilimia 50.4, ikifuata Rukwa kwa  asilimia 49.8 wakati kiwango cha kitaifa ni asilimia 30 kwa mwaka 2022 ikilinganishwa na asilimia 34 mwaka 2015.

UTAWALA BORA, RUSHWA

Kuhusu utawala bora, anasema ili uonekane katika ngazi zote, ni lazima kutokomeza rushwa.

 “Rushwa inakwenda na jinsi ambavyo tunafanya siasa, ikishaanzia kwenye siasa hakuna  wa kuipiga vita. Ni tatizo kubwa sana linakwaza uchumi na sekta zote pia usalama wa nchi,” anaonya Dk. Olomi, ambaye alikuwa mmoja wa wataalamu walioandika Dira 2025.

Anasema rushwa ni pamoja na ‘wananchi masikini’ kuchanga fedha za kununua ‘wapigakura’ wakati wa mchakato wa uteuzi.

Akizungumzia uchaguzi huru na wa haki, anakumbusha kauli ya ushindi  ‘nje ya boksi’ iliyotolewa na aliyekuwa Waziri Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, aliyeahidi kwamba angemsaidia Mbunge wa Bukoba Mjini (CCM), Stephen Byabato, ashinde ubunge mwakani kwa madai kuwa ushindi wa uchaguzi hautegemei wingi wa kura kwenye boksi bali anayehesabu na kutangaza matokeo.

Uteuzi wa Nape umetenguliwa na CCM imejitenga na kauli hiyo kwa kueleza kuwa itaheshimu matokeo halali ya chaguzi zote ukiwa wa serikali za mitaa mwaka huu na mkuu mwakani.

Dk. Olomi anaonya: “Watu wanasikiliza na wanajazwa presha ya hasira kidogo kidogo, mwisho linakuwa jambo baya kwenye nchi yetu.”

Kuhusu matumizi ya rasilimali, Dk. Olomi anashauri katika miaka 25 ijayo, dira mpya isisitize tathmini na namna ya kuzitumia ikiwamo matumizi ya dawa za asili na uhifadhi wa lugha na maarifa asilia kwa manufaa ya nchi na dunia.

MKAPA/DIRA 2025

Mkapa aliongoza nchi kuanzia  1995 hadi 2005 na katika kipindi hicho, aliandaa na kuanza kusimamia utekelezaji wake. Alifariki dunia Julai 24, 2020 jijini Dar es Salaam alipokuwa akitibiwa.