AKIDAI DANADANA YA MWAJIRI...Mwalimu aliyeibukia kambi ya Makonda, asimulia shida akili ‘imesomba’ ajira yake

By Beatrice Shayo , Nipashe
Published at 07:11 AM Jul 18 2024
Mwalimu Ndeitoi Laizer.
PICHA: BEATRICE SHAYO
Mwalimu Ndeitoi Laizer.

IKIWA sehemu ya yaliyojiri katika Kambi Tiba ya Makonda jijini Arusha, fuatilia simulizi ya aliyetibiwa, mwalimu anayesumbuliwa na shida ya maradhi akili. Endelea

“Nilitoka kazini nikajikuta siitaki hii kazi nalala nyumbani nakosa amani, naona kuna watu wananitisha, watu wa kazini kwangu wananisema vibaya napata na hofu ya kifo sikuwa najua kama nina tatizo la akili,” ni maneno ya Mwalimu Ndeitoi Laizer. 

Huyo amekuwa akifundisha katika Shule ya Msingi Mkapa, katika Halmashauri ya Musoma, Kata ya Bukima Kijiji cha Kastamu mkoani Mara.  

Anajitambulisha kuwa mtaalamu wa masomo ya Sayansi, Hisabati na Kiingereza, anafundisha kuanzia darasa la tatu hadi la saba.

“Kutokutulia sehemu moja ninakuwa ni mtu wa kukimbia kimbia, sauti zinanitisha! Ninakuwa ni mtu mwenye hofu ya kuuawa, kila ninapokaa najiona kama sipo salama wakati mwingine nahisi watu wananisema hata nikilala usiku nahisi watu wananiongelea vibaya,” anaeleza. 

Mnamo Juni 30, mwaka huu, alijitokeza kwenye kambi maalum ya madaktari bingwa iliyokuwa inatoa huduma mkoani Arusha na akapatiwa matibabu.

Anasimulia namna mwaka 2018 alianza kuwa na tatizo hilo akiwa anatoka kazini, baada ya kufika nyumbani alifanya uamuzi wa kuacha kazi kutokana na vitisho alivyokuwa ‘anaviona’.  

Mwalimu Laizer, aliyeajiriwa katika shule hiyo Februari mwaka 2012, anasema baada ya kufika Arusha, bado wazazi wake hawakuweza kugundua tatizo lake mapema, akawa anafungwa kamba. 

“Walinifunga kamba wakiwa wanadhani nimelogwa. Kuna daktari mmoja wa Hospitali Levolosi, iliyopo jijini Arusha alianza kunipatia huduma ya afya yangu na ikatengamaa,” anasema. 

Anasema alivyopata nafuu mwaka 2021 alirudi shuleni kwake kuendelea na kazi hakupatiwa ushirikiano, akinena akaishia kuzungushwa bila ya majibu sahihi. 

“Niliambiwa kuna barua ya kufukuzwa kazi imeandikwa, ipo kwenye faili, kwa sababu hawakuwa na taarifa zangu na hii barua haikuweza kunifikia,” anasema Laizer. 

Mwalimu Ndeitoi Laizer. PICHA: BEATRICE SHAYO

Laizer anasema, mwaka jana alienda kufuatilia barua hiyo haikuwapo, akifafanua majibu halisi kuwa: “Niliambiwa kitaitwa kikao cha kunijadili taarifa zangu, zikifika makao makuu Dodoma, waniite kwao nikajieleze. 

“Ndio nasubiri mpaka sasa sijapatiwa majibu na nina familia, hii changamoto imenirudia, ndio maana nikaja kuonana na wataalamu katika hii Kambi ya Makonda.” 

TATIZO LAMRUDIA 

“Hii hali ilinifanya nije kuonana na daktari wa kambi ya matibabu bure, baada ya mke wangu kusikia hilo tangazo akanileta Juni 29 mwaka huu, nikafanyiwa vipimo...,” anaeleza. 

Anasema changamoto anayopata ni kuzipata dawa alizoandikiwa, kutokana na kuwapo foleni kubwa hata  inamlazimu kurudi siku inayofuata na bado hakufanikiwa kutokana na umati kuongezeka katika dirisha la dawa. 

Laizer anasema, akaamua kwenda kukopa Sh. 7,000 kwa jirani yake za kuzinunua dawa hizo anazotumia sasa, akiendelea: “Hizi dawa nazitumia mpaka sasa zimenisaidia.  

“Ndio maana umeona nimeweza kupangilia vizuri maelezo yangu tunavyozungumza awali hali hiyo inavyonitokea nashindwa kupangilia maelezo yangu vizuri,” anasema Laizer. 

MSHAHARA KUSITISHWA  

Laizer anaeleza barua ya kufukuzwa shuleni hadi sasa, hajapatiwa na mshahara ulisitishwa baada ya mwezi mmoja kuondoka kazini.

 “Nakumbuka waliacha kunipa mshahara kati ya Juni au Julai mwaka 2018 baada ya mimi kuondoka ndani ya mwezi mmoja nilifutwa mshahara wangu mpaka sasa sijajua hatima yangu,” anasema. 

Anasema tangu mwaka jana alivyoandika maelezo, alitegemea angepatiwa taarifa ya matokeo yake, hadi sasa hakuna alichojulishwa, hata kumsababishia msongo wa mawazo. 

NAMNA UGONJWA UNAVYOANZA

Msaikolojia Tiba wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Alex Ndagabwene, aliyempatia matibabu, akiutaja kitaalamu ugonjwa unaomsumbua mwalimu huyo. 

Anasema ni kundi mojawapo katika ugonjwa wa akili, asilimia kubwa inavyojionyesha imetawaliwa na imani, ambazo sio za kweli.

Ndagabwene anafafanua, huwa anapatwa na hali ya kujiona yupo katika mateso au kujihisi kuna wanaomchunguza maisha yake.

Anaeleza ni ugonjwa unaoambatana na dalili kubwa za imani zisizo za kweli, akiamini kwa asilimia 100 ni za kweli.

 “Yeye anaweza kuamini kuna watu wanamfuatilia ama wapo watu wenye lengo baya na yeye, ni imani imara isiyotikisika anayoiamini lakini jambo hilo halipo. Ni imani ya kuhisi anatendewa uovu ama yuko hatarini kuangamizwa akishaamini hilo ni ameamini,” anasema.

 Mtaalamu huyo, anafafanua dalili nyinginezo ni kuwa na ‘maruweruwe’ kuona vitu ambavyo mwingine havioni au kuona watu anaowajua, hawapo katika eneo alilopo.

Anazifafanua hisia hizo ni mtu kuona vya kutisha, mwingine hawezi kuviona, huku akisikia sauti zikimsemesha.

Kusikia sauti na hali za kutisha, ni hali anayoitaja inaweza kumsababishia kushindwa kuhudhuria matukio ya kijamii akijiona hayupo salama.

Ndagabwene anatoa mfano wa mwanafunzi, kuacha masomo ghafla akiamini kuna vitu vibaya vinaendelea dhidi yake, au anafuatiliwa na watu chuoni bila kuwa na uthibitisho sahihi.

 “Anaweza kuhisi wanafunzi na walimu wapo pamoja kutaka kumfanyia kitu kibaya na kwenda kutoa taarifa hata kituo cha polisi kueleza kuna watu wanamfuatilia ila kwenye kuthibitisha kina nani hawezi kuwajua,”anasema.

 Mtaalamu huyo anaeleza, mamlaka hiyo inaposhindwa kuchukua hatua kwa alichokieleza, anajenga imani nayo inashirikiana na madau tajwa, akifafanua kwa kauli:

“Kama yupo kazini ataacha na wengi wameacha shule kwa mtindo huo.”

 Mtaalamu huyo anasema, baadhi yao hupelekwa kutibiwa kwa mganga wa asilia au wanauombewa shida hiyo ya afya ya akili na katika uhaliia, mtu anapoacha kazi ndani ya saa 24 hadia 48 akiondoka bila ya taarifa, inaacha ujumbe umeongezeka maradufu.

 UGONGWA UNAVYOTIBIKA  

Anasema ugonjwa una tiba na mgonjwa anaweza kurudi kazini kuendelea na majukumu yake, huku akitumia dawa kwa usahihi na kuhudhuria kliniki anazopangiwa. 

Ngagabwene anasema kuna waliotibiwa na wanaendelea na shughuli zao, bila ya changamoto, ili mradi wanafuata  maelekezo ya wataalamu. 

“Matibabu yapo ya dawa ambayo yanaenda kutuliza maruweruwe ya vitu anavyoviona vya kutisha ama imani potofu iliyojengeka na kupunguza ama kuondoa sauti azisikiazo bila uwepo wa watu halisi.  

“Kuna matibabu ya kisaikolojia yanayosaidia kuzitikisa zile imani anazokuwa nazo, ama kutambua dalili zinavyoanza na kuchukua hatua mapema, bila kusahau  kujifunza namna nzuri ya kutatua changamoto za kimaisha na kuepukana na vichochezi vya ugonjwa.” 

SABABU ZA UGONJWA

Ndagabwene anasema sababu za ugonjwa huo wa akili kuwa unasababishwa na vitu vitatu ambazo ni vinasaba, kisaikolojia na mazingira aliyopitia mgonjwa bila kusahau matumizi mabaya ya vilevi kama vile bangi na pombe.

Anasema, ugonjwa huo kuna wanaorithi kutoka kwenye familia na sayansi inaeleza hata mazingira magumu mtu aliyopita, yana mchango katika hali hiyo.

 “Tulikuwa tunaomba uongozi wa mkoa (Mara na Arusha) kumsaidia mwalimu huyu arudi kazini kwa kufuata taratibu zinazohitajika tutashukuru kwa kuwa ugonjwa huu ulimuanzia akiwa kazini,” anatamka msaikolojia. 

MKE ASIMULIA

Mke wa mwalimu huyo, Neema Laizer, anasema anasimulia namna mume wake alivyorejea akimtamkia ameacha kazi na alivyomuuliza sababu, akamjulisha ‘anahofia kifo’. 

“Hakunipa taarifa kama anakuja Arusha. Nilishangaa kumuona ananiambia kaacha kazi, nikamuuliza kwanini? Akanimbia sitaki kwenda kazini, ninahofia kifo changu,” anasema. 

Neema, anasema hawakugundua ugonjwa unaomsumbua, mpaka walipoenda hospitali na kukutana na mtaalamu aliyewapatia dawa na afya yake kurejea vizuri. 

Pia anaeleza mwaka 2021, mumewe akamwambia anaenda shuleni kufuatilia kinachoendelea na hakupatiwa majibu yanayoeleweka, ikimlazimu mwaka jana kwenda kumsaidia kufuatilia kwa pamoja.    

Anasema, walikaa mwezi mmoja wakifuatilia wakamwambia aandike barua hakuna majibu waliyopatiwa hadi sasa na kujikuta wanaendelea kuishi katika wakati mgumu. 

“Familia ina mahitaji mengi tunapata shida kupata huduma za hospitali bima tumesitishiwa kuzitumia chakula mpaka apate kibarua cha kwenda kufanya na mafundi,” anasemaNeema anasema kwa sasa ana mtoto mchanga, hana biashara anayoifanya, hivyo kilio chake ni kurejea familia ipate mahitaji yake. 

“Natamani angerudishwa katika nafasi yake, ili aweze kuwalea hawa watoto changamoto katika chakula mpaka ‘abangaize’, hii ndio inanipa shida, maana mimi sina kazi nipo nyumbani,” anasema. 

Aidha, anasema kwa sasa hali yake ipo vizuri angerudishwa kazini huo ugonjwa sio kwamba unamtokea kila mara, baada ya mwaka 2018 haukutokea hadi mwaka huu. 

Mama huiyo anasema, kuna kipindi aliacha kutumia dawa akiwa yupo vizuri, hata akashangaa mwaka huu ugonjwa huo ukamrudia. 

“Kikubwa anachokilalamikia ni kuwaza kazi yake anasema haelewi amepotezaje kazi yake hicho ndio anachokisema mara kwa mara anawasiliana na wenzake wa Musoma hawampi ushirikiano,” anasema.