Wagombea vijana TLS kupambana na vishoka

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 01:05 PM Jul 22 2024
Wakili Revocatus Kuuli
Picha: Mpigapicha Wetu
Wakili Revocatus Kuuli

WAGOMBEA nafasi ya urais na uenyekiti, mawakili vijana kutoka Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), wamejinadi kurudisha chama hicho kuwa na nguvu ya awali kwa kutimiza misingi halali ya uchaguzi na kuondokana na vishoka katika taaluma hiyo.

Baadhi ya wagombea wa nafasi ya urais TLS, walisema hayo walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya ofisi hizo jijini Dar es Salaam baada ya kumalizika kwa mdahalo uliowakutanisha wagombea hao.

Wakili Revocatus Kuuli, alisema kuna baadhi ya watu wanakiona chama hicho kupoteza ubora, lakini wagombea ambao tunagombea sasa tumeweka mikakati ya kukirudisha chama kuwa na nguvu na kutekeleza misingi iliyojiwekea chama.

Alisema chama kikipoteza misingi na kukosa watu makini, lazima kitayumba na dhamira ya wagombea wajao ni kukirudisha kiwe katika misingi imara.

Naye Wakili Sweetbert Nkuba, alisema kama atapata dhamana ya kukiongoza chama hicho atahakikisha atasambaratisha vishoka walioko kwenye taaluma hiyo ambao hawajasomea sheria.

Alifafanua atahakikisha mawakili wote wanasajiliwa katika chama ili kugundua wababaishaji kwa kutaka kutambua waliposajiliwa, ofisi zao zitambulike kisheria ili kuwabaini wale wababaishaji wasio na ofisi wazuiwe wasifanye kazi za uwakili.

“Kuna baadhi ya watu wanaojiita mawakili wanafanyia kazi zao za uwakili hata baa, sasa hao mimi nikipata dhamana tutacheza nao kwa maana wanaharibu taaluma,” alisema.

Alisema kuimarisha TLS kunatakiwa kuwe na sauti moja ambayo kitaimarisha chama na ikiwamo na kupatikana viongozi wenye umakini na dhamira thabiti ya kusimamisha chama na si ujanja ujanja.

Aidha, alisema akipata dhamana atahakikisha anasaidia mawakili vijana chipukizi wasitozwe ada nyingi kuwa mawakili, kuwajengea weledi kwa kuwa mawakili wengi wanashindwa kutekeleza kazi zao kwa kukosa mitaji na maeneo ya kufanyia kazi.

“Nitahakikisha kupatikana kwa maslahi ya mawakili, bima ya afya na bima ya maisha kwa mawakili, vituo vya malezi kwa mawakili vijana pamoja na kuboresha mahusiano na kuunganisha mawakili na taasisi muhimu za serikali ikiwamo mahakama na jamii,” alifafanua.

Naye mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa mawakili vijana, wakili Denis Bwana alisema kwa kupitia Sheria namba 307 ya Bunge katika kifungu cha nne, TLS ina wajibu kuishauri serikali, kuishauri Bunge TLS kuwa ni chombo cha mfano katika jamii kwa kusaidia masuala ya kisheria nchini.

Alisema, wagombea vijana hawaridhishwi na mwenendo wa TLS kwa kuwa imepoteza hadhi yake na ilivyo sasa na kumekuwa na minong’ono mingi kwa kuonekana kuwa imeshikiliwa kutokana na kushindwa kujisimamia.

“Tunahitaji viongozi sahihi TLS isimame kama tutashindwa kujisimamia wenyewe tutawezaje kusimamia chaguzi zijazo, tunatakiwa tuwe mfano hata katika chaguzi zetu za ndani ili hata vyama vya siasa vituangalie sisi, kuachana na uchaguzi wa ubabaishaji,” alisema.

Jumla ya wagombea watano wamejikita katika kinyang’anyiro cha kugombea urais TLS na uchaguzi unatarajiwa kufanyika Agosti 2, mwaka huu mkoani Dodoma.