2024 unavyowapa wapinzani mawazo yasiyoisha

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:59 AM Dec 18 2024
Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na mabalozi wanaowakilisha nchi zao.
PICHA: IKULU
Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na mabalozi wanaowakilisha nchi zao.

MWAKA 2024 unaelekea ukingoni ukibakiza wiki mbili za kuuhitimisha ifikapo Jumatano Desemba 31 saa sita usiku. Unapomalizika, unakumbukwa kwa matukio mbalimbali yaliyojiri kwenye kipindi chote cha siku 365 na robo ambayo ni sifa ya mwaka mrefu.

Tukio muhimu kwa mwaka huu linalojiri kwenye siasa ni uchaguzi wa serikali za mitaa unaofanyika Novemba 27 na kusababisha gumzo kwa vyama vya upinzani baada ya CCM kuviacha mbali ikizoa viti vingi.
 
 Itakumbukwa malalamiko ya vyama vya upinzani yanaanzia kwenye mchakato wa kuandikisha wapigakura kwenye daftari la mkazi, ukuchukuaji  na urejeshaji wa fomu na hata wakati wa uchaguzi yakaibuka malalamiko likiwamo sakata la baadhi ya mawakala kuzuiwa kuingia katika vituo vya kupigia kura.
 
Inadaiwa na upinzani kuwa baadhi ya wagombea wao walinyimwa fomu, huku waliobahatika kuzipata, wakishindwa kuzirejesha baada ya kuzijaza kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni watendaji kufunga ofisi.
 

Lakini baadhi ya waliobahatika kurejesha fomu hizo, wakawekewa mapingamizi yakiwamo ya kukosea umri wao wengine wakidaiwa kuandika wana miaka 400 badala ya 40 na majina mfano Salim kusomeka Salama wakati jinsi ni mwanaume, hivyo kujikuta wakiwa nje ya ulingo huku wachache wakibahatika kupenya.
 
 Hicho walichokiita 'figisu' kilisababisha CCM kupata ushindi wa wenyeviti wa serikali za vijiji kwa nafasi ya viti 12,150 sawa na asilimia 99.01. Waziri wa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa ndiye aliyatangaza matokeo hayo.
 
 Matokeo hayo yaliyoacha vidonda vyenye maumivi kwa upinzani, Mchengerwa akitangaza matokeo  anasema CHADEMA ilipata viti 97 sawa na asilimia 0.79 na kwamba vitongoji nane wagombea wake walifariki dunia.
 
 Anataja maeneo ambayo wagombea walifariki baada ya uteuzi kuwa ni halmashauri za wilaya za Kilwa (2), Nanyumbu (1), Itilima (1), Ikungi (1), Manyoni (1), Uyui (1) na Mbarali na kwamba uchaguzi utafanyika tena.
 
 Chama cha ACT-Wazalendo, kilipata viti 11, wakati CUF imebeba jumla ya viti 10, NCCR Mageuzi kiti kimoja.

 Katika nafasi za mwenyekiti wa kitongoji anasema CCM ilishinda nafasi 62,728, CHADEMA nafasi 853 huku ACT-Wazalendo ikishinda nafasi 150, CUF nafasi 78, NCCR -Mageuzi imeshinda nafasi 10.

 Aidha, anasema UDP ilishinda nafasi sita, UMD nafasi mbili na ADC nafasi moja.

Mwenyekiti wa mtaa, Waziri anasema CCM ilishinda viti 4213 sawa na asilimia 98.83 huku CHADEMA ikishinda nafasi 36 sawa na asilimia 0.84, ACT Wazalendo nafasi tisa sawa na asilimia 0.21, CUF  nafasi 4 sawa na asilimia 0.09 na CHAUMA nafasi moja sawa na asilimia 0.02.

 OMBI LA CCM
 
 Wiki chache kabla ya uchaguzi huo, Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Emmanuel Nchimbi kwa niaba ya chama chake anatoa wito kwa Wizara ya TAMISEMI kupuuza makosa madogo madogo katika hatua ya mwisho ya kusikiliza rufaa za mapingamizi.
 
 Katibu Mkuu huyo anatoa ombi hilo kwa lengo la kuwapa Watanzania wengi zaidi nafasi ya kugombea kwenye uchaguzi huo ili kutoa hamasa ya demokrasia kuendelea kukua nchini.
 
 "Natoa wito wa CCM kwa waziri mwenye dhamana na serikali za mitaa, kwamba tunatambua wamefuata sheria, lakini ni muhimu kukumbuka kwamba demokrasia yetu bado ni changa inahitaji kukua, tutachukua muda kujifunza makosa yataendelea kupungua, tunaiomba TAMISEMI katika hatua ya mwisho ya rufani kuyapuuza makosa madogomadogo, ili Watanzania wengi zaidi wapate nafasi ya kugombea. Msimamo wa CCM ni huu na nasisitiza msimamo huu ninaoutoa una baraka za Mwenyekiti wa CCM, Samia Suluhu Hassan”.
 
 Kauli hiyo ya Dk. Nchimbi inatokana na malalamiko ya vyama vya upinzani vikiwamo CHADEMA, ACT na CUF kulalamikia majina ya wagombea wao kuenguliwa kwa sababu mbalimbali.
 
Baadaye Waziri wa TAMISEMI Mchengerwa anaagiza wenye malalamiko kupeleka mapingamizi ambapo yaliwasilishwa kwa hatua ya kusikilizwa rufani za wagombea walioenguliwa.
 

Hata hivyo, uchaguzi ulimalizika kwa kilio ambacho na sasa vyama vikuu vya upinzani kikiwamo cha ACT-Wazalendo kimetangaza kutoutambua uchaguzi huo.
 
MATAMANIO YA RAIS
 
Mwanzoni mwa mwaka huu katika sherehe za kuukaribisha mwaka huu ziitwazo (Diplomatic Sherry Party), Rais Samia Suluhu Hassan, anaahidi kuwa  haki, demokrasia, sheria na utawala bora vitadumishwa wakati wote wa uchaguzi wa serikali za mitaa.
 
Anasema hayo kwa mabalozi wanaliopo Tanzania wanaoziwakilisha nchi zao pamoja na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, kwamba ili kuwa na uchaguzi huru na haki, kikosi kazi huru cha kupitia na kushauri mageuzi muhimu katika mfumo wa siasa kiliundwa na  kiliwasilisha ripoti yake mwaka 2023.
 
 Kwa mujibu wa Rais, mapendekezo mengi ya kikosi kazi yaliyopokelewa na serikali na wadau wote, yalihusu kuongeza uwazi katika mchakato wa uchaguzi ikiwa ni pamoja na uteuzi wa mwenyekiti wa tume ya uchaguzi.
 
Lakini anasema masuala machache hayakupokelewa moja kwa moja  
 ambayo yalikuwa kinyume na katiba, na kwamba yanaweza kuchukuliwa wakati wa mchakato wa katiba.
 
Anasema serikali itaendeleza ushirikiano na balozi hizo kwa mujibu wa katiba, tunu za taifa, usawa, umoja na mshikamano wa kitaifa, lakini akawataka mabalozi hao kutoingilia uchaguzi na kuzingatia mila, kanuni na maadili ya kidiplomasia.